Bi.
Arodia Gebasaki ambaye ni mjane akisimulia jinsi mila ya kutakasa
wajane inavyofanyika kwa mwandishi wa makala haya (hayupo pichani)
ambapo yeye alikataa kufanyiwa mila hiyo na hakuna madhara yoyote
aliyopata tangu kufiwa na mume wake, miaka 14 iliyopita
Baadhi
ya wajane wakiwa katika picha ya pamoja na mwandishi wa makala haya
baada ya kufanya mahojiano kuhusu mila ya kutakasa wajane wilayani
Ukerewe, Mwanza. Wajane hao wameipiga vita mila hiyo kutokana na
kumdhalilisha mwanamke.
"Udhalilishaji
huu uliojificha katika mila inayoitwa Okusomboka kwa Wakerewe ni tendo
ambalo hufanyika kwa maana ya kuhitimisha uhusiano wa ndoa kati ya mume
na mke aliyefiwa. Mila hiyo huhitaji uhusiano huo uhitimiswe hivyo
sababu ulianzishwa kwa tendo la ndoa.BIBI alibakwa,mama akabakwa, dada amebakwa na mke wangu atabakwa nitakapofariki.”
Huo ndiyo uhalifu mkubwa uliojificha kwenye mila ya Okusomboka (kutakasa) kwa wakazi wa Ukerewe hasa kwa Wakara na Wajita.Kwa Wakerewe ubakaji ni jambo la kawaida na unatukuzwa kwa mikono miwili kupitia mila ya Okusombaka.
Hayo
ndiyo maisha ya kawaida kwa wakazi wa Ukerewe mkoani Mwanza wanaotukuza
ubakaji, mbakaji anapomaliza tendo hilo, wakati mwingine anashangiliwa
kwa kupigiwa vigelegele na akina mama akionekana shujaa wa kuondoa watu
mikosi kupitia ubakaji, ingawa wao hutafsiri kuwa wanasomboka.
Ubakaji
huo kupitia mila ya Okusomboka ni sehemu ya maisha ya kawaida kwa
wakazi wa Ukerewe na unaheshimiwa kiasi kwamba wale wanaokataa kubakwa
wanatengwa na kunyooshewa vidole kila wanapopita.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza juu ya mila
ya Okusomboka (utakasaji) umebainisha vitendo vya ubakaji vimekuwa
vikitendeka tangu enzi na enzi na kuingia katika karne hii ya sayansi na
teknolojia.
Ambapo
ubakaji huo, unalenga wanawake wajane na unafanyika siku ya nne ya
matanga tangu kutokea kifo cha mwanaume ndani ya familia.Bila
kujali uchungu anaokuwa nao mjane wa kupoteza mume wake, anatafutiwa
mbakaji (Omwesya-yaani mtakasaji) ambaye anakodiwa na kulipwa ujira ili
kutekeleza kitendo hicho cha kubaka mjane, ambacho kwa Ukerewe ni cha
heshima, katika kuhitimisha uhusiano kati ya mume aliyekufa na mjane
aliyebaki.
Ingawa
sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka 1998 inatoa adhabu kali kwa
watu wanaopatikana na hatia ya makosa ya ubakaji, kwa Ukerewe hawajui
kama Okusomboka ni kubaka, hivyo kukiuka wazi wazi sheria hiyo
inayotolewa kwa watu wanaofanya vitendo hivyo.
Ubakaji
unafanyika kwa uwazi na wameenda mbele zaidi kwani kuna watu maalumu
ambao wanalipwa fedha na wakati mwingine hata mifugo kwa ajili ya
kuwabaka wanawake wanaofiwa na waume zao kwa hoja kwamba wanatimiza
sharti la mila hiyo.
Mbakaji
kabla ya kuanza kitendo hicho, huwa anaandaliwa chakula maalumu ikiwemo
pombe ambayo huwa anakunywa na kuchangamka na hapo ndipo anaaza kubaka.
Kutokana
na hali hiyo wanawake wengi walioolewa wilayani Ukerewe ni wabakwaji
watarajiwa na wale watakao kataa kubakwa, basi wajiandae kutengwa na
ndugu, kunyooshewa vidole na jamii inayowazunguka na mali za marehemu
waume zao kutotolewa urithi.
Pia, mjane anayekataa kutakaswa ajiandae kutopata mwanaume wa kumuoa.
Vi
kwa z o h i v y o , n d i v y o vinavyowashinikiza wakubali kubakwa na
watu maalumu ambao hukodiwa kwa fedha au kulipwa mifungo kwa ajili ya
kubaka wajane.
Katika
mila hii, mwanamke analazimishwa kufanya tendo la ndoa bila ridhaa yake
tena na mtu asiyemfahamu na haandaliwi kwa namna yoyote ile kwa ajili
ya tendo hilo.
Wakati kwenye majumba ya utakasaji unafanyikwa kwa njia ya maombi, kwa Ukerewe unafanyika kwa njia ya ubakaji.
Okusomboka
ni tendo la ndoa linalohusisha watu wawili, mjane ambaye amefiwa na
mume au mke na mwingine ambaye yupo kwa ajili ya kazi hiyo.
Mfano
leo hii ikitokea mwanamke akafiwa na mume wake, baada ya mazishi
yanafanyika matanga ambapo siku ya nne ya matanga, anakodiwa mtu kutoka
miongoni mwa watu wanaokodishwa kwa ajili ya kutakasa mjane na kufanya
naye tendo la ndoa tena bila hiari ya mjane.
Ubakaji
uliojificha kwenye mila ya Okusomboka (kutakasa) kwa Wakerewe ni tendo
ambalo linafanyika kwa maana ya kuhitimisha uhusiano wa ndoa kati ya
mume na mke ulioanzishwa kwa tendo la ndoa, hivyo ni lazima uhusiano huo
uhitimishwe kwa tendo hilo kutokana na mmoja wa wanandoa kuwa
amefariki.
Utakasaji huo unafanyika kwa pande zote yaani mwanake na kwa mwanaume, lakini unatofautiana mazingira unapofanyika.
Mfano,
mwanamke anapofiwa na mume wake anakodishwa mtu maalumu wa kufanya naye
tendo la ndoa na hapo kunakuwa hakuna maridhiano yoyote kati ya
mtakaswaji na mtakasaji, bali maridhiano yanatokana na kile anacholipwa
mtakasaji ndipo anafanya tendo hilo.
Lakini,
mwanaume anapofiwa na mke wake anaenda mwenyewe mtaani kutafuta
mwanamke wa kufanya naye tendo la ndoa wakati mwingine akisindikizwa na
wapambe watakaothibitisha kwamba, alipata mwanamke na kufanya naye tendo
la ndoa, hivyo anakuwa ametakasika.
Wanafanya
hivyo, kwa kuamini kwamba, marehemu wakati anafikwa na mauti hakupata
fursa ya mwisho ya kufanya tendo la ndoa hilo na mwenzi wake.
Kwa msingi huo, wanafanya hivyo kama ishara ya kuhitimisha uhusiano wa wanandoa hao, yaani marehemu na yule aliyebaki hai.
Wakerewe wanaamini kuwa, mjane au mgane akishatakaswa ile mikosi yote iliyosababisha kifo cha marehemu inakuwa imeondolewa yote.
Pia
wanafanya hivyo kwa kuamini kwamba, marehemu wakati anafikwa na mauti
hakupata fursa ya mwisho ya kufanya tendo hilo na mwenzi wake.
Hiyo inakuwa ni ishara ya kumalizika kwa uhusiano wa wanandoa hao, yaani marehemu na yule aliyebaki hai.
UBAKAJI WENYEWE
Mmoja
wa wazee anayefahamu mila hiyo ambaye pia aliwahi kufanyiwa mila hiyo,
Juma Mtallo (83) mkazi wa Nkilizi katika Kijiji cha Mmakeke wilayani
Ukerewe, anasema pindi mwanamke anapofiwa na mumewe, kama kawaida
yanafanyika matanga kwa siku kati ya tano na saba kulingana na uwezo wa
wafiwa.
Katika kipindi hicho, mjane huyo anatakiwa kuhudumiwa na kuandaliwa chakula na mtu aliyewahi kufiwa na mwenzi wake.
“Anakuwa
ndani ya nyumba amefunikwa nguo na wanaoenda kumsalimia na kumhudumia
ikiwa ni pamoja na kumpikia chakula ni wale waliowahi kufiwa,” anasema
Mtallo.
Anasema,
kwa kipindi hicho anakuwa hajaoga. “Siku ya nne ndipo wanaanza taratibu
za kumuogesha na akishamaliza ndipo anapelekwa kwa mbakaji
(mtakasaji).”
Anaongeza
kwamba baada ya mtakasaji kumaliza kazi hiyo, anaondoka kwa majigambo
na wakati mwingine akiimba; “Wanaume wafe wanawake wabaki…wanaume wafe
wanawake wabaki,” anasema huku akiongeza huwa anaimba hivyo ili wanaume
wazidi kufa na yeye azidi kupata kazi ya kubaka wajane.
SIKU YA UBAKAJI
Kwa
mujibu wa mila hiyo, siku ya kubaka, mbakaji huwa anaandaliwa chakula
kizuri pamoja na vinywaji hasa pombe kwa gharama za familia
inayotakaswa.
Mmoja
wa wanawake waliowahi kutakaswa, Anna Sebastiane mkazi wa Tarafa ya
Ukara Kata ya Bukungu, wilayani Ukerewe anasema, siku mtakasaji
anapoenda kutakasa mjane, anapokelewa kwa heshima kubwa.
Anaeleza
kwamba wakati mwingine anaweza kumwambia mtakaswaji; “Hebu cheza nione
kama unaweza,” anasema yaani aoneshe umahiri wa kutikisa nyonga wakati
wa tendo la ndoa.
Anafafanua
kwamba, endapo ataona mjane hawezi kutikisa nyonga, anaongeza gharama.
Mfano endapo aliwatoza fedha basi atapenda aongezewe kiasi atakachoona
kinamfaa au kama ni mifugo kama vile mbuzi, atataka aongezewe mwingine
kwa jinsi atakavyoona inafaa.
Hata pale asipovutiwa sura ya mtakaswaji, mtakasaji anapandisha gharama kwa jinsi atakavyoona inafaa.
Anasema, endapo utakasaji utafanyika nyumbani kwa marehemu basi ndani ya nyumba inabidi wawepo watoto wake ambao hawajaolewa.
“Wakati
utakasaji unafanyika (ubakaji) watoto wanakuwa wanasikia jinsi Omwezya
(mtakasaji) anavyonguruma (akitoa maelekezo kwa sauti nene akimwelekeza
mjane jinsi anavyotaka alale au namna ambavyo anataka atingishe nyonga
yake) na hapo kitanda kinachokuwa kinatumika ni cha marehemu,” anasema
Sebastiane.
Anapoulizwa kama watoto wanasikia hiyo sauti? Sebastiane anacheka kwanza huku akivuta pumzi, kisha anasema;
“Sio
watoto peke yake, hata wanaokuwa nje wanafahamu kinachoendelea …si
unaona hali ya nyumba zetu (mbovu kiasi kwamba nyingi hazina faragha).
Anasema anakuwa anahimiza mtakaswaji atingishe nyonga ili apate raha.
“Watakasaji
wengine, hawakuwa na staha na tendo la ndoa, kwani walipokaribia
mshindo (kutoa mbegu za uzazi) walipiga kelele kwa kunogewa na uhondo
wakati huo huo akiashiria kwamba kazi aliyopewa amehitimisha,” anasema
na kuongeza kuwa akishamaliza anavaa nguo na kutoka nje ya nyumba kwa
mbwe mbwe kisha kulipwa chake.
Anasema,
watakasaji wengine waliondoka wakiimba; “wanaume wafe wanawake
wabaki..wanaume wa f e wa n awa k e wa b a k i . ” Anasema hiyo kwa
kufurahia kile walicholipwa. “Wakati anaondoka anapigiwa vigelegele na
akina mama kwa kufurahia kuhitimisha mila hiyo…mila hii unaweza kuiona
ni mbaya, lakini yakishakufika utaona umuhimu wake,” anasema Sebastiane.
Hata
hivyo, anasema: “ Mila hii (Okusomboka) ni aibu kwa watoto wanaokuwa
ndani ya nyumba wakisikiliza mama yao akitakaswa, huku akihimizwa
atingishe nyonga… tendo la ndoa linahitaji faragha, lakini utakasaji
hauna faragha na unamdhalilisha mwanamke,” anasema na kuongeza kuwa ni
jambo la aibu ndiyo maana tendo la ndoa linahitaji faragha.
Sebastiane anapoulizwa kama mtakasaji anatumia kondomu ili kujikinga na magonjwa, anasema jambo hilo halipo.
Pia
anasema, mtakasaji na mtakaswaji wanatakiwa wafanye tendo moja la ndoa
(yaani mshindo mmoja) na wasifanye tena tendo hilo maishani mwao, endapo
wakirudia watakuwa wamekiuka sharti la mila hiyo hivyo mikosi inaweza
kurudia familia ya mjane.
“Kwa
hiyo atalazimika atakaswe (abakwe) upya na mtakasaji mwingine,
vinginevyo wanaamini kuwa familia yake itaendelea kuandamwa na mikosi,”
anasema .
Anataja mikosi hiyo kuwa ni pamoja na familia kuandamwa na vifo na kuugua mara kwa mara.
MASHAHIDI
Mashahidi
wanaoshuhudia tukio hilo, wanasema wanakuwepo kwa ajili ya kuhakikisha
kwamba tendo hilo limefanyika, ili kuondoa wasiwasi wa wajane
kudanganya.
Mjane
mwingine, Arodia Gabaseki (64) mkazi wa Kata ya Ulagala, Tarafa ya
Masonga wilayani Ukerewe anasema mashuhuda wanakuwa nje katika mazingira
ambayo watakuwa na uhakika kuwa tendo hilo linafanyika.
Anasema
kwamba, kutokana na wajane kuogopa mikosi, lazima wakubali na kwamba
mgurumo wa mtakasaji nao kwa wakati mwingine ni ishara nzuri kwao.
Anaeleza
kwamba, mara baada ya kutakaswa anarejea nyumbani akiwa ameinamisha
kichwa chini na kupokewa kwa furaha na wanandugu waliopo kwenye matanga,
kwa kuwa wanaamini kuwa uhusiano kati ya mjane na marehemu
umehitimishwa na hakuna matatizo yoyote yanayoweza kuwapata.
SIFA YA MTAKASAJI
Ofisa
wa Taasisi ya Kuboresha Mila na Desturi katika Jamii ya Ukerewe
(KUMIDEU), taasisi ambayo inajihusisha kutoa elimu ya kutokomeza mila ya
kutakasa wajane, Musiba Kakulu anasema mtakasaji ni mtu anayeonekana
hakubaliki ndani ya jamii kutokana na matendo hayo.
Anasema,
watakasaji wengi ni walevi, wachafu, wasiokuwa na wanawake na mara
nyingi walitegemea kuendesha maisha yao kwa kutegemea malipo wanayopata
kwa njia ya utakasaji.
“Kutokana
na umuhimu wa mila ya kutakasa, mtakasaji (Omwezya) anakuwa hana
umuhimu ndani ya jamii,” anasema Kakulu. Sifa nyingine anasema ni mtu
anayejua dawa na anayependa kusimamia mila na desturi.
Pamoja
na kuwa na hali hiyo, lakini thamani yao inaonekana pale walipohitajika
kutakasa, kwani watu wenye heshima zao ndani ya jamii hawakubali kabisa
kutakasa watu ambao tena haijulikani wenzi wao wamefariki kwa magonjwa
gani.
“Mtakaswaji
kama ni bibi kikongwe, anapata shida kwani mtakasaji anatoza gharama
kubwa kama vile ng’ombe wakati uwezo anakuwa hana, lakini ndugu lazima
wachangishane ili wampate ng’ombe huyo,” anasema.
Anasema,
wakati mwingine mtakasaji anapotakiwa kwenda kwa mtakaswaji na ni mzee
sana analazimika atafutiwe usafiri hadi nyumbani kwa mjane