Watanzania watatu wameuawa hivi karibuni jijini Cape Town, Afrika ya
Kusini kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya. Watanzania hao
walipigwa risasi na kundi la watu waliokuwa wameficha nyuso zao nje ya
duka lijulikano kama Maisha Tuck Shop jumanne iliyopita katika barabara
ya Veld, Athlone, Cape Town.
Watanzania wawili walifariki papo hapo na mmoja kufia hosipitali. Mtu
mwingine, raia wa Afrika Kusini, alijeruhiwa vibaya katika shambulio
hilo. Mmiliki wa duka la Maisha Tuck, Ashim Nassoro, alisema kuwa aliona
kundi la watu wakiwa na bunduki za aina ya AK-47 na pistols wakipiga
risasi nje ya duka lake.
Bw. Nassoro alidai waliouawa walikuwa marafiki zake, alisema yeye
alikuwa nyumbani na mke wake na mtoto wake, ambapo ni karibu na duka
hilo aliposikia milio ya risasi.
“Nilikuwa ndani na nilimwambia mke na mtoto wangu walale chini mpaka
milio ya risasi iishe” alisema Nassoro na kuongeza “waliwapiga risasi
watu waliokuwa ndani ya nyumba halafu wakaenda kwenye duka. Walipiga
risasi watu wawili dukani, mmoja aliyekuwa kwenye geti na mwanamke mmoja
aliyekuwa kwenye nyumba.”
Nasroro aliongeza kuwa alikuwa anawajuwa Watanzania hao kwa sababu wote
wanatoka Tanzania na wamekuwa wakiishi pamoja tokea walipowasili Cape
Town miaka mitano iliyopita. Mtu mwingine aliyeshughudia tukio hilo
alisema kuwa waliowauwa Watanzania hao walikuwa hawana wasiwasi na
walirudi kwenye gari yao taratibu na kuondoka eneo la tukio.
Kufuatia tukio hilo, polisi ilimkamata Abdus Salaam Ebrahim ambaye ni
kiongozi wa kikundi kinachopiga vita dhidi ya uhalifu na madawa ya
kulevya nchini humo kinachojulikana kama People Against Gangsterism and
Drugs (Pagad). Abdus Salaam Ebrahim amefikishwa mahakami leo kwa
mashtaka ya mauaji.
Hata hivyo, mahakama imeyaondoa mashtaka hayo kwa muda kufuatia ombi la
mwendesha mashtaka ili kuruhusu uchunguzi zaidi kufanyika. Wakati hakimu
akiyandoa mashtaka hayo, wafuasi wa kikundi hicho cha Pagad waliokuwa
wamejazana mahakamani hapo walishangilia huku wakisema “Allahu Akbar”.
Majina ya Watanzania waliouawa hayakuwekwa kwenye charge sheet.
Pagad ni kikundi kilichoanziswa mwaka 1995 kupambana na uhalifu na
madawa ya kulevya kwenye jiji la Cape Town baada baada ya juhudi za
serikali kulegalega. Kampeni ya kikundi hiki ilianza mwaka 1996 baada
kumkamata, kumpiga na kumchoma moto hadi kufa Rashaad Staggie ambaye
alikuwa kiongozi wa kikundi cha uhalifu jijini Cape Town. Serikali ya
Afrika Kusini ilishawahi kudai huko nyuma kuwa Pagad ni kikundi cha
kigaidi baada ya kudaiwa kulipua kwa bomu hoteli ya Planet Hollywood
mwaka 1998. Hata hivyo, Pagad ilipinga kuhusika kwenye shambulio hilo.
Kikundi hiki kilipotea lakini kikaja kuibuka tena kuanzia mwaka 2011 na
kampeni yake ya kuchukua mitaa inayotawaliwa na uhalifu na biashara ya
madawa ya kulevya. Wadadisi wa mambo wanadai kuwa kurudi tena kwa Pagad
kwa gia ya kupambana na uhalifu, hasa madawa ya kulevya, itafanya hali
kuwa mbaya hasa kwenye jimbo la Western Cape.
Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la milipuko ya mabomu kwenye sehemu
zinazouza magari na pia kwenye nyumba za makazi ya watu zilizopo Athlone
na maeneo mengine jijini Cape Town. Matukio haya yamekuwa yakitokea
zaidi kwenye nyuma za makazi zinazotuhumiwa kutumika kufanyia biashara
ya madawa ya kulevya. Kikundi cha Pagad kimekanusha kujihusisha na
matukio hayo.
No comments:
Post a Comment