Pages

Translate

Tuesday, 3 December 2013

VIAZI LISHE MKOMBOZI WA UMASKINI JIJINI MWANZA

 Na Lydia Mapunda

Kama ilivyo kawaida ya misemo ya watafiti wengi wasemao mbegu bora ndio tija kwa kilimo bora.  Msemo huu umekuwa ukitimia katika vituo mbalimbali vya utafiti katika kilimo kwa kujizatiti katika tafiti za mbegu bora zenye  manufaa kwa wakulima nchini.

Mkoani Mwanza kituo cha Ukiriguru Agricultural Research Institute kimefanya utafiti na kuja na mbegu mpya ya viazi vitamu vilivyopewa jina la viazi lishe. Mbegu hizi za viazi lishe vililetwa mwaka 2002 kutoka nchini Uganda na shirika la International Potato Centre  na kufanyiwa utafiti na hatimaye sasa kanda ya ziwa wameanza kufaidi matunda yake.

Viazi vitamu ni kati ya mazao makuu ya mizizi yanayozalishwa kwa wingi  na kutumiwa kama  chakula.

Mara zote zao hilo linapewa nafasi kubwa kuzalishwa na wakulima kwa sababu linavumilia ukame na linahesabiwa kuwa ni moja kati ya mazao ya kinga ya njaa kama ilivyo kilimo cha mihogo.
 


Mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa viazi vitamu ni Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na Ruvuma japo kuwa viazi vitamu hivi hilimwa karibu katika kila mkoa hapa Tanzania

Katika Mkoa wa Mwanza viazi lishe vimeonekana kuwa mkombozi baada ya TAHEA (Tanzania Home Economics Association) kuingilia kati na kuwasaidia wakulima kutambua umuhimu wa viazi hivyo. Kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti ya Ukiriguru UARI (Ukiriguru Agricultural Research Institute), TAHEA waliamua kutoa mafunzo kwa wakulima ili waweze kujikwamua kimaendeleo na kiuchumi kupitia mbegu mpya za viazi lishe ambazo ni matokeo ya utafiti wa mbegu bora za viazi hivyo uliofanywa na UARI.
Wanawake ndio waliokuwa wakwanza kupata mafunzo hayo baada ya kuonekana wao ndio wakulima wa zao hilo kutokana na zana ya kwamba halina faida kibiashara hivyo kulimwa kwa matumizi ya chakula pekee.
Baada ya utafiti kufanyika na kupatikana aina tano ikiwa ni Ejumla, Karoti Dar, karoti C, Kabode na Jewel za mbegu mpya ambazo zimetofutiana matumizi na ustahimilivu wake, ndipo TAHEA ikawafundisha wanawakea hao kilimo bora, uvunaji bora pamoja na usindikaji ili kupata manufaa zaidi ambayo hapo awali hayakuwepo.
 
Pichani, Unga viazi lishe baada ya kuwekwa kwenye paketi tayari kwa kwenda sokoni 

Ramadhani Bundala ambaye ni afisa kilimo wa TAHEA akifafanua kazi kubwa ambayo wameifanya katika mradi huu wa kuwafundisha wakulima wa viazi kujikwamua kimaisha alisema kuwa“ wanawake wamekuwa wakielemewa sana na kazi za kulea familia huku wakijibakiza nyuma kuwa wao huwa wanalima mazao kwa ajili ya chakula hivyo tukaona ni bora tuwaelekeza wanawake hawa kuwa wanaweza wakalima viazi kama zao la biashara. Tukawaweka katika vikundi na kuwapa mbegu mpya kisha kuwafundisha kuanzia kuandaa shamba mpaka usindikaji. Huwezi amini kwa sasa kilimo hiki cha viazi kimevamiwa na wanaume baada ya kuona mafanikio walioyapata kwenye vikundi hivi.”
Bundala alisema kuwa mbali na kuwa chanzo cha mapato viazi lishe pia vina faida kubwa ikiwamo kuboresha afya hasa za watoto chini ya miaka mitano. Pia viazi lishe vyenye vitamin za aina nyingi ikiwamo vitamin A, vinasaidia watu wenye matatizo ya macho, kuboresha afya za akina mama wajawazito na wanaonyonyesha na kuongeza kinga ya mwili hasa kwa watu wanaoishi na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa upande wao wakulima, wanakikundi cha Imala buhabi cha jijini mwanza wametoa shukrani zao kwa TAHEA pamoja na Ukiriguru kwa kuwafikisha walipo kwani wanamabadiriko makubwa kimaisha tofauti na hapo awali.

Naye Bi Mwanaidi  mjumbe wa kikundi hicho alisema kuwa japo kuwa yeye ni mjane anayelea familia anauwezo wa kuwapeleka watoto wake shule na kujenga nyumba nzuri ya familia kutokana na viazi lishe anavyolima.
Wakieleza kwa upande wa changamoto wakulima hao walisema kuwa pamoja na mafanikio hayo pia wakulima wa zao hilo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na ukosefu wa soko la uhakika na  ukosefu wa usafiri kutoka shambani kwenda sokoni.

Wameiomba serikali kushirikiana mashirika na kampuni binafsi kuwahamasisha wakulima  kuongeza jitihada katika kilimo hicho na kuongeza idadi ya maofisa ugani ili wawaongezee uwezo wa kuzalisha na kutafuta masoko zaidi. Na ikiwezekana serikali iwasaidie wakulima hawa kuwatangazia kazi zao katika soko la nje ili kuwaendeleza wakulima.

kwa mantiki hiyo basi Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA),  pia wanapaswa kuwafikia wakulima ili waweze kukagua kazi za wakulima, kuwaelimishe kwa lengo la kuwawezesha kuzalisha kwa ubora zaidi ili kuwapa uelewa wakulima ni jinsi gani wanaweza kuandaa bidhaa zao ili waweze kufika mbali zaidi na kujikwamua kutoka katika wimbi la kilimo duni na kufika mbali zaidi kama ilivyo katika kilimo cha mazao mengine kama vile kahawa, korosho na mazao mengine ambayo yapo kwenye ramani ya kuipatia pesa za kigeni nchi yetu.

Nae Robert Kileo afisa habari wa Ukiriguru amesema kuwa Kutokana na umuhimu wa viazi lishe Kituo cha utafiti wa Kilimo Ukiriguru  kikishirikiana na TAHEA kwa pamoja wamebuni mpango wa  kuhamasisha wakulima na wananchi kwa ujumla ili wafahamu umuhimu wa zao hilo.



Kileo alisema kwakuwa Tanzania ipo katika kufanya mapindizi ya kijani na kilimo kwanza inatakiwa kila sekta katika serikali kuunga mkono jitihada za wakulima ili kufanya kazi yakilimo iwe ajira kwa watanzania wengi ambao kilio chao kikubwa sasa ni ukosefu wa ajira nchini. 

Wataalam kutoka katika vituo hivyo wanasema kuwa, mbali na kuwaelimisha kuhusu faida zake pia wakulima wanaelimishwa umuhimu wa usindikaji wa viazi lishe na uendelezaji wa masoko katika mikoa ya kanda ya ziwa

Hivyo  serikali inapaswa kuingilia kati katika kuhamasisha wananchi kulima zao hilo, kutafuta masoko kwa ajili ya wakulima ambao wamekwishaanzisha kilimo hicho na kuwataka wananchi ambao bado hawajajiunga wafanye hivyo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Ushauri mwingine kwa serikali ni kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kukibadilisha kilimo cha viazi lishe ili kiwe cha kisasa na cha tija pamoja na kumwezesha mkulima mdogo kumiliki ardhi  na kuanzisha vituo vya kumsaidia.

Baadhi ya bidhaa zitokanazo na vizi lishe 



4 comments:

  1. acheni kuedit kazi za watu ninyi

    ReplyDelete
  2. mimi nataka hizo mbegu nipo mlandizi pwani.je naweza kuzipataje.namba yangu 0688 220664

    ReplyDelete
  3. Kwa Arusha nitapata wapi mbegu?

    ReplyDelete
  4. Mimi nataka viazi lishe

    ReplyDelete