Tuesday, 3 December 2013
DK SLAA ASITISHA ZIARA YAKE KUTOKANA NA HALI YA USALAMA KUTOKUWA SHWARI
MWANGWI wa uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema wa kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto na wenzake, mbali na kutikisa katika kanda sita kati ya kanda nane muhimu za chama hicho nchini, sasa umeanza kukubalika na Sekretarieti ya chama hicho Taifa.
Jana Kurugenzi ya Habari ya Chadema, ilituma ratiba ya ziara za Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, mikoani iliyoonesha amekubali ushauri wa kusogeza mbele ziara ya kutembelea majimbo nane ya Kigoma.
Awali Dk Slaa alitarajiwa kuanza ziara ya kuimarisha chama mkoani Kigoma kuanzia kesho lakini juzi Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Jafari Kasisiko, alisema baada ya kutafakari kwa kina na kwa kutumia hekima na busara, walipendekeza ziara hiyo isogezwe mbele.
Sababu za mapendekezo hayo kwa mujibu wa Kasisiko, ni kutoa nafasi kwa uongozi wa Mkoa, kwenda kuwaelimisha wanachama kutii uamuzi wa Kamati Kuu wa kumvua madaraka Zitto na wenzake, hata kama uamuzi huo umewaudhi, lakini lengo ni kudhibiti vitisho vya kuvuruga amani katika ziara hiyo vilivyokuwa vimetolewa.
“Mkoa uliomba Taifa liahirishe na kusogeza mbele tarehe ya ziara hiyo muhimu kwa mkoa wetu, ili Mkoa kama ngazi ya chini ya Kanda na Taifa, uende katika majimbo hayo na kuwaelimisha wanachama na wapenzi wetu, kuhusu kuheshimu na kuwa na nidhamu na uamuzi utolewao na ngazi ya juu yetu, hata kama una maumivu.
“Maoni ya wengi mkoani na kwa viongozi wa Chama ni kuudhiwa na uamuzi wa Kamati Kuu ambao ni dhahiri ulilenga kummaliza Zitto kisiasa.
Mkoa ulitishika na vitisho baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa majimbo ya Mkoa, kuwa hali ya usalama si nzuri kwa ujio wa kiongozi wetu Dk Slaa… endapo hali haitokuwa salama Mungu aepushie mbali,” alisema Kasisiko katika taarifa yake.
Dk Slaa ashaurika Pamoja na Chadema kusisitiza kuwa ziara hiyo itakuwepo, lakini taarifa ya jana ya Kurugenzi ya Habari ya Chadema, ilieleza kuwa badala ya kuanza ziara mkoani Kigoma kama ilivyokuwa awali, sasa ataanza ziara ya siku 20 kuanzia leo lakini mkoani Shinyanga.
Bila kufafanua atakaa Shinyanga kwa siku ngapi, taarifa hiyo ilifafanua kwamba ziara hiyo itamfikisha Dk Slaa mpaka mkoani Kigoma, ingawa haikueleza lini atakwenda katika mkoa huo anakotoka Zitto na atakaa kwa siku ngapi.
“Siku ya Jumatano Desemba 4 mwaka huu (leo), Katibu Mkuu Dk Slaa atakuwa Wilaya ya Kahama, siku inayofuata Desemba 5, atakuwa Wilaya ya Kakonko, Jimbo la Buyungu na Desemba 6, atakuwa Jimbo la Muhambwe. Ratiba ya siku zinazofuata itaendelea kutolewa kwa vyombo vya habari,” ilieleza taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Habari ya Chadema.
Mwenyekiti Singida
Wakati Dk Slaa akianza ziara za kuimarisha chama, vuguvugu la kupinga uamuzi wa kuvuliwa madaraka kwa Zitto, limeendelea kutikisa chama hicho katika kanda zake, ambapo jana katika Kanda ya Kati, Mwenyekiti wa Mkoa wa Singida, Wilfred Kitundu, alijiuzulu.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa tangu 1992, amechukua uamuzi huo kupinga Kamati Kuu kuwavua madaraka akina Zitto, hatua ambayo imeshachukuliwa katika kanda tano za chama hicho nchini.
“Nimeona ni vema sasa niuthibitishie umma wa Tanzania kuwa kwenye Chadema unaruhusiwa kugombea vyeo na nafasi zote isipokuwa Uenyekiti wa Taifa, ndio maana Zitto tuliyemuunga mkono, leo hii anashambuliwa kwa dhamira yake safi ya kidemokrasia.
“Tunampa onyo kali Katibu Mkuu Dk Slaa kuwa asithubutu kukanyaga Singida, ikiwa bado hajayafanyia kazi maelekezo yetu hapo juu. Kuzunguka kwake mikoani baada ya kumvua vyeo Zitto ni kwenda kuthibitisha kuwa amefanya makusudi mpango wake huo.
“Nimejiuzulu Uenyekiti wa Mkoa wa Singida kuanzia leo (jana) tarehe 3.11.2013 na kuahidi kuwa nitapambana mpaka mwisho wa tone la damu ya uhai wangu, kuhakikisha demokrasia ya ndani ya chama hiki inaheshimiwa na kwamba Watanzania hawadanganywi tena,” alisema Kitundu katika taarifa yake ndefu kwa umma.
Ofisi Arusha
Wakati katika Kanda ya Kati Kitundu akijiuzulu, ofisi za chama hicho za Wilaya ya Arusha, Mkoa na Kanda ya Kaskazini jana zilichomwa moto na watu wasiojulikana.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Levolosi, Ephata Nanyaro, alikiri kuchomwa kwa ofisi hizo zilizoko katika jengo moja eneo la Ngarenaro jijini hapa.
Nanyaro alisema ofisi hizo wana wasiwasi zilichomwa saa moja asubuhi kwa kuwa hali hiyo ilionekana saa mbili asubuhi baada ya ofisi hiyo kufunguliwa na kukuta moto ukiwaka katika baadhi ya maeneo.
“Ofisi imechomwa moto eneo la juu lakini huenda mchomaji alikuja na kutupia moto juu ya paa. Hata hivyo hawajafanikiwa malengo yao maana ni paa tuu na mbao zilizoshika moto,” alisema Nanyaro.
Alisema ana wasiwasi kuwa tukio hilo lilitekelezwa na watu aliowaita wahujumu wa chama chao, ambao ni wale waliofukuzwa hivi karibuni na chama hicho wakiwatumia watu aliowaita kuwa ni wafuasi wao bila kufafanua zaidi.
Hata hivyo, kiongozi aliyetimuliwa hivi karibuni, Ijumaa iliyopita ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Monduli, Mchungaji Amani Mollel, ambaye alidaiwa kukiuka kanuni za chama hicho baada ya kuitisha kikao cha kumtetea Zitto.
“Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha, napenda kuujulisha umma wote kwa ujumla kuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Monduli, Mchungaji Amani Silanga Mollel, amekoma/amesimamishwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Monduli kuanzia tarehe 29 Novemba 2013 kutokana na tuhuma nzito za uvunjifu wa kanuni za maadili ya chama,” alisema Katibu wa Chadema, Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alipokuwa akitangaza uamuzi huo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kanda zingine
Kanda zingine zilizokwisha kutoa kauli za kupinga Kamati Kuu ni pamoja na Kanda ya Mashariki Dar es Salaam na Pwani, kupitia kwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Temeke na mjumbe wa Baraza Kuu, Patrick Joseph, Kanda ya Kusini, Lindi ambako Mwenyekiti wa mkoa huo, Ally Chitanda, alijiuzulu wadhifa wake na kubakia na ujumbe Baraza Kuu Taifa.
Kanda ya Ziwa Magharibi, Mwanza kulitolewa tamko na waliojiita umoja wa matawi 189 ya Chadema Mwanza, yakiongozwa na mwanachama Robert Gwanchele. Kwa sasa Chadema inajiendesha kupitia kanda 10.
Kanda ya kwanza ni ya Mashariki Dar es Salaam, inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Kanda ya pili ni Kusini, kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, ikifuatiwa na Kaskazini yenye mikoa ya Tanga, Manyara ,Kilimanjaro na Arusha.
Pia ipo Kanda ya nne ya Kati inayojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida; Kanda ya tano ya Nyanda za Juu Kusini, iliko mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na Ruvuma.
Kanda ya sita ya Magharibi inajumuisha mikoa ya Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma; Kanda ya saba ya Ziwa Mashariki yenye mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara na Kanda ya nane ni Ziwa Magharibi, yenye mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.
Pia zipo Kanda ya tisa ya Pemba, yenye mikoa ya Pemba Kusini na Pemba Kaskazini na Kanda ya kumi ya Unguja. HABARILEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment