Pages

Translate

Tuesday, 5 November 2013

TUFAA LATOA AJIRA KWA VIJANA WA MJINI


              

Na Lydia Mapunda






“Asiyefanya kazi na asile” hii ni kauli ya Athumani Idd mfanya biashara wa matunda na mboga mboga Soweto jijini Mbeya. Alitoa kauli hiyo alipotembelewa na mwandishi dukani kwake jijini Mbeya.

 Athumani ni miongoni mwa wafanyabiashara wa maaatunda ya tufaa, embe, zabibu na machungwa na kwa upande wa mboga mboga huuza Uyoga, spinachi cornflower. Biashara hiyo aliibuni baada ya kutafuta ajira kwa mda mrefu bila mafanikio hivyo alianza kujihusisha na kilimo cha mboga mboga na kisha kuanza biashara hiyo aliyo nayo. Alisema “Vijana wengi wa mjini wamekuwa wakilalamikia ugumu wa maisha kutokana na ukosefu wa ajira ambapo imepelekea wengi wao kujihusisha katika vitendo vya uvunjifu wa sheria za nchi. Nimemaliza chuo cha UDSM (University of Dar es salaam) nimesomea mambo ya biashara, lakini sijabahatika kupata ajira hivyo nimeona nijiajiri mwenyewe kwenye kilimo cha mbogamboga na uuzaji wa matunda kitu ambacho sijutii kukifanya na Napata faida kubwa kuliko hata mshahara ambao ningelipwa. Na kati ya matunda yote niyauzayo tufaa linauzika sana kuliko mengine yote.

Mbali na Athumani Idd pia wapo vijana wengi sana ambao wamekuwa wakijishughulisha na biashara ya matunda hayo katika sehemu mbalimbali za nchi yetu haswa mijini. Hapo awali lilionekana ni tuda linaloliwa na watu wenye kipato kikubwa au watu wa mjini peke yao kitu ambaocho kimekuwa tofauti kwa sasa kutokana na uwingi wa matunda hayo na kuuzwa karibu kila mahalli hata barabarani kitu ambacho hapo awali haikuwa hivyo kwani hapo mwanzo tunda hili liliuzwa katika maduka makubwa pekee.

Mbali na biashara ya matunda ambayo imeenea sana sehemu za mijini, tufaa ni Tunda pekee ambalo limeonekana kutoa ajira kwa vijana wengi wanaojishughilisha na biashara hiyo. Na hiyo  ni kutokana na tunda lenyewe kupendwa na watu wengi pia upatikanaji wake hauna msimu maalum.
 
Kwa kuliongelea tunda hili ni tunda moja maarufu duniani ambalo hupendwa kuliwa na watu wote bila kujali lika la mtumiaji, hii inatokana na utamu, ulaini wake pamoja na faida za kiafya zinazopatikana kwa kula matufaa. Na wakati mwingine limekuwa likitumiwa na wapendanao ili kutoa ishara ya upendo baina yao

 Matunda haya hustawi zaidi kwenye nyanda za juu ambako joto sio kali, sehemu kama lushoto, mkoani Tanga, Arusha, miteremko ya Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Njombe, Songea na sehamu nyingine nyingi zenye hali ya hewa zinazofanana na hizo. Udongo unaofaa kwa kilimo cha tufaa ni wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji.

Unaweza kupanda kwa kutumia mbegu au kwa kununua miche bora kutoka kwenye taasisiza kilimo mfano Uyole Mbeya kwa wakulima wa nyanda za juu, Tengeru kwa wakazi wa Arusha na SUA kwa wale wa Morogoro nk. kama utatumia mbegu basi ni bora kununua mbegu bora au ukikosa mbegu basi jaribu kutumia zile utakazopata kutoka kwenye tunda lenyewe kwa kufuata kanuni bora za kilimo

Kutokana na hilo ipo haja ya serikali ya nchi yetu kuona kwamba hiyo ni fursa tosha kwa wakulima kupewa mafunzo na kuwawezesha ili kujizatiti katika kilimo cha matunda pendwa kama tufaa ili kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja kama si kwa taifa zima

Kwa sasa matufaa mengi yaonekanayo barabarani huletwa Tanzania yakitokea Afrika ya kusini ambako ndiko mafanikio makubwa yamepatikana kwa kilimo cha matunda barani Afrika. Na kilimo cha tufaa nchini humo limefanikiwa baada ya utafiti wa mbegu bora (hybrid) kufanyika na tufaa ni miongoni mwa tunda ambalo lilifanyiwa utafiti huo na ndipo mafanikio yalipopatikana.

Akiongea kuhusu kuruhusu kuingia kwa matunda hayo meneja wa TFDA mkoani Mbeya Bwana Rodney Alananga, amesema kuwa wao kama TFDA wamechunguza kwa umakini na wamehakikisha kuwa matunda haya yanayotoka Afrika ya kusini hayana madhara kama ambavyo watu wengine wamekuwa wakidhani na kuogopa kula matunda hayo kwa dhana ambayo wengi wao wamekuwa wakisema yanamdhara kwa afya ya binadamu. “sisi kama TFDA huwa tunaruhusu chakula kuingia nchini kama hakina madhara hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kufuata sheria za kibiashara mpakani kama vile kulipia ushuru  na vinginevyo watu wayatumie tuu kwani tunawahakikishia kuwa matufaa hayo hayana madhara ya aina yoyote” alisema meneja Rodney


Kwa upande wa wakulima wao wameiomba serikali kuchukua baadhi ya wakulima wanaotoka katika maeneo yanayolima matufaa na kuwapeleka Afika ya kusini ili kujifunza kwa vitendo jinsi ya ukulima bora wa matunda hayo ili wao pia waje kuwa mfano kwa wakulima wengine ili kuinua kilimo cha matunda hayo Tanzania. “sisi mpaka leo tunalima matufaa yaleyale ya zamani ambayo ukiyapeleka sokoni watu huyaita ya kienyeji  na wengi hawayapendi kwakuwa yana radha ya uchachu tofauti na yale ya kizungu” akimaanisha yale yatokayo Afrika kusini. alisema Yuda Nyamirandu mkulima wa njombe

“Mkulima hashawishiki mpaka ameona kwa macho ama sivyo utatumia nguvu kubwa sana kumshawishi mkulima kuwa mbegu Fulani inafaida na ndio maana wakulima wa mahindi wanawekewa shamba darasa ili waone na hii isiishie kwenye mahindi tuu” alisema Emmanuel Sanga

Akiongea kwa uchungu sana, Bwana Emmanuel alisema anasikitishwa sana na serikali ya Tanzania ambavyo haijaweka kipaumbele kujali kilimo kimatendo huku akitolea mfano jinsi wakulima ambavyo wanapata shida katika miundo mbinu, pamoja na teknolojia duni katika kilimo. “ Ndio maana vijana wanaona hakuna haja ya kujitesa kuingia katika sekta ya kilimo maana ni kazi ya mateso na ndio maana wanakimbilia mijini, lakini serikali ingejali sekta hii hakuna kijana ambaye angekwenda mjini wote tungebakia kwenye kilimo, lakini sasa matokeo yake hiyo kazi wanafanya wazee wasiokuwa na nguvu matokeo yake njaa inaikumba nchi”

Ikiwa kama kuna uwezekano wa vijana kupata elimu katika kilimo na kuwezeshwa kifedha ni hakika ya kwamba kilimo kwanza ikatimia kuliko kuiacha kauli hii ikaendelea kubebwa na wazee peke yao kama ilivyo sasa kwa vijana wengi kukimbilia mijini na kuwaacha wazee wakashughulika na kilimo. Na malengo haya yanaweza timia ikiwa kila mtanzania atasumama katika nafasi yake na kutimiza majukumu yake impasavyo.

Hata hivyo Tanzania bado hatujachelewa kwani taasisi za utafiti zipo na hivyo utafiti ukifanyika Tanzania yaweza kujikuta juu katika ramani ya wakulima bora duniani na kupata faida kubwa kama wazipatazo wenzetu. Kwani mbegu bora ni chanzo cha tija na mapato kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment