Pages

Translate

Monday 2 December 2013

RIPOTI YA CAG YAWATESA MAWAZIRI NA WABUNGE



Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick S.L. Utouh.
 

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaanza mkutano wake wa 14 mjini Dodoma leo, huku kukiwa na homa ya matokeo ya mjadala wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2011/12.
Taarifa hiyo inatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo sambamba na majibu ya awali ya Serikali kuhusu kasoro katika matumizi ya fedha za umma zilizobainishwa na CAG, huku Kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zikitarajiwa kutoa taarifa ambazo zitakuwa mwongozo wa mjadala bungeni.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema jana kuwa, kwa kawaida wabunge wanapaswa kujadili taarifa ya CAG kabla ya mkutano wa Bunge la Bajeti ambalo hufanyika Aprili, ili kuwawezesha kutoa maoni na maelekezo yanayopaswa kuzingatiwa katika mwaka wa fedha unaofuata. Kwa kuzingatia kalenda ya mikutano ya Bunge, mkutano wa 14 ulipaswa kufanyika Februari 2014, lakini kama Spika Anne Makinda alivyotangaza katika mkutano uliopita, unafanyika kuanzia leo ili kutoa fursa kwa Bunge Maalumu la Katiba ambalo litakaa kati ya Januari na Machi 2014.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema jana kuwa tayari Serikali ilishawasilisha majibu ya awali kuhusu hoja za ukaguzi na kwamba baada ya taarifa za LAAC na PAC kutakuwa na majibu ya nyongeza kwa hoja mpya zitakazoibuliwa na kamati hizo. “Serikali tayari ilishatoa majibu ya awali sasa kwa sababu Kamati za PAC na LAAC zilikuwa zikikutana na watendaji wakuu wa Serikali ambao taasisi au wizara zao zilionekana kuwa na kasoro kwenye hesabu, tutawasikia watasema nini na hapo ndipo Serikali itatoa tena ya nyongeza,” alisema Lukuvi.
Tangu Rais Jakaya Kikwete aliporidhia taarifa ya CAG kuwasilishwa bungeni kisha kujadiliwa na wabunge, baadhi ya vigogo wa Serikali wakiwamo mawaziri na watendaji wakuu ambao wizara na idara wanazoziongoza zilibainika kuhusika na upotevu mkubwa wa fedha za umma waling’olewa katika nafasi zao. Katika mjadala wa mwaka jana, mawaziri sita na naibu mawaziri wawili walitimuliwa kazi, yakiwa ni matokeo ya mjadala mkali bungeni wa ripoti ya CAG ya 2010/2011. Mbali na vigogo hao, pia fagio hilo liliwakumba wakurugenzi wakuu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na yule wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu zilizoisukuma Serikali kupeleka bungeni marekebisho katika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008, huku ikiongeza vifungu ambavyo vilitafsiriwa kuwa vinapunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya CAG. Kwa maana hiyo, Bunge linajadili kwa mara ya kwanza ripoti ya CAG tangu marekebisho ya sheria hiyo yanayozuia Bunge kujadili ripoti ya CAG kabla Serikali haijajibu hoja za ukaguzi, yapitishwe bungeni Februari mwaka huu.
Operesheni tokomeza
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inatarajiwa kuwasilisha taarifa kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanza Oktoba 4 mwaka huu ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kabla ya kusitishwa na Serikali Novemba Mosi. Uamuzi wa kusitishwa kwake ulitangazwa bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kutokana na wabunge wengi kuilalamikia kwamba iliambatana na uporaji, utesaji watuhumiwa na uchomaji nyumba za watu wasiokuwa na hatia. Jana, Dk Kashililah alisema kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli ilikuwa katika hatua za mwisho kukamilisha taarifa yake kama ilivyoagizwa na Spika Makinda na kwamba: “Huenda wakapewa nafasi ya kuwasilisha taarifa yao kutokana na umuhimu wake.”
Jana, Lembeli alikiri kamati yake kuanza kazi rasmi na kwamba tayari imewahoji watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama lakini akakataa kuwataja. “Ni kweli tulishaanza kazi na tulianzia Dar es Salaam na tumehoji watu mbalimbali na kesho (leo) tunaanza kwenda mikoani lakini naomba nisizungumze zaidi ya hapo… mambo mengine subirini taarifa bungeni,” alisema Lembeli. Kusitishwa kwa Operesheni Tokomeza Ujangili kulionekana kumgusa pia Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati akilihutubia Bunge Novemba 7, mwaka huu alisisitiza kuwa operesheni hiyo ilikuwa sahihi kwa masilahi ya nchi.
Shughuli nyingine
Dk Kashililah alisema Mkutano huo wa 14 wa Bunge utapokea na kujadili taarifa za kamati 15 za Bunge zikiwa na maazimio, mapendekezo au maelekezo kwa Serikali. Alitaja shughuli nyingine kuwa ni miswada miwili ya Serikali; wa Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013 na Sheria ya Takwimu na kusomwa kwa mara ya kwanza kwa Muswada Binafsi wa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) unaohusu kuundwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana nchini. Maazimio matatu ambayo yanahusu ushirikiano wa majeshi katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki, ushirikiano wa masuala ya fedha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Azimio la Mabadiliko ya Chuo cha Tengeru.

No comments:

Post a Comment