Manfree baada ya kunaswa na mke wa mtu.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lililoongeza faraja na furaha ya
shetani kule kuzimu, lilijiri juzikati huko Kimara Mwisho ndani ya
gesti moja (jina lipo kwenye droo zetu).
Akizungumza kwa uchungu mkubwa, mume wa mwanamke huyo ambaye hakupenda
jina lake liupambe ukurasa huu, alisema siku nyingi Manfree amekuwa
akimsumbua mke wake, hali iliyokuwa ikimpa wakati mgumu mwanamme huyo
mwenye mke.
“Jamaa amekuwa akimsumbua sana mke wangu, nilipokuja kuzipata taarifa
hizi nilishangaa sana lakini pia niliumia kama mwanamme,” alisema
mwenye mke huyo.
Mwenye mke (kushoto) akiongea na mke wa mtuhumiwa.
Kwa mujibu wa mume huyo, kufahamiana kwa Manfree na mkewe kulikolea
zaidi baada ya mwanamke huyo kuhitaji fremu kwa ajili ya biashara ya
duka ambapo kwa kutumia uenyeji wa jamaa huyo, alionesha kutaka
kumsaidia.
Mwanamme huyo aliendelea kusema kuwa sinema ya kunaswa kwa mwanamme
huyo ilianza siku moja baada ya yeye kwenda kwenye baa ya jamaa huyo
kuangalia mpira (hakuzitaja timu).
Alisema akiwa hapo baa, mara mke wake alitokea na kukaa kwenye kiti,
meza nyingine. Jamaa huyo naye akaenda kukaa na mke wa jamaa na kuanza
kuzungumza.
Nguo za Manfree zikiwa zimetundikwa chumbani.
“Mimi sikujua walichokuwa wakikizungumza na wala sikuwa na wasiwasi kwa
vile jamaa ananifahamu, anafahamu yule ni mke wangu na anawafahamu hadi
watoto wangu,” alisema mwanamme huyo.
Akaongeza: “Tulipofika nyumbani, mke wangu akasema amesikia mimi nina
wanawake wengi nje, nimewafungulia biashara na mambo mengine kibao.
“Nilimuuliza ameambiwa na nani, akawa anagomagoma kunijibu lakini
nilipombana sana mwisho akamtaja jamaa. Kumbe alipokaa naye pale baa
ndiyo alikuwa akimwambia uongo huo.
“Mke wangu akaongeza kusema kuwa jamaa huyo kwa muda mrefu amekuwa
akimtaka wakutane ‘praiveti’ lakini yeye amekuwa akimkatalia kwa sababu
analinda heshima ya ndoa yake.
“Mke wangu alinionesha meseji ambazo jamaa alikuwa akimtumia, niliumia
sana. Kwa kweli inauma sana jamani hasa kitendo hicho kufanywa na mtu
ambaye mnafahamiana!”
Kwa mujibu wa mwanamme huyo, hali hiyo iliendelea kuisumbua ndoa yake huku maneno ya Manfree yakizidi kumvuruga kichwani.
Mume huyo alizidi kueleza kuwa baada ya mkewe kukiri kwamba Manfree
amekuwa akimtaka wakutane chemba ndipo kwa pamoja walikubaliana kuandaa
fumanizi.
“Nilimwambia mke wangu lazima tutege fumanizi, lengo ni kumfanya jamaa
aachane na tabia hizi ambazo zinaweza kuharibu ndoa, watoto wakateseka
na mambo menginemengine. Nilimruhusu amkubalie kukutana gesti,” alisema
mume.
Mume anasema siku ya tukio, Manfree bila kujijua alimtumia meseji
mwanamke huyo, akamuomba wakutane ndani ya gesti moja iliyopo Kimara
Mwisho ambapo bila kupoteza muda mwanamke huyo alimtonya mumewe juu ya
meseji hiyo.
“Baada ya kunionesha meseji hiyo nilitafuta baadhi ya marafiki zangu ili twende pamoja kwenye eneo la tukio wakawe mashahidi.”
Baada ya mke kufika ndani ya gesti hiyo, mume anadai alimtaarifu jamaa
huyo ambaye alitokea na kumwambia mwanamke huyo kuwa amuongezee
shilingi elfu kumi kwani chumba ni elfu ishirini.
Kwa mujibu wa mume huyo, baada ya wawili hao kuingia chumbani humo,
jamaa huyo alivua nguo zote na kukimbilia bafuni. Nyuma, mwanamke huyo
aliutumia mwanya huo kumtaarifu mumewe ambaye naye aliwashika masikio
marafiki ili wakae mkao wa kumnasa jamaa huyo.
Muda mfupi baadaye, mume anasema Manfree alitoka bafuni na kufikia
kitandani puu! Hana hili wala lile, mwanamme huyo akiwa na ‘skwadi’
yake walizama ndani, wakagonga mlango, Manfree akakaribisha, alijua ni
mhudumu amemletea bia maana aliagiza.
Mume alizidi kusema kuwa jamaa alipigwa butwaa na kuonekana kuweweseka.
Yeye akamuuliza imekuaje yuko na mke wake chumbani? Jamaa akawa hana la
kujibu.
Katika maelezo yaliyomo kwenye video ya tukio zima Manfree anajieleza
akimuomba msamaha mume huyo pamoja na wote waliokuwa chumbani humo.
Mwanaume huyo anadai kuwa kwa hasira aliamua kumpigia simu mke wa
Manfree ili afike kwenye gesti hiyo kushuhudia mumewe alivyokutwa na
mke wa mtu gesti.
Anasema: “Mke alifika, akamkuta mumewe hajavaa nguo, aliumia sana lakini hakuwa na la kufanya.”
Baada ya ‘mhangaikaji’ wetu kuzipata data hizo, juzi asubuhi alimtafuta
Manfree kwa njia ya simu ya mkononi kupitia namba alizopewa na watu wa
karibu. Mwanzoni jamaa huyo alionekana kugoma lakini baada ya kubanwa
kwa vielelezo alikubali huku akisema japo alinaswa lakini pia jamaa hao
walitumia njia za kumteka.
“Aa..! Ni kweli nilikutwa na zahama hiyo lakini jamaa waliniteka bwana.
Hata hivyo, sitarudia tena kuwa na uhusiano na wake za watu na
tulishamalizana na mwenye mke kwa kumuomba msamaha,” alisema Manfree.
Katika hali ya kushangaza, baada ya mkewe kupigiwa simu na mwandishi na
kukiri kuwa ni kweli mumewe alinaswa chumba cha gesti akiwa na mke wa
mtu, alisema bado anampenda na kwamba ndoa yao bado iko imara kama
mizizi ya mti wa mbuyu!
“Ni kweli mume wangu alifumaniwa lakini bado nampenda sana na siwezi
kumwacha, nitamvumilia maana ni mume wangu,” alisema mke wa Manfree
aliyejitambulisha kwa jina moja la Sarah.