• Asema muswada uliopitishwa bungeni unalenga kuifuta tume yake
na Irene Mark
Tanzania Daima
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amesema Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 uliopitishwa na Bunge hivi karibuni unalenga kuifuta tume hiyo kabla ya kumaliza muda wake.
Muswada huo ambao ulipitishwa na wabunge wa CCM pamoja na Augustine Mrema wa TLP (Vunjo), ulisusiwa na wabunge wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kutokana na kuchakachuliwa baadhi ya vipengele huku Zanzibar ikiwa haijashirikishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema miongoni mwa vipengele vilivyofanyiwa marekebisho kwenye sheria hiyo ni kile kinachotaka tume yake ivunjwe baada ya kuanza kwa Bunge la Katiba.
Hoja za Warioba ndizo hizo zinazopigiwa kelele na vyama hivyo vitatu pamoja na makundi ya asasi za kiraia huku viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwabeza na kudai muswada huo ulipitia taratibu zote.
Alisema marekebisho hayo yanakwenda kinyume cha sheria mama iliyounda tume hiyo ambayo inaweka wazi kwamba majukumu ya tume yatafika ukomo baada ya kupigwa kura ya maoni.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, uamuzi wa wabunge hao utaleta mkanganyiko endapo watashindwa kuelewana kwenye baadhi ya vipengele, kwani hapatakuwa na mtu wa kuwafafanulia, kwa kuwa tayari tume itakuwa imevunjwa.
“Sheria iliyounda tume hii inasema wazi kwamba ukomo wa tume ni baada ya wajumbe wa tume hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu kura ya maoni na mchakato wa kupiga kura hiyo utakapokamilika.
“Wao hawaoni sababu ya sisi kuendelea kuwapo hapa, nawaomba watafakari kipengele hicho,” alisema Warioba aliyepata kuwa waziri mkuu wa Tanzania.
Kabla ya kuhitimishwa kwa mkutano wa 12 wa Bunge mjini Dodoma, wabunge wa upinzani walitoka nje wakisusia kupitishwa kwa mabadiliko ya sheria hiyo, wakidai kufutwa kwa baadhi ya vipengele vilivyobadilishwa dakika za mwisho bila kuwahusisha.
Kususa huko wakati kikao kinaendelea kuliambatana na vurugu baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kuwataka askari wa Bunge kumtoa nje Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, jambo lililowafanya wabunge wa vyama hivyo vitatu kutoka wote.
Pamoja na madai hayo, wabunge hao walilalamikia utendaji wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Katiba na Sheria chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana, kwa kubadili vipengele hivyo kabla ya kuupitisha bungeni.
Baada ya wabunge wa upinzani kususa, wabunge wachache wa CCM waliokuwapo ukumbini hapo na Mrema, walipitisha mabadiliko hayo na kuyapeleka kwa rais ili asaini na kuifanya kuwa sheria.
Nje ya Bunge
Moto uliowashwa nje ya Bunge na viongozi wa upinzani pamoja na makundi ya asasi za kiraia umebadili upepo kwani kelele za kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo zimezidi kuongezeka.
Ni katika hatua hiyo, mawaziri kadhaa, William Lukuvi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Stephen Wasira na Mathias Chikawe wa Katiba na Sheria, wamekuwa wakiendelea kuwabeza wapinzani.
Hivi karibuni Waziri Chikawe alifikia hatua ya kumtisha Rais Kikwete akisema kuwa endapo hatausaini muswada huo kuwa sheria atakuwa ametangaza mgogoro na Bunge.
Pia Wasira naye amenukuriwa akisema kuwa wanaopinga muswada huo usisainiwe lazima wampe rais sababu za kutofanya hivyo, kwa vile hana, na kwamba milango ya Ikulu kwa wapinzani hao kujadiliana na mkuu wa nchi imefungwa.
Matamshi hayo ndiyo yamewaleta pamoja viongozi wa vyama hivyo na makundi mengine wakizunguka kwa wananchi kuwaeleza karoso zilizomo kwenye muswada huo ambao CCM inataka kutumia turufu hiyo kuhodhi mchakato wa Katiba mpya.
Angalizo la Warioba
Mwenyekiti huyo aliwataka wanasiasa kuacha malumbano katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, huku akikanusha uvumi kwamba baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wametishia kujiuzulu.
Badala yake aliwataka waketi pamoja na kukubaliana kuhusu vipengele wanavyotofautiana kwenye rasimu hiyo, kisha kuwaeleza wananchi manufaa ya kuwa na Katiba ya wote.
“Huu si wakati wa Tanzania kutengana, wanasiasa wanapaswa kutumia fursa walizonazo kukaa pamoja na kushirikiana ili tupate Katiba bora, hatuwezi kupata Katiba kwa maandamano, mikutano na mivutano baina ya vyama vya siasa,” alisema.
Kwa mujibu wa jaji huyo, kilichopo kwenye rasimu hiyo ni maoni ya wananchi, hivyo hakuna haja ya kubadili, bali kuboresha ili kila Mtanzania anufaike na uwepo wa Katiba hiyo.
Alifafanua kuwa kuna baadhi ya wajumbe wa mabaraza walidiriki kuwakashifu wajumbe wa tume yake, hasa kutokana na wanasiasa kutoa matamshi ya kuwalenga wajumbe hao wa tume.
“Hilo limetusikitisha, matamshi hayo yalitolewa kwa lengo la kuwadhalilisha wajumbe wa tume na kuishushia thamani kazi kubwa wanayoifanya ndani ya tume,” alisema.
Jaji Warioba alisema pamoja na changamoto hizo, tume ilifanikiwa kukamilisha mchakato huo ambapo kwa kupitia mikutano 179 ambayo ilihudhuriwa na wajumbe 19,337 wa mabaraza ya Katiba walipata maoni.
Mbali na hatua hiyo, Jaji Warioba alisema tume imepokea maoni kutoka kwa makundi, asasi na taasisi mbalimbali 600 kuhusiana na rasimu ya Katiba mpya.
Alisema baada ya kukusanya maoni hayo, tume inatarajia kuanza mchakato wa kuchambua ili kuandaa ripoti itakayokuwa na maboresho na kuikabidhi kwa rais kwa ajili ya kuendelea kwa mchakato mwingine.
“Tumewahoji wawakilishi wa wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania Bara na Visiwani, zaidi ya vikundi 176 vyenye uwakilishi wa watu tofauti tulikusanya maoni yao.
“Naamini Watanzania wanataka Katiba inayoheshimu utu wa mtu, umoja na kuvumiliana,” alisisitiza Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment