Pages

Translate

Friday, 15 November 2013

MITIHANI KIDATO CHA NNE -2013 YAVUJISHWA



MTIHANI wa Taifa wa Kidato cha Nne, umeingia dosari baada ya walimu wawili akiwamo Mkuu wa Shule, kushikwa wakishiriki kutoa majibu kwa wanafunzi wao.
Tayari Polisi mkoani Singida, inashikilia walimu hao wa Sekondari ya Nkinto wilayani Mkalama kwa tuhuma ya kuvujisha mtihani huo unaoendelea kufanyika nchini kote hivi sasa.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Mkuu wa Shule, Monica Sebastian (30) na msimamizi wa mtihani huo, Agaloslo Otieno (32).
 
Alisema watuhumiwa hao walivujisha mtihani huo juzi kati ya saa 3 na 3:30 asubuhi katika shule hiyo iliyopo Kata ya Mwangeza Tarafa ya Kirumi.
 
Alidai kuwa Mwalimu Agaloslo aliyekuwa akisimamia mtihani katika shule nyingine ya Mwangeza, aliandika baadhi ya maswali ya Kiswahili na Uraia kwenye simu yake ya mkononi na kumtumia Mkuu wa Shule yake ya Nkinto, Monica aliyekuwa shuleni kwake.
 
Baada ya Monica kupata maswali hayo, inadaiwa alitafuta majibu akiwa chooni huku wanafunzi wakimfuata huko huko na kupewa majibu.
 
Kamanda Kamwela alisema lengo lao lilikuwa kusaidia wanafunzi, wafanye vizuri katika mtihani wao wa kidato cha nne mwaka huu. Alisema wanafunzi waliishaambiwa wadanganye wanakwenda chooni, ili wakapewe majibu na Mkuu wa Shule.
 
"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa uvujishaji huo ulifanyika kwa nyakati tofauti kati ya Monica na Mwalimu Agaloslo akiwa anasimamia mtihani huo katika shule tofauti.
 
“Baada ya Mkuu wa Shule kutumiwa maswali, alijificha chooni na watahiniwa kwa nyakati tofauti waliomba ruhusa kwa wasimamizi kwenda kujisaidia na hapo walimkuta Mkuu wa Shule na kuwapa maelekezo ya namna ya kujibu maswali hayo," alisema Kamanda Kamwela.
 
Alisema baada ya Polisi kupata taarifa ya siri kutoka kwa wasamaria, iliweka mtego katika Sekondari ya Nkinto na kumkamata Mwalimu Monica huku simu yake ikiwa na baadhi ya maswali ya mtihani.
-Habari Leo

No comments:

Post a Comment