SIMU moja baada ya Waziri wa Maliasili
na Utalii Balozi Khamisi Kagasheki, kutangaza kwamba Mamlaka ya Mapato
nchini (TRA) inahusika katika ujangili, Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison
Mwakyembe pia ameibuka leo na kutangaza kwamba TRA pamoja na Mamlaka ya
Bandari (TPA) kwa pamoja zinahusika katika biashara ya magendo nchini.
Balozi Kagasheki akiwa visiwani Zanzibar katika zoezi la kupakuwa shehena
kubwa ya pembe za Tembo ikiwa na vipande 1,021 na uzito wa kilo 2,915
ambayo haijawahi kukamatwa nchini, alisema kwamba TRA wanahusika katika
ujangili huo kwa sababu wao ndiyo wenye mamlaka ya kuhakikisha kwamba
mizigo yote haramu haipiti katika bandari hiyo.
"Katika hili siwezi kumumunya maneno,
lazima tu nisema ukweli hata kama wenzetu hawa watakasirika, lakini
ukweli ni kwamba hawana pa kukwepea kwani wanahusika kwa asilimia 100
katika ujangili huu, kwa sababu kama watu wasingekuwa na maslahi katika
hili kontena lisingekamatiwa hapa Zanzibar, hii ni ishara kwamba TRA
wanahusika na kusaidia kulipitisha hadi huku"alisema Balozi Kagasheki.
Balozi alisema kwamba, shehena
hiyo iliyokuwa tayari kusafirishwa kuelekea Philiphine ilikuwa katika
magunia 98 yaliyochanganywa na magunia mengine ambayo yalikuwa
yamefungwa pamoja na baadhi ya vitu vya baharini yalikuwa tayari
yameshawekwa ndani ya kontena la futi 40 tayari kwa kusafirishwa kwenda
Philiphne yakiwa katika hatua za mwisho za mamlaka husika za bandarini.
Katika hatua nyingine, Waziri wa
Uchukuzi Dk Mwakyembe akiwa jijini Tanga ametangaza vita rasmi na
wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa za magendo kupitia Bandari bubu
Mkoani Tanga huku akidai kwamba maofisa wa vyombo vya Serikali waliopo
kwenye mtandao huo watakiona cha moto. Dk Mwakyembe aliwataka watambue
kuwa, kiama chao kimefika kwa sababu tayari Serikali inayo majina ya
wafanyabiashara na baadhi ya maofisa wa Polisi, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA) wanaotumika kufanikisha
upitishaji magendo.
Dk Mwakyembe ambaye aliwasili Tanga juzi
na kufanya ziara ya ghafla kutembelea bandari bubu zilizoko mkoani
hapa, alitangaza vita hiyo alipozungumza na maofisa wa TRA, Polisi, TPA
na wafanyabiashara. Alisema baada ya Serikali kudhibiti Bandari ya Dar
es Salaam, wafanyabiashara magwiji wa upitishaji bidhaa za magendo
wamehamishia nguvu zao Tanga. “Natangaza rasmi vita dhidi ya walio
katika mtandao huo, watambue hatuwezi kuruhusu Bandari ya Tanga, bandari
bubu na mpaka wa Horohoro kuwa gulio la walanguzi, wapitishaji dawa za
kulavya na wahamiaji haramu,” alisema.
No comments:
Post a Comment