Dar
es Salaam. Marekani imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa
binadamu ya mwaka 2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa
wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
Tanzania
imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi 44 ambazo zinajaribu kupambana na
biashara hiyo, lakini hali inazidi kuwa mbaya zaidi
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya
nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy
in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha
wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za
mashambani na biashara ya ngono.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka
huu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka
bayana kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya
ndugu na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda
kuwasomesha au kuwatafutia ajira nzuri mijini.
“Unyonyaji
wa wasichana wadogo na utumikishaji majumbani ndilo tatizo
linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa kwa ajili ya biashara
ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya zinaongezeka. Pia, wasichana
wananyonywa kwenye maeneo ya utalii,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto
kutoka Burundi na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na
India wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na
majumbani nchini Tanzania.
“Baadhi
ya raia kutoka nchi jirani huingia Tanzania kwa hiari yao, lakini
hulazimishwa kufanya kazi majumbani kabla ya kupelekwa kutumikishwa
kwenye biashara ya ngono Afrika Kusini, Ulaya na Mashariki ya Kati,” inaeleza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Angela Kairuki alimtaka mwandishi kumtumia ripoti hiyo kwa njia ya
baruapepe ili aweze kuisoma na kuitolea maelezo.
Alipotafutwa siku ya pili, alisema kuwa
ameipokea na kuikabidhi ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) ili
ifanyiwe kazi na baadaye kutoa majibu.
“Ripoti niliipata nikaikabidhi ofisi ya
DPP kwa kuwa wao ndio wanaoweza kuitolea maelezo baada ya kuisoma.
Maoni yangu lazima yawe ya kitaalamu siwezi kusema bila kupata taarifa
kutoka kwao,” alisema.
Lawama kwa Serikali
Ripoti hiyo inaitupia lawama Tanzania
kwa kutokuwa na sheria thabiti za kupambana na biashara haramu ya
kusafirisha binadamu, huku ikitolea mfano namna ilivyoshindwa kuwasaidia
raia wake waliokuwa wakinyanyaswa nje ya nchi.
“Kamati ya Serikali ya kupambana na
usafirishaji binadamu, haijachukua hatua za kutosha katika kutekeleza
mpango mkakati wa kupambana na vitendo hivyo,” inaeleza na kuongeza:
“Serikali
imeshindwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa
usafirishaji wa binadamu kama ambavyo inaelekezwa kwenye sheria ya
kudhibiti biashara hiyo ya 2008.”
Taarifa hiyo inaitaka Tanzania kuongeza
nguvu katika kutekeleza sheria ya kudhibiti biashara ya kusafirisha
binadamu ya 2008 kwa kuwakamata na kuwashtaki wahusika wote, lakini
ikaikosoa kwa kusema inatoa adhabu ndogo kwa mtu anayebainika kufanya
makosa, ikiwa ni pamoja na kumhukumu kwenda jela miaka 10, kulipa faini
au vyote viwili kwa pamoja.
“Sheria hiyo haifanani na nyingine
kama za mtu anayepatikana na kosa la kubaka au kufanya kosa jingine la
jinai. Mamlaka imesema ina kesi nne inazozichunguza, saba zipo
mahakamani toka mwaka jana, zikiwepo mbili mpya,” inasema ripoti.
Pia, Serikali ya Tanzania imelaumiwa
kwa kushindwa kuripoti maendeleo ya uchunguzi wa maofisa wake
waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji binadamu.
LHRC na TGNP
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema tatizo la
usafirishaji wa binadamu pia linachangiwa na wasichana kuwa na tamaa ya
maisha mazuri, hivyo kukubali ahadi ambazo hupewa kwamba wanapelekwa
kusoma, wasifahamu wanarubuniwa.
“Wengi wanatamani kwenda ‘majuu’
wakidhani watapata elimu, lakini baadaye wanaingizwa kwenye vitendo
vinavyowafedhehesha na kuwafanya wakate tamaa kabisa,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema katika siku za karibuni
kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wasichana
waliochukuliwa vijijini kwenda mijini kufanya kazi.
Alisema pamoja na tatizo hilo
kuongezeka hapa nchini, hakuna tafiti za kutosha ambazo zimefanywa na
wadau mbalimbali kuonyesha madhara yaliyopatikana hadi sasa.
“Katika siku za usoni kumekuwa na
ongezeko kubwa la vitendo vya kunyimwa chakula, kupigwa na kufukuzwa
kazi huku wasichana wengine wakitumika kwenye biashara ya ngono,” alisema na kuongeza:
“Ripoti hii isiishie kwenye makabrasha bali ifanyiwe kazi ili jamii yote ijue kuwa hili ni tatizo.”
Ripoti hiyo inabainisha kuwa watu
47,000 pekee ndio walioweza kuokolewa mwaka jana kutoka kwenye mazingira
ya utumikishwaji kati ya milioni 27 waliopo katika hali hiyo duniani.
No comments:
Post a Comment