Imani za kimila wilayani Misungwi
mkoani Mwanza zinadaiwa kusababisha baadhi ya wajawazito kunyweshwa
maji machafu yakiwemo yaliyofuliwa shati la mume husika anayetuhumiwa
kufanya ngono wakati mke akiwa mjamzito, kwa kile kinachodaiwa ni
kuondoa mkosi ili mjamzito husika ajifungue salama.
Katika jamii ya wenyeji wilayani hapa,
ni kwamba mjamzito anaposhiriki katika tendo la ndoa na wanaume wengi,
hupata kifafa cha mimba siku ya kujifungua na dawa yake ni kunyweshwa
maji yaliyolowekwa mchanga kutoka eneo alilowahi kuzalia mbwa.
Hayo yalielezwa katika mafunzo ya afya
yanayoendelea wilayani hapa. Kuhusu kunyweshwa maji yaliyofulia shati,
Mhudumu wa Afya katika Kijiji cha Mwamanga, Manyanda Kanyumbo alisema
ikitokea mjamzito akachelewa kujifungua na ikagundulika mumewe alikuwa
na uhusiano na wake wengi, shati lake hufuliwa na kisha mjamzito huyo
hunyweshwa maji yaliyotumika.
“Watu wanaamini akishakunywa maji
machafu ya mumewe hujifungua haraka na salama na kikombe alichonywea
hufunikwa uvunguni mwa kitanda hadi atakapojifungua”, alisema.
Kwa upande wa mjamzito aliyetembea na
wanaume wengi, jamii inaamini kwamba ili aweze kujifungua salama,
lazima uchukuliwe mchanga sehemu ambayo mbwa amewahi kuzalia, ulowekwe
kwenye maji na kisha mjamzito husika anywe kuondoa mkosi kabla ya siku
ya Katika mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na hospitali ya Aga Khan kwa
kushirikiana na Chuo cha Maendeleo na Ushirika cha MS TCDC kilichoko
jijini Arusha, Kanyumbo alisema, “wanaamini kabisa mwanamke ambaye
amechangia wanaume wengi, siku ya kujifungua kuna uwezekano mkubwa wa
kupata kifafa cha mimba”.
Kanyumbo aliendelea kusema, “ili aweze
kujifungua salama, bibi hufuata mchanga wa sehemu aliyozalia mbwa na
kuuloweka kisha humnywesha, maana tunaamini mbwa hukutana na mbwa wengi
ili aweze kutunga mimba, wale mbwa wengi huwafananisha na wanaume
wengi.”
Jacqueline Martin muuguzi wa Mwanangwa,
alisema baadhi ya watu wanaamini mjamzito akivuka mto, mtoto wake
hazaliwi mapema na pia mwanamke huyo haruhusiwi kunywa maji akiwa
amesimama.
Wanadai akinywa maji akiwa amesimama siku ya kujifungua, mtoto hawezi kushuka haraka.
Vile vile wanaamini mjamzito akikaa kwenye jiwe au kinu, mtoto huchelewa kuzaliwa. --
No comments:
Post a Comment