KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida kaburi
ambalo alizikwa mtoto Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki
dunia miaka mitatu iliyopita na kuonekana akiwa hai hivi karibuni, jana
lilifukuliwa na viungo vya mwili wake kukutwa ndani.
Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi
mkali wa polisi pamoja na Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali
Mkoa wa Mwanza, Lucas Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu
waliokuwa eneo hilo, baada ya nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo,
Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati ufukuaji huo ukiendelea, huku
mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akianguka
na kuzirai.
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo
la tukio, Ndungulu alisema kuwa wameamua kufukua kaburi hilo ili kupata
sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya vipimo.
“Lengo la kufukua kaburi hili ni kutaka
tupate kiungo chochote cha mwili wa marehemu ili tufanye utafiti wa
kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu anayedaiwa kuwa ni mtoto wao
ndiye,” alisema.
Alisema kuwa ufukuaji huo umemalizika
na kwamba wamepata baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu na kuchukua
baadhi ya mifupa ya mapaja yote mawili ambayo itapelekwa katika
hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo
hivyo yatatolewa baada ya wiki mbili kama hakutakuwa na tatizo lolote
la kukatika kwa umeme.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali
ya Wilaya ya Geita, Adamu Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua
viungo hivyo, pia watachukua damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.
“Tumechukua pia damu ya mama na baba wa
Maulidi mwenyewe ili tukapime vinasaba (DNA) na kama alivyosema
mtafiti, majibu yatatoka baada ya wiki mbili,” alisema.
Akizungumza baada ya kazi ya ufukuaji
kumalizika, baba mzazi wa mtoto huyo, Maulidi Shabani, alisema kuwa
endapo majibu yatakuja tofauti au vile wanavyokusudia, wapo tayari
kuyapokea na kwamba ikigundulika huyo aliyeonekana ni Maulidi, pia
watampokea na kuendelea kumtunza.
“Lakini nina imani kuwa huyu aliyeonekana ni mwanangu Maulidi kabisa, kwa sababu anazo alama zote,” alisema mzazi huyo.
Mtoto Maulidi aliyefariki dunia miaka
mitatu iliyopita na kufanyiwa matanga, alionekana akiwa hai baada ya
kukutana na mama yake ana kwa ana mapema wiki hii asubuhi wakati
akienda kwenye shughuli zake za biashara.
Ilidaiwa na wazazi wake kuwa Maulidi
alitoweka ghafla na kushindwa kurudi nyumbani kwao Januari mosi 2011,
wakati alipokuwa amewapeleka mbuzi malishoni na mwili wake kuonekana
baada ya siku tatu akiwa amefia kwenye kisima cha maji.
Kwa mujibu wa baba yake, Maulidi
hakurudi nyumbani siku hiyo, ambapo waliendelea kumtafuta bila
mafanikio na ndipo baada ya siku tatu walimkuta akiwa amefia ndani ya
kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji cha Nyankumbu, Kitongoji cha
Mwembeni.
Tukio hili ni la tatu kutokea mkoani
hapa ambapo wilayani Kasamwa, mwanamke aliyefariki dunia miaka mitano
iliyopita alionekana hai na kutambuliwa na ndugu yake. Tukio la pili
lilitokea Wilaya ya Chato, wakati kijana aliyefariki dunia miaka miwili
iliyopita alionekana akiwa hai.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment