Jeneza lenye mwili wa mtoto mchanga limezua taharuki kwa wananchi na wakazi wa Mtaa wa Ihago, Kata ya 
Mahina, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza.
 Tukio hilo la  kushangaza na la aina 
yake, lilitokea Agosti 29, mwaka huu, majira ya saa 12:00 asubuhi baada 
ya kugunduliwa na mfanyabiashara Ester Musa (28) likiwa limetelekezwa 
kwenye mlango wa mgahawa wake.
Jeneza hilo linaaminika kufukuliwa na watu wasiofahamika kwenye moja ya makaburi eneo la Mahina jijini hapa.
Akizungumza  kuhusiana na tukio hilo, 
Ester anayemiliki na kuendesha mgahawa alisema, alifika katika eneo lake
 hilo la biashara, ghafla akapigwa na mshangao baada ya kuona jeneza 
likiwa mbele ya mlango wa mgahawa wake.
“Nashindwa kujua nini maana ya tukio 
hili sababu hivi karibuni nilikuta barua imebandikwa ukutani ikinitaka 
nihame kutoka eneo hili, vinginevyo nitaona nitakachofanyiwa. Leo 
nimekuta jeneza mlangoni,” alisema Ester na kuongeza;
“Tukio hili nalihusisha na imani za 
kishirikina lakini kubwa linachangiwa na wivu wa kibiashara.Tangu 
lizaliwe sijawahi kuona jambo kama hili. Hapa sijawahi kugombana na mtu 
yeyote nashangaa kufanyiwa kitendo cha namna hii katika eneo la biashara
 yangu.”
Mwenyekiti wa mtaa huo, Anthony Deus 
alisema kitendo cha kufukua mwili wa marehemu tena mtoto mchanga, si cha
 kibinadamu na ni tukio la kusikitisha katika jamii, hivyo 
watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza,
 ACP Christopher Fuime, alikiri kuwapo kwa  tukio hilo na kusema hakuna 
mtu aliyekamatwa akihusishwa nalo.
“Tunaendelea na uchunguzi lakini hadi 
sasa hakuna aliyekamatwa akihusishwa na tukio hili la kusikitisha… 
wananchi wameuzika upya mwili wa mtoto huyo,” alisema.
 
 
No comments:
Post a Comment