AINYOOSHEA KIDOLE SERIKALI YA CCM
 
   WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amevitaka vyombo vya dola na
 wafanyabiashara wakubwa nchini, kujenga mahusiano bora kati yao na 
wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) ili kuondoa tabaka la matajiri na
 masikini linaloweza kuathiri uchumi wa taifa. Lowassa
 aliyasema hayo jana wakati akizungumza na machinga wa eneo la Makoroboi
 jijini Mwanza, ambao pamoja na mambo mengine aliwachangia sh milioni 20
 kwa ajili ya kutunisha mfuko wao. Mwanasiasa
 huyo ambaye pia ni mbunge wa Monduli, aliinyoshea kidole Serikali ya 
chama chake cha Mapinduzi (CCM) na kuitaka ihakikishe inatekeleza kwa 
vitendo ilani yake inayosisitiza wananchi kuwezeshwa kiuchumi ili 
kuondoa matabaka.
 
      Huku akishangiliwa na wafanyabiashara hao, Lowassa ambaye 
aliongozana na baadhi ya makada wa CCM kutoka ndani na nje ya Mwanza, 
alisema kila mwananchi wa Tanzania lazima ale, ingawa kwa namna 
tofauti. Alisema kuwa ili amani iwepo nchini, lazima Jeshi la Polisi na wafanyabiashara wakubwa wawathamini wafanyabiashara wadogo. “Tunataka
 tuwasaidie hawa vijana wetu, maana ni nguzo kubwa sana katika maendeleo
 ya taifa. Ilani ya CCM inasema lazima watu wawezeshwe kiuchumi. “Kwa
 maana hiyo katika nchi yetu kila mtu lazima ale. Na kula kwenyewe 
tunatofautiana, huyu anakula mkate na huyu anakula hiki. Na ili amani 
iwepo lazima RPC au OCD na wafanyabiashara wawathamini machinga,” 
alisema Lowassa.
 
      Pia alitahadharisha kuwa endapo wafanyabiashara hao wadogo 
watadharauliwa katika nchi, lazima watakula sahani moja na matajiri. Alitumia pia fursa hiyo kukanusha tuhuma dhidi yake kwamba amejilimbikizia mali. “Wapo
 baadhi ya watu wanasema hela ninazotoa hizi ni zangu. Mimi sina fedha, 
ninazotoa ninapewa na marafiki zangu. Mimi si tajiri wa fedha, ila ni 
tajiri wa marafiki na ushawishi ninao,” alitamba. Katika
 hatua nyingine, Lowassa alikataa kuulizwa maswali na wamachinga hao 
akisema ameandaa kamati itakayoratibu harambee ya kuwachangia kwa lengo 
la kupata sh bilioni moja. “Kwa
 maandalizi ya harambee nitakayorudi tena kuifanya, na ili mjue kwamba 
nipo makini natoa hundi ya sh milioni 10 na milioni 10 nyingine nitaitoa
 leo hii,” alisema Lowassa ambaye baadaye aliondoka kwa kutembea kwa 
miguu hadi Mwanza Hotel.
 
 
No comments:
Post a Comment