CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewaonya makada
wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward
Lowassa, na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
kuwa wasipoteze muda kuusaka urais 2015 kwa njia ya harambee makanisani
na misikitini. Onyo
hilo limetolewa na wabunge wa CHADEMA Kanda ya Ziwa wakati wakihutubia
mkutano wa hadhara uliofanyika kituo cha mabasi Igoma jijini Mwanza,
wakisema kuwa pamoja na makada hao kutumia nyumba za ibada kujijenga
kisiasa wasipoteze muda wao kuwania nafasi hiyo kwani hawawezi kuipata.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, mbunge wa Nyamagana,
Ezekiel Wenje, alisema kuwa Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa uwaziri
mkuu mwaka 2008 kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond
kwa sasa anaonekana kuhaha kuchangisha fedha makanisani, misikitini na
Wamachinga akitaka aungwe mkono katika harakati zake za kisiasa. Wenje
aliwasihi wananchi kuchukuwa fedha zinazotolewa na Lowassa, lakini
akawataka wafanye uamuzi wa kuiangamiza CCM katika uchaguzi wa serikali
za mitaa mwaka 2014 uchaguzi mkuu wa 2015. “Lowassa
ambaye ni mbunge wa Mondoli na mjumbe wa NEC, amekuwa kinara wa
kuhudhuria harambee akilenga kujiimarisha kisiasa. Nasikia majuzi
alikuja hapa Mwanza kuchangisha fedha kwa Machinga. Na huyu Sitta eti na
yeye anausaka urais...jamani Tanzania imekuwa nchi ya kuchezewa hivi?”
“Sasa fedha wanazotoa zipokeeni lakini maamuzi yenu ya kuiondoa CCM
madarakani na kuipa madaraka hayo CHADEMA mwaka 2015 yapo pale pale,”
alisema Wenje kisha kushangiliwa na wananchi waliofurika mkutanoni
hapo. Aliongeza
kuwa ili kuthibitisha kwamba serikali haiwajali wananchi wake, imetoa
misamaha kwenye mafuta yanayotumika katika migodi ya madini nchini,
lakini wananchi walalahoi wanatozwa kodi ya sh 1,000 kwenye laini ya
simu, wanja na vipodozi vingine vya wanawake. Wenje
alisema kuwa suluhisho pekee la Watanzania kujinasua na janga la
umaskini ni kuiondoa madarakani serikali ya CCM pamoja na kuwa na Katiba
nzuri inayojali ustawi wao.
Alisema kuwa CHADEMA kimedhamiria kukusanya saini za Watanzania
milioni 10 kwa lengo la kutaka Katiba mpya iamuru Spika wa Bunge,
mawaziri wasitokane na wabunge ili kujenga uwajibikaji. Mambo
mengine muhimu ndani ya Katiba mpya yatakayowekewa saini na wananchi ni
pamoja na kuundiwa mabaraza ya Katiba ambayo yatawashirikisha, kuwepo
mawaziri saba katika baraza la mawaziri, dira ya maendeleo ya taifa,
haki za binadamu, Bunge kuwa na wabunge 75 na mihula mitatu ya ukomo wa
ubunge. Naye
mbunge wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi, aliwataka wananchi
kutambua jinsi serikali ya CCM ilivyoshindwa kuwapelekea maendeleo
kinyume cha Katiba ya nchi.
No comments:
Post a Comment