“Ninatoa dakika 10 kwa aliyeingia na mavazi
 ambayo hayatakiwi kanisani humu kutoka mara moja akavae vizuri, la 
sivyo ndoa yao haitafungwa,” alisema Padri Haule wa Kanisa hilo lililoko
 Oysterbay, Dar es Salaam.
Awali vurugu hizo zilizotokea Jumamosi iliyopita, zilianzia nje, wakati 
Katekista wa Parokia hiyo, Yohane Maboko, alipotangazia wanandoa na 
ndugu zao waliokuwa mabega wazi au kuvaa nguo fupi, kutafuta nguo za 
kujifunika au wasiingie kabisa kanisani.
Maharusi walikubali kutekeleza ombi hilo, wakavishwa vitambaa mabegani 
vya rangi tofauti na gauni jeupe la harusi, wakaruhusiwa kuingia 
kanisani, tayari kufunga pingu zao za maisha.
Hata hivyo, mmoja wa ndugu wa maharusi hao ambaye jina lake 
halikupatikana mara moja, alipotaka kulazimisha kuingia na kivazi chake 
cha mabega wazi, alizuiwa na Katekista Maboko. Katekista huyo alimfuata 
mwanamke huyo ili kumrudisha akavae vizuri, lakini aliibua zogo na 
kulazimisha kuingia na vazi hilo.
Zogo hilo lilipoendelea, wanandugu waliingilia kati, wakitetea vazi hilo
 ambapo mmoja wa wanandugu, alimvua miwani Katekista Maboko na kuipiga 
chini ikavunjika huku yeye na wenzake wakimtolea maneno makali ya 
kumtaka asimzuie ndugu yao kuingia kanisani. 
Wakati ndugu hao wakimdhibiti Katekista Maboko, mwanamke huyo alitumia 
mwanya huo na kupenya hadi ndani ya Kanisa, ambamo Padri Haule, alikuwa 
akijiandaa kuanza ibada.
Baada ya Padri Haule kupata taarifa, alitangaza kuwa ndoa ya maharusi wa msichana huyo, haitafungwa hadi awe ametoka. 
Licha ya Paroko kutangaza hivyo, bado ukaidi uliendelea jambo 
lililomfanya Katekista Maboko kumfuata tena dada huyo na kumwamuru atoke
 nje, ambapo aliendelea kupinga na baadaye akatekeleza amri hiyo ya 
Paroko.
 Baada ya hapo shughuli za kufungisha ndoa ziliendelea kwa amani na 
utulivu hadi mwisho maharusi wakatoka kwenda kuendelea na mambo mengine.
Akizungumza na mwandishi wetu, Katekista Maboko alisema waumini hao 
walikiuka maadili ambayo Kanisa lina wajibu wa kulinda na kuyasimamia 
ili waumini wake wayafuate. 
Alisema miwani yake iliyovunjwa ilikuwa na thamani ya Sh 90,000 na baada
 ya ibada hiyo, aliyetenda kosa hilo alimwendea na kumwomba radhi na 
kulipa Sh 50,000 na kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki wakati wowote.
Maboko alisema uvaaji wa mavazi yasiyotakiwa kanisani hapo, umekuwa 
ukipigiwa kelele mara kwa mara, na hata katika mafundisho ya ndoa 
huambiwa lakini ukaidi unaendelea. 
“Maharusi wakati wa mafundisho ya ndoa 
tunawaambia kuhusu mavazi yao na hata ya ndugu zao watakaowasindikiza 
kanisani, kuwa wavae kistaarabu lakini hawasikii,” alisema Katekista 
Maboko. 
Makanisa mengi siku hizi yamekuwa yakipiga marufuku uvaaji wa nguo fupi 
na zinazoacha mabega wazi kwa wasichana na wanawake, wakati wa ibada za 
kawaida na za ndoa.
Habarileo 
 

 
No comments:
Post a Comment