MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma imetupilia
mbali mashitaka yaliyokuwa yamefunguliwa na serikali dhidi ya Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) kwa madai ya kumtukana Waziri
Mkuu Mizengo Pinda. Akitoa
hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Eliezel Luvanda
alitupilia mbali mashitaka hayo kutokana na hati ya mashitaka dhidi ya
mbunge huyo kuwa na upungufu. Luvanda
alisema kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 132 (20) hati hiyo haikuwa
na maelezo ya kutosheleza kuonesha ni lugha gani iliyodaiwa kuwa ni ya
matusi aliyotumia mshitakiwa huyo dhidi ya Pinda.
Awali akisoma hati hiyo, Mwendesha Mashitaka, Hariet Lopa alidai
kuwa Juni 24 mwaka huu akiwa katika Manispaa ya Dodoma, Mbilinyi aliweka
ujumbe wenye lugha ya matusi dhidi ya Waziri Mkuu Pinda kinyume cha
sheria. Kabla
ya hakimu kutoa hukumu hiyo, wakili na mwanasheria wa CHADEMA, Tundu
Lisu, aliwasilisha utetezi wake mbele ya mahakama hiyo akiitaka
kuitupilia mbali kesi hiyo kwa vile hakuna matusi yanayotajwa yakidaiwa
kutolewa na mbunge huyo dhidi ya Pinda. Lissu
alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 132 (20), hati hiyo
haikuwa na maelezo ya kutosheleza kuonesha ni lugha gani iliyotumika na
ni matusi gani, hivyo haiwezi kuwa kesi ambayo inaweza kuendelea
kusikilizwa.
Lissu alidai kuwa maneno yanayodaiwa yangesababisha uvunjifu wa amani
hayakutajwa katika hati hiyo huku akihoji upande wa mashitaka unataka
Sugu ajitetee kwa shitaka lipi. Aliendelea
kuieleza mahakama hiyo kuwa kama hati hiyo ya mashitaka iliyopelekwa
mahakamani hapo itaendelea kutumika, itakuwa imekiuka sheria, hivyo
akaitaka mahakama hiyo kuifuta kesi hiyo. Hakimu
Luvanda alipomtaka mwendesha mashitaka wa serikali kujibu hoja ya
Lissu, alishikilia msimamo wake na kuiomba mahakama kuendelea
kuisikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa ni mpya, hivyo makosa ambayo yapo
yatafanyiwa marekebisho wakati shauri likiendelea. Hata
hivyo Lissu alipinga kauli ya mwanasheria wa serikali kwa madai kuwa
hati ya mashitaka ni chafu na imeandaliwa ovyo, hivyo mahakama kukubali
kuendelea kusikiliza kesi hiyo ni kosa na hivyo ni vyema ikatupiliwa
mbali.
“Mheshimiwa hakimu naomba kesi hii itupiliwe mbali kwa kuwa hati ya
mashitaka ni chafu na ni ya ovyo. Naomba itupiliwe mbali na mtuhumiwa
aachiwe huru,” alisema Lissu na kuongeza kuwa wapo tayari hata kesho
kuendelea na kesi hiyo ikiwa serikali itaandaa hati sahihi. Hata
hivyo, baada ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka
alidai wataendelea na upelelezi na ukikamilika wataandaa hati mpya. Akizungumza
mara baada ya hukumu hiyo, Lissu alisema mahakama hiyo imetenda haki na
kama upande wa mashitaka haukuwa umeridhika na hukumu hiyo, ujipange
upya na kupeleka hati ya mashitaka.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) alisema hata
hivyo kufutwa kwa kesi hiyo hakumaanishi mteja wake hawezi kushitakiwa
tena, kwani bado Waziri Mkuu Pinda anaweza kwenda polisi kutoa maelezo
kama anaona kweli ametendewa kosa hilo. Kwa
upande wake, Sugu baada ya kuachiwa huru alisema kuwa anachoshauri ni
Pinda kujitafakari upya juu ya kauli zake anazozitoa hasa kuhamasisha
watu kupigwa. Awali,
Sugu alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma kuwa aliweka
ujumbe mfupi katika mtandao wa kijamii ambao ulikuwa unamtusi Waziri
Mkuu Pinda.
Hata
hivyo, alikuwa akipelekwa katika kituo cha polisi cha kati kwa
mahojiano na jana ilikuwa ni mara ya kwanza kufikishwa mahakamani.
Source: Kaijage D . ( June 2013). Sugu ambwaga Pinda. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment