Serikali imesisitiza kuwa haitavumilia kuona baadhi ya watu wanaendelea kupanda mbegu za chuki za kidini na kisiasa miongoni mwa Watanzania na imesisitiza kuchukua hatua bila huruma kuzimaliza njama hizo.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana, wakati akiahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge hadi Agosti 27, mwaka huu.
“Nataka niwahakikishie Watanzania kuwa serikali haitavumilia hata kidogo kuendelea kupandwa mbegu za chuki na za kidini na kisiasa miongoni mwa Watanzania.
“Serikali itachukua hatua kali bila huruma kuzima njama hizi mbaya dhidi ya taifa letu…vile vile, hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika bila kujali hadhi na nafasi yake katika jamii,” alisema.
Waziri Mkuu Pinda aliwasihi viongozi wa serikali, kisiasa, kidini na wananchi wote kwa ujumla, kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ili kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu.
Aliwataka Watanzania wote kushirikiana na vyombo vya dola katika kuwabaini wahalifu hao na kukataa vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchini.
“Kila mwenye taarifa za kuwezesha kukamatwa kwa watu wanaohatarisha amani ya nchi yetu atoe taarifa kwa Jeshi la Polisi na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na kwa maslahi ya taifa letu,” alisema.
Alisema ziko dalili ya kuwepo kwa vikundi vya watu wachache wasioitakia mema nchi ambavyo vinataka kupandikiza chuki za kisiasa na kidini miongoni mwa Watanzania na kuleta mapigano na mauaji miongoni mwao.
Alisema kwa mfano, hivi karibuni, katika kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita pamekuwepo na matukio ya vurugu, fujo na uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Singida na Iringa.
Alisema hofu ya migogoro ya kidini imetokea Zanzibar, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Geita.
Alisema baadhi ya matukio hayo yamesababisha vifo na majeruhi ikimwemo, kujeruhiwa askari na wananchi, uharibifu wa miundombinu, uharibifu wa mazingira na mali za serikali na watu binafsi.
Alisema matukio mfululizo ya fujo, vurugu pamoja na tukio la kulipua mabomu kanisani na hivi karibuni katika mkutano wa hadhara huko viwanja vya Soweto katika Kata ya Kaloleni mkoani Arusha na katika kampeni ya Chadema katika viwanja hivyo, yamesababisha hofu kubwa kwa wananchi na hisia ya uwepo wa tishio la kuendelea kwa vitendo vinavyoashiria ugaidi nchini.
Alisema matukio ya aina hii yakiachiwa yaendelee, uchumi wa nchi utadorora kutokana na ushiriki hafifu kwenye shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu inatanguliwa na nyingine aliyoitoa pia katika kikao cha bunge kilichomalizika ambapo alisema kwa wale wanaokadi amri halali ya Jeshi la Polisi wapigwe tu.
“Na mimi nasema wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi wapigwe tu, kwa sababu hakuna namna nyingine ya kupambana na wakaidi zaidi ya kuwapiga”.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini(CCM), Murtaza Mangungu aliyetaka kujua ni hatua gani zinazochukuliwa na serikali kufuatia matukio ya vurugu za mara kwa mara nchini.
No comments:
Post a Comment