Pages

Translate

Tuesday 25 March 2014

BILA BIOTEKNOLOJIA HAKUNA KILIMO KWANZA TANZANIA


Tanzania kama nchi nyingine haiwezi kukwepa maendeleo ya bioteknolojia kutokana na utandawazi na maendeleo ambayo yapo duniani kote, kwa kuwa bioteknolojia ya kisasa ni nyenzo muhimu katika kuboresha kilimo, uzalishaji viwandani, afya, hifadhi ya mazingira pia kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Akitoa ufaanuzi kwa waandishi wa habari  mkuu wa utafiti  COSTECH (Tanzania Commission for Science and Technology) Dr Nicholaus Nyange alisema bioteknolojia ni taaluma ya kutumia michakato ya kibaolojia katika  viumbe hai ili kupata mahitaji na huduma kwa maendeleo na maisha bora ya binadamu. Ambapo alisema kuwa ilianza kutumika tangu binadamu alipoanza kuchagua mimea, kutumia amira kutengeneza mikate, pombe na mvinyo, kutumia bacteria kutengeneza jibini na siagi ili kupata kitu kilicho bora.


Hata hivyo bioteknolojia imekuwa ikitumika viwandani, kwenye afya na hata katika sekta ya kilimo. Matumizi hayo yamekuwa yakikuwa na kubadirika kutokana na kukuwa kwa sayansi na teknolojia  duniani.

Kama ilivyo kawaida kila maendeleo yajapo huanza kutumika kufuatana na mahitaji ya mahali husika ikiwa ni pamoja na umuhimu wake. Akiongea kuhusu ukuaji wa biateknolojia Dr. Nyange alisema miaka 6,000 iliyopita matumizi ya micro-organisms ilianza kutumika, karne ya 19 uzalishaji wa miche kwa kutumia tishu ulianza kutumika na miaka ya 1970 biolojia ya molekuli na tekinolojia ya uhandisi jeni ilianza kutumika pia.

Kama ilivyo kauli mbiu ya Tanzania “kilimo kwanza” katika sekta ya kilimo nia ikiwa kukuza na kuendeleza sekta hii kwakuwa ndio uti wa mgongo wa nchi serikali imeweka mkazo katika kuendeleza elimu ya mapinduzi ya kijani kote nchini. Pamoja na juhudi hizo sayansi na teknolojia ni lazima itumike kutokana na mabadiriko mbalimbali yanayotokea ikiwa ni pamoja na bioteknolojia.

Hata hivyo zipo asasi na mashirika ambayo yamejitolea kuendeleza ukuaji wa sekta ya kilimo Tanzania kwa kuenenda na ukuaji wa sayansi na teknolojia. Nia ni kufanya kilimo kuwa na tija kwa mwananchi mmoja mmoja na nchi kwa ujumla wake

Kutokana na mabadiriko ya hali ya hewa na kuwepo magonjwa ya mimea, sekta hii imekuwa na changamoto nyingi zinazopelekea kudidimia kwa sekta hii kila uchwao.

Kwakuwa sekta hii si ya wakulima peke yao bali hutegemea wanasayansi pia, ambapo wao hufanya utafiti wa kugundua suruhisho ya changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kutumia bioteknolojia ili kupata ufumbuzi.


Akieleza jinsi bioteknolojia ilivyosaidia katika kilimo  Dr Nyange alisema kuwa ni pamoja na kudhibiti magonjwa, kuimarisha ubora wa mazao, kupata mbegu na mazao yanayohimili ukame na kukuza uzalishaji wa mazao.

Nae msimamizi wa maabala ya MARI (Mikocheni Agrcultural Research Institute)  Charles Kayuki amesema matumizi ya bioteknolojia yanaongeza tija kwa kuzalisha aina za mazao yenye kustahimili ukame na ukinzani dhidi yamagonjwa na wadudu ambapo alisema wamepata mafanikio makubwa katika mazao ya mgomba na mhogo, huku utafiti katika mazao mengine ukiendelea.


 Zaidi ya hayo, matumizi ya bioteknolojia yameonekani kuwa ni ukombozi wa kilimo nchini kutokana kuwepo kwa teknolojia ya uhandisi jeni ambayo huwezesha kuleta ufanisi mkubwa katika kilimo. Matumizi ya uhandisi jeni humfanya mkulima kupata mazao bora na mengi katika eneo dogo tofauti na ilivyo sasa ambapo ukulima hutumia nguvu nyingi mapato kidogo kitu ambacho kimewakatisha tama wakulima wengi na kuwafanya kuona kilimo hakina faida kwao na kubaki kuishangaa serikali ikisema ndio uti wa mhongo.


Hivyo Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zenye kutaka maendeleo, na kilimo ndio tegemeo kubwa la ajira kwa wananchi wake inapaswa kutumia kiufasaha biotaknolojia ili kukuza sekta hii. Na hayo yote yanawezekana ikiwa elimu zaidi itatolewa kwa wakulima ili kuondoa mawazo mgando na fikra potofu katika matumizi ya bioteknolojia. Serikali itambue yakuwa kilimo kwanza bila bioteknolojia ni sawa na kucheza ukwata bila kwenda mbele.

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment