WAUMINI wa Kanisa la Break Through
Assemblies lililoko eneo la Boko Magengeni nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam linadaiwa kuuza Sakramenti kwa Sh 100,000 kwa kila muumini.
Hatua hiyo inadaiwa
kuwanyima wasio na fedha chakula hicho cha Bwana hivyo kusababisha
malalamiko dhidi ya uongozi wa Kanisa hilo la Walokole.
Habari
za uhakika zilizolifikia gazeti hili, zilisema tukio hilo lililoshangaza
waumini lilitokea Januari 19. Kanisa hilo linaongozwa na Mchungaji
Godfrey Simtomvu.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati
tofauti, na kwa masharti ya kutotajwa majina, waumini walisema kitendo
hicho kiliwashangaza siku hiyo kanisani hapo walikokuwa wamekwenda kwa
ajili ya Ibada kama siku zingine.
Akisimulia, mmoja wao alisema
baada ya Mchungaji kuhubiri, vililetwa vikombe na mikate ambayo hutumiwa
kanisani kama ishara ya kushiriki pamoja Chakula cha Bwana. Makanisa
mengine hutambua ibada hiyo kama ya Sakramenti ya Chakula cha Bwana.
“Baada
ya vifaa hivyo kufika kanisani hapo vilionekana kuwa vichache tofauti
na waumini waliokuwa kanisani hapo…ndipo Mchungaji alipopaza sauti kuwa
mwenye Sh 100,000 na zaidi ndiye atakayeshiriki,” alisema na kuongeza
kuwa Januari 26, alishindwa kuabudu kutokana na kitendo hicho.
Alisema
baada ya kutamka hivyo, waumini wengi walinywea wakashindwa kusogea na
kupisha watu wapatao 10; lakini baada ya kuona idadi imekuwa ndogo zaidi
ikatangazwa kuwa hata wenye Sh 50,000 wanaweza kusogea mbele kushiriki.
Aliongeza kuwa wakati wote huo waumini walikuwa wakitazamana,
wakijiuliza juu ya utaratibu huo mpya, jambo ambalo ni kinyume na
ilivyokuwa awali kanisani.
Alisema Mchungaji baada ya kuona
idadi ya waumini inazidi kupungua, akawatangazia kuwa wasiokuwa na fedha
wajiandikishe kisha wapokee chakula hicho kisha na kesho yake wapeleke
kiwango hicho cha fedha. Muumini mwingine alisema jambo lililoshangaza
wengi ni utaratibu huo mpya ambao awali haukuwapo kwani walikuwa
wakitangaziwa wiki moja kabla na kutakiwa kujitayarisha kwa ajili ya
ibada hiyo ya Chakula cha Bwana.
“Awali Mchungaji alikuwa
akitupa taarifa wiki moja kabla, akiwataka waumini kujitayarisha na
kusafisha nyoyo zao kabla ya kushiriki kitendo hicho ambacho tuliamini
kuwa ni kitakatifu na chenye mafundisho makubwa kwa waumini,” alisema na
kuongeza kuwa hilo la kununua chakula lilizuka ghafla na hakujua hatma
yake.
Mwingine alisema mbali na kununua chakula hicho, pia jambo
lililozusha mshangao kwa waumini ni Mchungaji huyo kuleta watu kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuhubiri Neno la Mungu akidai
kuwa ni wahubiri ambao nao husisitiza neno la kutoa tu.
“Waumini tunaamini kuwa Bwana Yesu alitoa chakula hicho bure…iweje leo waumini wauziwe tena kwa kupangiwa kiwango?” Alihoji.
Akizungumzia
madai hayo, Mzee wa Kanisa hilo alisisitiza kuwa yeye si msemaji wa
Kanisa hilo na kusema madai hayo hayana ukweli na kwamba siku hiyo,
Mchungaji hakumaanisha kwamba utakuwa utaratibu, bali ilikuwa ni
kuhamasisha utoaji kwa muumini mwenye nacho. Alisema kufanya hivyo
halikuwa lengo la kutafuta fedha bali kupeleka Neno la Mungu mbele.
“Msemaji
wa Kanisa ni Mchungaji mwenyewe, ukiniuliza sana mimi utakuwa
unanionea, kama unamtafuta na ukamkosa atakuwa redioni katika kipindi,”
alisema mzee huyo.
Akizungumzia malalamiko hayo, Mchungaji
Simtomvu alisema kutokea kwa hali hiyo si imani ya Kanisa hilo bali
ilitokana na mhubiri kutoka Kongo ambaye alifunuliwa na Mungu na kutaka
waumini kuweka maagano yao na Mungu kwa mwaka huu.
Alisema hayo
yalikuwa mafunuo ya mtu na si imani na ni kitu ambacho hutokea mara moja
tu na kutolea mfano wa yai linapouzwa kwenye mnada kwa bei kubwa,
ingawa bei yake halisi inajulikana.
“Laiti ningemfahamu
aliyeleta taarifa hiyo ningemsaidia, kwani amekengeuka, mbona Mchungaji
TB Joshua wa Nigeria huuza maji katika vichupa vidogo kwa gharama kubwa
inayoweza kufikia Sh 75,000,” alisema Mchungaji Simtomvu.
Alisema
tukio hilo ilikuwa ni kwa muumini anayetaka kuweka agano na Mungu wake,
kwamba mwaka huu amtendee mambo gani na kuhoji kuwa zipo imani za ajabu
ajabu lakini haziripotiwi.HABARILEO
No comments:
Post a Comment