Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya.
DAR ES SALAAM
LICHA ya deni la taifa kuongezeka na
kufikia Sh27 trilioni mwaka jana, Serikali imesema bado ina sifa za
kuendelea kukopa kutokana na mapato ya ndani kuwa madogo.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya alisema jambo
linalozingatiwa na Serikali ni kuhakikisha fedha za mikopo zinatumika
kwa shughuli za kukuza uchumi.
“Deni la taifa linajumuisha
deni la Serikali kutoka vyanzo vyake vya mapato ya ndani na nje ya nchi
pamoja na deni la nje ambalo Serikali imelidhamini kwa sekta binafsi,”
alisema Mkuya.
Alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, deni
la taifa lilifikia Sh27 trilioni, kati ya kiwango hicho deni la nje ni
Sh20.2 trilioni na ndani ni Sh6.8 1 trilioni, huku deni la nje la sekta
binafsi likifika Sh3.5 trilioni.
“Tunaendelea kukopa na deni linaongezeka. Linaongezeka kwa mikopo inayochukuliwa na ile ambayo haijalipwa,” alisema.
Akitaja
sababu za kuongezeka kwa deni hilo alisema: “Linaongezeka kwakuwa nchi
bado inaendelea kukopa, kuendelea kuwepo kwa madeni ya nyuma kutokana na
muda wake wa kuyalipa kutofika, kuongezeka kwa watu na shughuli za
kiuchumi pamoja na kuwepo kwa madeni ambayo kwa mujibu wa mikataba
yanatakiwa kusamehewa.”
Alisema kutokana na kuwepo kwa
orodha ndefu ya nchi zinazokopa, hivi sasa Tanzania imejikita zaidi
katika kukopa mikopo yenye masharti ya kibiashara ambayo ni tofauti na
mikopo yenye masharti nafuu.
Hata hivyo, Mkuya alisema kila
mwaka Serikali inafanya tathmini kama inaweza kuhimili deni kutokana na
shughuli za kiuchumi ndani ya nchi. “Tathmini ya mwisho tumefanya
Septemba mwaka jana, haifanywi na Serikali pekee, inahusisha pia Shirika
la Kimataifa la Fedha (IMF) na Benki ya Dunia (WB),” alisema Mkuya.
Waziri
huyo alivitaja viashiria vinavyoonyesha kuwa nchi ina uwezo wa kuhimili
deni kuwa ni thamani ya deni la nje ikilinganishwa na uchumi wa nchi
(GDP),”
“Deni la nje sasa hivi ni asilimia 25 ambayo ni sawa
na asilimia 24.8 ya uchumi wa nchi. Lakini ukomo wa kukopa kwa kutumia
kiashiria hiki ni asilimia 50 ya deni, hivyo bado tuna vigezo vya kukopa
maana tupo katika asilimia 24.”
Alisema thamani ya leo la deni lote la taifa kwa uchumi wa nchi ni asilimia 40.5 na kwamba ukomo wake ni asilimia 74.
“Lakini hilo halitufanyi kukopa zaidi, ila kutokana na hali ya uchumi tutakopa katika vyanzo nafuu,” alinena.MWAANANCHI
No comments:
Post a Comment