MKAZI wa Bunju B, Grace Chapanga(34),
anashikiliwa na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa tuhuma za wizi
wa mtoto mchanga wa kike mwenye umri wa mwezi mmoja.
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa
Polisi Suleiman Kova alisema Chapanga alimuiba mtoto huyo, Veis Venus
Desemba 27 mwaka jana katika maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam.
Alisema
mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo baada ya kumhadaa mama wa mtoto
aitwae Salma Frank (29), mkazi wa Kawe Mji Mpya kwa kumuomba ambebee
huku wote wakiwa abiria wa daladala, wakitokea Hospitali ya
Mwananyamala.
Kova alisema walipofika kituo cha daladala Mwenge,
mtuhumiwa aliteremka upesi na kutoweka na mtoto, wakati mwenye mtoto
akikusanya vitu vingine alivyokuwa navyo.
“Chapanga alitenda
kosa hilo kwa kushirikiana na Halima Alabi (46), mkazi wa Boko Maliasili
ambaye naye alikamatwa Januari 4 mwaka huu,” alisema.
Alisema
watuhumiwa wote baada ya kutenda kosa hilo, waliondoka kwenda Sumbawanga
mkoani Rukwa, ambapo Chapanga alimdanganya mumewe kuwa yeye ni mjamzito
na angependa kwenda kujifungulia nyumbani kwao Sumbawanga.
“Upelelezi
wa tukio hilo ulifanikisha kumkamata mume wa Chapanga aitwaye Daniael
Mwaikambo (38), mkazi wa Bunju B, ambaye pia ni mfanyakazi wa Uhamiaji
Makao Makuu Dar es Salaam na kwenda naye Sumbawanga, ambapo walimkuta
mtuhumiwa na kumkamata” alisema.
Inasemekana kwamba tangu Chapanga na Mwaikambo wafunge ndoa mwaka 2010 hadi sasa, wanandoa hao hawajabahatika kupata mtoto.
Aidha,
Kova alisema mwaka 2012 Chapanga alifanyiwa upasuaji wa uvimbe tumboni
na daktari alimwambia hatoweza kushika mimba tena, jambo ambalo mwanamke
huyo hakumueleza ukweli mume wake wala ndugu yake yeyote hadi
alipopanga njama na hatimaye kufanikiwa kumuiba mtoto huyo.
Alisema
upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa kufuatilia uchunguzi wa
vinasaba (DNA) vya mama mzazi, mtuhumiwa na mtoto aliyeibwa. Pia alisema
mtoto huyo amekabidhiwa kwa mama yake mzazi. HABARILEO
No comments:
Post a Comment