Pages

Translate

Monday, 27 January 2014

MEYA WA KIGOMA AZALILISHWA NA MLINZI WA CHADEMA


WAKATI mvua ikisambaratisha mikutano ya Chadema mkoani hapa, tafrani imezuka jukwaani kwa mmoja wa walinzi wa viongozi walio kwenye msafara wa chama hicho kumkunja shati na kumtoa kwenye kiti cha viongozi wakuu, Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bakari Beji.


Tafrani hiyo ilizuka juzi jioni katika viwanja vya Mwanga Centre mjini hapa wakati Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na wa Ubungo, John Mnyika wakitoa hotuba.


Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa katika jukwaa la viongozi wakuu wa Chadema, wakati tafrani hiyo ikitokea, alishuhudia madiwani wa Kigoma Ujiji na viongozi wa chama hicho wilaya ya Kigoma Mjini, wakiwashambulia kwa maneno walinzi hao wa viongozi nakusema kitendo kilichofanyika kimemdhalilisha kiongozi huyo wa wananchi, tena nyumbani kwake.

Kabla ya tafrani hiyo, Lema alitaka kujua alipo Meya Beji na baada ya kuoneshwa akiwa nyuma ya viti vya viongozi wakuu alimfuata akasalimiana naye na kumtaka akae viti vya mbele walipokuwa wamekaa yeye na Mnyika.

Baada ya Lema kueleza hivyo aliendelea na taratibu zingine za mkutano ndipo Meya Beji akahamia viti vya mbele kabla mlinzi huyo, kumfuata na kumwambia hatakiwi kukaa hapo na aondoke mara moja.

Kutokana na kauli hiyo, baadhi ya waliokuwa karibu na Meya huyo walimfahamisha mlinzi huyo kwamba huyo ni Meya, lakini alishikilia msimamo wake na kumkwida shati ukosini akimsisitiza kwamba anapaswa kuondoka hapo.

Hali hiyo ilifanya madiwani na viongozi wa chama hicho wilaya ya Kigoma Mjini kupiga kelele kupinga kitendo cha mlinzi huyo, wakidai kimemdhalilisha Meya.

Baada ya kelele hizo, mlinzi aliondoka jukwaa kuu na kushuka chini, ambapo viongozi waliokuwa mahali hapo walitaka achukuliwe hatua za kinidhanmu kwa kitendo cha kumdhalilisha Meya.

Hata hivyo, kauli hiyo ya madiwani wakiongozwa na diwani wa Katubuka, Bilanyanye Bakayemba iliamsha zogo kubwa kutokana na baadhi ya watu kumtetea mlinzi huyo, kuwa inawezekana hakuwa anamjua Meya huyo ambaye pia ni wa Chadema.

Pamoja na utetezi huo, ilielezwa kwamba wakati akimtaka Meya kuondoka jukwaa kuu, mlinzi huyo alitambulishwa kuwa ni Meya lakini hakusikiliza na badala yake alifikia kumkwida shati, jambo ambalo baadhi ya watu walieleza kuwa alidhamiria kumdhalilisha.

Meya alionekana kushangazwa na kitendo hicho licha ya kusema, alijitambulisha kwa mlinzi huyo lakini alishangaa kukwidwa shati na kusukumwa ili atoke eneo hilo. Baadaye, Mnyika na Lema walimchukua Meya na kusimama naye jukwaani huku wakimwomba radhi kwa kitendo hicho wakieleza kuwa haikuwa mahali pake, kuanza kupigiana kelele wenyewe kwa wenyewe na kwamba litashughulikiwa kiutendaji.

Wakati tafrani hiyo ikiendelea, mvua kubwa ilikuwa ikinyesha ambayo hapo awali ilisababisha watu kukimbia na viongozi baada ya mashauriano mafupi walitangaza kuahirishwa mkutano huo juzi ili ufanyike jana.

Habari za ndani zilizopatikana kutoka kwa viongozi wa chama hicho na baadhi ya watu waliokuwa kwenye msafara huo wa viongozi, walisema licha ya kuvunjika kwa mkutano huo wa mjini hapa, mkutano mwingine uliokuwa ufanyike kijiji cha Mkongoro, Kigoma Kaskazini ambako Chadema imesimamisha mgombea katika uchaguzi mdogo wa udiwani, ulivunjika kutokana na mvua kubwa.

Baada ya kuvunjika mkutano wa juzi jioni Mjini Kigoma, viongozi wa Chadema walitafuta vibali ili uweze kufanyika jana saa nne asubuhi, hata hivyo haikuwezekana, kutokana na kukosa vibali na viongozi hao kulazimika kuendelea na ratiba yao wakienda Kasulu.HABARILEO

No comments:

Post a Comment