Pages

Translate

Sunday, 19 January 2014

GAZETI LA MWANANCHI LAOMBA RADHI KWA ANNA TIBAIJUKA

 
Katika toleo la Alhamisi Januari 9, 2014 gazeti hili lilichapisha habari kuhusu matokeo ya ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka katika Shamba la Mpunga la Kapunga, wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Baada ya uchunguzi wetu wa kina tumebaini kuwa habari hiyo ilipotosha ukweli na kutoa hisia potofu kwamba Waziri

Tibaijuka alibadili msimamo wake juu ya kuondoa eneo la hekta 1,870 kutoka kwa eneo la mwekezaji na kurekebisha hati, baada ya kuandamana na mwekezaji kwenye gari.

Tumejiridhisha pasipo shaka kuwa wananchi wa Kapunga walimsikiliza Waziri kwa makini, pamoja na kuwa kulikuwa na minong’ono ya hapa na pale katika baadhi ya wakati.

Kutokana na vyanzo mbalimbali, tumefahamishwa kwamba awali, katika kikao cha ndani na viongozi wa Kijiji, Waziri Tibaijuka aliwafafanulia msimamo wa Serikali wa kurejesha eneo lao lililomilikishwa kimakosa kwa Nafco mwaka 1995 kabla ya shamba hilo kuuzwa kwa mwekezaji mwaka 2006.

Waziri alisisitiza kwamba eneo litarejeshwa bila masharti, maana ni haki yao na pia ni suala la uhakika wa chakula kwao.

Waziri alikwenda Kapunga kukagua eneo hilo pamoja na kushughulikia kwa upana wake mgogoro uliokuwapo kati ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji na ziara yake ililenga kutoa maelekezo kwa wataalamu wa Wizara jinsi ambavyo ramani ya shamba hilo itarekebishwa kulingana na jiografia ya kijiji, shamba na matumizi yake.

Baadaye waziri alifuatana na viongozi wa wilaya, kijiji na waandishi wa habari kumtembelea mwekezaji na kufanya kikao cha wazi, ambako pia alimweleza mwekezaji kwamba eneo la hekta 1,870 litapunguzwa kutoka kwenye eneo la shamba na kurejeshwa kwa wananchi bila masharti yoyote.

Alimshauri mwekezaji kwa hiari yake arejeshe hati ili irekebishwe na wizara la sivyo atamwandikia Rais akipendekeza hati yote ifutwe na eneo kupimwa upya.

“Baada ya kauli hiyo, ndipo mwekezaji akasema, tena kwa utani, ngoja kwanza nikutembeze uone eneo halafu nitakujibu kwenye gari.” Kwa utani huo, watu waliangua kicheko, kwa hivyo inawezekana wengine walitafsiri kuwa kitendo cha waziri kupanda gari la mwekezaji pamoja na Mkuu wa Wilaya, Gulam Hussein Kifu, kungewafanya washawishiwe isivyo halali ili kubadili msimamo zaidi wa kupata picha halisi ya mgogoro kati ya mwekezaji kwa upande mmoja na wanakijiji kwa upande mwingine. Pamoja na hayo yote, Waziri aliendelea kushikilia msimamo wa kutatua mgogoro kwa manufaa ya pande zote mbili.

Tunakiri habari hiyo ilikuwa na upungufu na ilileta taswira na hisia potofu kwa wasomaji wetu. Tunamwomba radhi Waziri Tibaijuka na wananchi wa Kapunga kutokana na taarifa hizo.

No comments:

Post a Comment