MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA),
amesema asilimia 40 ya Baraza la Mawaziri limedumaa kwa sababu limeshindwa
kutekeleza majukumu yake. Msigwa pia alikilaumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa kimeshakuwa
chakavu kwa kushindwa kutoa matumaini kwa Watanzania. Alitoa kauli hiyo bungeni juzi wakati akichangia mjadala wa
taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Kamati ya Bunge ya
Bajeti na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali. Alisema kila mwaka wabunge wamekuwa wakizungumza mambo yale yale
na serikali imekuwa ikijibu vilevile wakati matatizo yale yale yameendelea
kuwepo.
“Bunge la mwaka juzi la Bajeti nilitoa takwimu za Wizara ya
Afya, kwamba asilimia 42 ya watoto wanaozaliwa Tanzania wamedumaa, mtu
anayedumaa hawezi kufikiri, hawezi kuhoji wala kudadisi, kwa kutumia takwimu
hizi hizi Baraza la Mawaziri ambao ni zaidi ya mawaziri 56, asilimia 40
wamedumaa na moja ya sababu ya kudumaa ni changamoto wanazozipata katika Bunge
hili. “Kila mwaka tunazungumza yale yale, tunapata majibu yale, watu
hawabadiliki maana yake kuna tatizo kwenye akili zao. “Matatizo ya wizi wa fedha lazima tuyapatie ufumbuzi,
haiwezekani kila siku tuseme yale yale, matatizo yapo pale pale,” alisema. Mchungaji Msigwa alisema lazima kuwepo kwa nidhamu ya
matumizi ya fedha za serikali na kuitaka serikali kuzikumbusha halmashauri
kwamba nchi inaongozwa kwa mfumo wa vyama vingi.
“Katika jimbo langu magari ya halmashaiuri yanatumika katika
shughuli za chama, mkurugenzi na meya wanalazimishwa na madiwani kwenda
uwanja wa ndege kumpokea Nape na Kinana, huu ni utovu wa nidhamu wa matumizi ya
fedha za umma na haukubaliki. “Ukiona mbunge rafiki wa mkurugenzi uje hapo kuna ‘deal’,
ukiona meya rafiki wa mkurugenzi hapo kuna kitu. Mkurugenzi na mbunge wakiwa
maaadui ujue mkurugenzi huyo anasimamia vizuri matumizi ya fedha,”
alisema. Msigwa alisema ni wakati muafaka wa Watanzania kuchagua chama
mbadala kuongoza nchi badala ya kuendelea kuichagua CCM. “Nashukuru sasa hadi Katibu Mkuu wenu wa chama kasema wazi
kwamba baadhi ya mawaziri ni mzigo, kazi yao ni kufunga tai na kutembea mjini
tu.
“Mbeya aliwaomba radhi Watanzania, sasa mnaanza kuongea lugha
yetu kwamba kuna mizigo, yaani hadi muambiane wenyewe ndo mnakubaliana… Hii Big
Result Now mmewakaririsha watu kama kasuku, mnahadaa Watanzania wakati watu ni
wale wale, wanafikiri vilevile, wanatenda vile vile eti Big Result Now. “Watanzania muda muafaka umefika, hiki chama chakavu kimechoka
ni vizuri tulete chama mbadala, mabadiliko yamefanywa sana hasa katika Baraza
la Mawaziri, lakini mambo bado yale yale,” alisema. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) alisema chanzo
kikubwa cha ubadhirifu wa fedha katika halmashauri ni wakurugenzi na wenyeviti
wa halmashauri au mameya huku akitoa mfano kwa Jiji la Mbeya. Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani (CCM) aliitaka serikali
kuchukua hatua za haraka kwa wale wote watakaobainika kuiba fedha za serikali. Dk. Kamani pia alimtetea Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwamba ni
kiongozi muadilifu, na kwamba anashangaa siasa za Tanzania kiongozi muadilifu
ndiye anayepigwa mawe.
No comments:
Post a Comment