Serikali imewasafisha aliyekuwa Katibu
Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo huku
ikimpandisha cheo aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali Deo Mtasiwa.
Nyoni alisimamishwa kazi pamoja na
aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa na wote kwa pamoja
walikuwa na tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao wakiwa watumishi wa
umma.
Jairo kwa upande wake alisimamishwa kazi
kutokana na kuchangisha fedha kinyume cha sheria kwa lengo la kusaidia
mchakato wa kupitisha bajeti ya wizara yake, katika mwaka wa fedha
2011/2012 na sasa ameondolewa kwenye utumishi wa umma, huku Bunge likiwa
bado halijapata taarifa ya utekelezaji wa maazimio yanayomuhusu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa
Nyoni kwa sasa amerejea kwa mwajiri wake wa awali, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), akishikilia nafasi ya mmoja wa wakuu wa idara, huku Dk
Mtasiwa akiwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, katika Ofisi ya Waziri
Mkuu, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katibu Mkuu Kiongozi
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amelithibitishia gazeti hili kuhusu watumishi hao na kwamba taratibu zimefuatwa.
“Mimi ninachojua ni kwamba Blandina
alikuwa mwajiriwa wa TRA na mkataba wake ulikuwa haujaisha… Siyo kwamba
alikuwa na mikataba miwili, kwenye utumishi wa umma huwa kuna utaratibu
wa kuazima watumishi wa umma.
Ndiyo maana unaweza kukuta mwanajeshi
anatolewa jeshini na kupelekwa uraiani au mtumishi kutoka idara moja
kwenda nyingine. Kwa upande wetu sisi tulishamwondoa kwenye ukatibu mkuu
na kule TRA hakuwa na tatizo,” alisema Balozi Sefue.
Kuhusu Dk Mtasiwa alisema: Uteuzi wa Dk
Mtasiwa ulikuwa wazi na hata alipoapishwa mambo yote yalitangazwa
hadharani.” Aliendelea kufafanua kuhusu Jairo akisema: “Jairo
alishaondolewa kwenye ukatibu mkuu, siyo mtumishi tena wa umma.” Naye
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo
alimtetea Nyoni akisema kuwa amerudi kwenye ajira yake ya awali.
“Siyo kwamba ameajiriwa TRA, amerudi tu
kwenye ajira yake ya zamani, alikuwa akifanya kazi hapa akaazimwa na
sasa amerudi,” alisema Kayombo na kuongeza: “Kwani amefanya kosa gani?
Kuna mashtaka yoyote aliyofanya unaweza kuyathibitisha?”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti
wa Bodi ya TRA, Bernard Mchomvu ambaye alisema Nyoni alishasafishwa na
Serikali ndiyo maana wamempokea. “Yule aliazimwa tu na Serikali…Sasa
kama Serikali imesham-clear sisi tutamkataaje?” alihoji na kuongeza:
“Kwa sababu sikumwomba huyo mtu,
nimeambiwa kwamba huyo yuko safi mimi nifanyeje? Unajua watu wanafurahia
wengine wakipata matatizo, hata kama mtu ameua, basi walete ushahidi.
Hata unaposema nchi imejaa rushwa, ulete ushahidi… kama Serikali
imeshamsafisha, ningemkataa ningekuwa mtu wa ajabu.”
No comments:
Post a Comment