KIGUGUMIZI cha serikali ya Rais Jakaya
Kikwete katika kuchukua uamuzi mgumu kwenye masuala mazito kimemwibua
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akisema nchi inakosa viongozi
jasiri wenye kusimamia utekelezaji wa mambo waliyoamua katika sekta
mbalimbali.
Alisema nchi ina tatizo kubwa la
uswahili mwingi wa kukaa kutekeleza kile kinachotakiwa kufanyika kiasi
cha kuwafanya kila mtu kuanza kulalamika.
“Hapa mnaamua bila kutekeleza, watu
hawana ujasiri wa kufanya maamuzi magumu, ni lazima awepo mtu mmoja wa
kuamua si wote kulalamika lalamika.
“Tukishakubaliana mambo ni lazima
yafanyike. Ni lazima tuondokane kuwa nchi ya kulalamika kuanzia
kiongozi wa juu mpaka mwananchi,” alisema.
Lowassa aliyasema hayo jana bungeni
wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Mipango ili kujadili Mpango wa
Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/16.
Lowasa ambaye ni mbunge wa Monduli
(CCM) alisema kuwa ni vema serikali ingekuwa na mipango michache yenye
kutekelezeka na tija kwa taifa.
Aliongeza kuwa kama angekuwa kiongozi
wa serikali angejikita kwenye vipaumbele vitatu ambavyo ni ajira, Reli
ya Kati na elimu kuliko kuwa na vipaumbele vingi visivyotekelezeka.
Alibainisha kuwa tatizo kubwa
linaloifanya serikali ishindwe kufanya vizuri kwenye maeneo mbalimbali
ni kujiwekea vipaumbele vingi huku rasilimali zake zikiwa chache na
wakati mwingine zile zinazopatikana hazitumiwi vizuri.
“Vipaumbele vingi mno utekelezaji wake
ni tatizo, tungechagua vichache, tukavisimamia na tuvitekeleze. Tukiwa
navyo vingi kwa wakati mmoja hatuwezi kuvitekeleza vyote, tuanze na
vichache tukivimaliza tunavifuata vingine.
Ajira
Alisema kama angekuwa kiongozi wa serikali angeanza na kipengele cha ajira ambacho kinakwenda sambamba na mipango.
“Huwezi kupanga bila kuzungumza habari
za ajira, tukiri kuna Watanzania wengi wamemaliza kidato nne, sita,
chuo kikuu, vyuo, darasa la saba walioko mitaani hawana ajira.
“Tusipowashughulikia, watakula sahani
moja na sisi, tusipoangalia yatatufika yale ya wenzetu ya Afrika
Kaskazini, si lazima yatufike lakini hawa wasio na ajira watakula
sahani moja na sisi,” alisema.
Lowassa aliongeza kuwa wanapaswa
kuangalia suala la ajira kwa umakini sana, kwamba inawezekana sana kila
mmoja akifanya wajibu wake.
Alibainisha kuwa nchi ya Hispania
ilikuwa na tatizo kubwa la ajira mara baada ya kutokea kwa mdororo wa
uchumi duniani lakini walikaa chini na kuamua kulitafutia ufumbuzi.
“Wale wenzetu waliamua kila mwekezaji
anayekwenda kwao sharti kubwa ni lazima atoe ajira kwa vijana, baada ya
miaka miwili walipiga hatua kubwa sana, lazima tuliangalie suala hilo
kwa umakini mkubwa sana,” alisema.
Lowassa aliwapongeza Mkuu wa Mkoa wa
Tabora, Fatuma Mwasa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu kwa
kuamua kuangalia suala la ajira kwa vijana.
Alisema viongozi hao wamethubutu kwa
kuwachukua vijana waliomaliza chuo kikuu na kuwapa matrekta na
kuwatafutia ardhi ya kilimo ambapo hivi sasa wanaendesha shughuli zao
vizuri.
Aliongeza kuwa Benki ya CRDB nayo imeanza kutoa mikopo kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu kwa kuchukua vyeti vyao kama dhamana.
“Wizara, watendaji na viongozi
mbalimbali kila mtu angetimiza wajibu wake katika hili jambo nina
hakika tatizo la ajira lingepungua kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Elimu
Alisema mjadala wa elimu usipuuzwe kwa kuwa lipo tatizo la msingi katika elimu ya Tanzania na hatua zinazochukuliwa hazitoshi.
Aliongeza kuwa alitegemea ripoti ya
tume iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza matatizo ya elimu hapa nchini
ingetolewa bungeni na ikajadiliwa ili wabunge wajue matatizo yaliyopo
na namna ya kuyatatua.
“Haitoshi kuchukua wanafunzi wengi
kumaliza chuo kikuu wakati akienda kwenye soko digrii anayoipata
haifai, hawezi kupata kazi kwa kuwa aina ya elimu aliyoipata
haimuwezeshi kuajiriwa.
“Wenzetu Ujerumani wanagawa digrii nusu
inatokana na ujuzi wa kitu fulani na nusu iliyobakia inatokana na elimu
aliyoipata hivyo kila kundi hapa lina uhakika wa ajira,” alisema.
Alisema kelele zinazopigwa na wananchi
juu ya matatizo ya elimu zinapaswa zisikilizwe na uitishwe mjadala wa
jambo hilo ili Tanzania isiachwe na jumuiya mbalimbali ikiwemo ile ya
Afrika Mashariki.
“Tukiacha mambo haya yaendelee kwenye elimu yetu tutakuwa wababaishaji na tutaachwa katika soko la ajira duniani,” alisema.
Reli ya Kati
Alisema kipaumbele chake kingine ni
kuboresha reli ya kati ambayo itachangia kupunguza uharibifu wa
barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa na serikali.
Lowassa alimpongeza Waziri wa Ujenzi,
Dk. John Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia ujenzi wa barabara
ambazo hivi sasa zimekuwa zikiharibika kwa kiwango kikubwa kutokana na
magari kupitisha mizigo mikubwa.
“Maroli yaliyopaswa kusafirishwa kwa
treni hivi sasa yanasafirishwa kwa magari, hapa ni lazima barabara
ziharibike, naomba muangalie kwa haraka sana Reli ya Kati,” alisema.
Lowassa pia alimpongeza Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harisson Mwakyembe, kwa jitihada za kutafuta ufumbuzi wa
foleni za jijini Dar es Salaam ambazo zinachangia kuzorotesha ukuaji wa
uchumi.
“Foleni Dar es Salaam it’s a nightmare
(jinamizi), muda tunaokaa katika foleni ukiujulimsha ni mrefu sana
serikali ni lazima mchukue hatua sasa, si suala la kusubiri,” alisema.
Afrika Mashariki
Lowassa aliitaka serikali kuacha
kugombana na marais wa Rwanda, Paul Kagame, Uhuru Kenyatta (Kenya),
Yoweri Museveni (Uganda) ambao wameamua kushirikiana na Sudan katika
masuala mbalimbali.
Asema Tanzania ijielekeze zaidi
kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo
ambako kuna manufaa makubwa zaidi.
Sumaye kufunguka
Wakati huo huo, Waziri Mkuu mstaafu wa
Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, ambaye ni mmoja wa watu wanaotajwa
kuutaka urais mwaka 2015, leo anakutana na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam kuanika kile kinachoelezwa kuwa ni mchezo mchafu
unaofanywa na mahasimu wake.
Hatua ya kada huyo wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), inafuatia tukio la hivi karibuni akidai kuhujumiwa
katika mwaliko aliopewa na vijana wa asasi isiyo ya kiserikali
inayojihusisha kuelimisha jamii kuhusu usalama na amani (Public
Terrorism Awareness Trust Fund and Human Welfare (PTA-HW).
Asasi hiyo iliandaa tamasha Jumapili
iliyopita jijini Dar es Salaam na kumwalika Sumaye kuwa mgeni rasmi
lakini katika mazingira ya kutatanisha saa chache kabla ya shughuli
hiyo iliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanza, aliarifiwa kuwa
imeahirishwa na kwamba atataarifiwa tarehe nyingine itakayopangwa.
Hata hivyo, katika hali isiyoelezeka
muda mfupi baadaye maandamano ya vijana hao yaliwasili katika viwanja
vya Mnazi Mmoja na kupokewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
kutoka Wilaya ya Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi.
Dalili za waziwazi za mgawanyiko
miongoni mwa waandaji zilijitokeza baada ya kuwasili kwa Karamagi
ambaye hakuwa ametarajiwa na waandaaji pamoja na washiriki wa tamasha
hilo.
Kwa muda mrefu sasa Sumaye amekuwa
akidai kuhujumiwa na wapinzani wake wanaomhofia katika mbio za urais
mwaka 2015 ambapo katika Uchaguzi Mkuu wa CCM mwaka jana alidai
kuchezewa rafu ya rushwa.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment