MAHAKAMA ya Rufani leo inatarajia kutoa
uamuzi wa ama kulikubali au kulikataa ombi la marejeo lililowasilishwa
na mwanamuziki wa dansi nchini, Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanae,
Papi Kocha ‘Mtoto wa Mfalme’, ambao waliomba mahakama hiyo ifanyie
marejeo hukumu ya kifungo cha maisha iliyoitoa Februari 2010, kwa kuwa
ina dosari za kisheria na kuwaachia huru.
Kwa mujibu wa hati ya wito wa mahakama
iliyotolewa kwa mawakili wa pande zote mbili, mahakama imemtaka Babu
Seya na mwanae pamoja na mawakili wa pande zote kufika leo mahakamani
ili wapokee uamuzi wa maombi hayo.
Oktoba 30 mwaka huu, jopo la majaji
watatu wakiongozwa na Jaji Nataria Kimaro, Salum Massati na Mbarouk
Mbarouk, walisikiliza ombi hilo lililowasilishwa mahakamani hapo na
wakili wa waomba rufani, Mabere Marando.
Wakili Marando alidai kwa mujibu wa
kanuni ya 66 ya Mahakama ya Rufaa ya mwaka 2009 inatoa mamlaka kwa
Mahakama ya Rufaa kufanya mapitio ya hukumu inazozitoa, hivyo wateja
wake wamewasilisha ombi hilo kwa sababu wanaamini mahakama ilikosea
kisheria katika hukumu yake Februari 2010.
“Waheshimiwa majaji, kwa sababu jopo
lenu katika hukumu yake lilikiri wazi wazi kuwa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu ilikosea kurekodi ushahidi wa watoto waliodai walitendewa
vibaya na waomba rufaa (Babu Seya na Papii) na sheria za nchi zinasema
endapo mahakama itabaini kuwa mahakama ya chini ilikiuka taratibu za
kurekodi ushahidi wa watoto wadogo, basi ushahidi ule wa watoto wadogo
uliotumika katika mahakama ya chini kuwatia hatiani washitakiwa unafutwa
na waomba rufaa au washitakiwa wanaachiwa.
“Nafahamu ni kazi ngumu kuwashawishi
nyie majaji kubadili uamuzi wenu mlioutoa katika hukumu ya Februari
2010, ambapo uliwatia hatiani wateja wangu, ila kwa utetezi huo wa
kisheria niliouainisha unaonyesha katika hukumu yenu mlikubaliana na
hoja yangu kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kurekodi ushahidi wa watoto
wadogo, naamini mtatumia busara zenu na kufuata sheria na leo naiomba
mahakama iwaachie huru wateja wangu,” alidai Marando.
Mawakili wa upande wa mjibu maombi
(DPP), Angaza Mwipopo, Jackson Mlati, Imaculata Banzi na Joseph Pande,
waliomba mahakama itupilie mbali ombi hilo, kwa kuwa sababu zote
alizozitoa alizieleza wakati wa usikilizwaji wa rufaa na ziliamuliwa
katika hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo Februari mwaka 2010.
Jackson alidai kama Marando anaona
hukumu ya mwaka 2010 ilikuwa na dosari, angeomba mahakama hiyo impangie
jopo la majaji watano wa kusikiliza ombi na si ombi lake kusikilizwa na
jopo la maji watatu wale wale waliotoa hukumu hiyo ambayo anadai ina
dosari.
No comments:
Post a Comment