MTOTO wa kaka wa Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, Willium Lukuvi, aitwaye Tomm
Malenga, ambaye ni katibu wake, amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili
wake baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuhusishwa na ujangili.
Habari zilizopatikana mjini hapa, juzi Jumapili, Oktoba 27, mwaka huu,
zinasema akiwa ofisini kwake siku hiyo, Tomm alifuatwa na maofisa wa
Wanyama Pori kwa kile kilichotajwa kuwa anahusika na ujangili.
“Walifika na kumkamata kisha wakaanza kumpiga, tena palepale ofisini
kwa Lukuvi. Amevunjika vidole vya mguu na mkono wake mmoja hauko sawa
baada ya kipigo hicho,” alisema mtoa habari wetu.
Tomm hakupatikana ili kuzungumzia sakata hilo lakini waziri Lukuvi
alifafanua baada ya kuzungumza na mwandishi wetu ambapo alisema
kilichofanyika anakijua na kwamba ni njama za wabaya wake.
“Sikiliza bwana, licha ya Tomm kuwa msaidizi wangu wa jimboni ni mtoto
wa marehemu kaka yangu. Wanasema eti ametajwa kwenye ujangili; sasa
kutajwa tu, unawezaje kwenda kumchukua mtu ofisini kwake, tena kwa
kumpiga? Huo siyo utawala wa kisheria,” alisema waziri Lukuvi.
Alisema, mtu aliyemtaja Tomm ni Gedi ambaye alikuwa wa kwanza kukamatwa
kwa ujangili na akasema amekuwa akishirikiana na mwanaye.
“Ukweli ni kwamba huyo Gedi ana usongo na mimi, kwani huwa ananipinga
tangu mwaka 1995. Aliwahi kugombea udiwani, tukagundua kuwa ni Msomali,
tukamfuta. Nadhani anatumia mwaya huo kunichafu mimi na familia yangu,”
alisema Lukuvi.
No comments:
Post a Comment