Kijana Said Hassan anadaiwa kumuua kikatili mtoto wa dada yake, Fatihia ‘Fety’ Said (2) na kuibua simanzi nzito.
Tukio hilo la kinyama lilitokea hivi karibuni maeneo ya Keko-Tolori jijini Dar ambapo ilidaiwa kuwa jamaa huyo ni teja.
Akizungumza kwa uchungu, mama wa Fatihia alisema kuwa siku ya tukio
(Jumatano iliyopita) aliamka asubuhi salama na mtoto wake ambapo
ilipofika muda wa saa 2:00 asubuhi alimpa mwanaye chai akawa anakunywa
huku anatembea, wakati huo yeye alikuwa akifanya kazi zake za usafi wa
ndani.
“Nilipomaliza usafi na kazi zangu nikaanza kumtafuta mtoto, sikumuona,
niliingiwa na hofu hivyo nikawa namsaka kila kona ya nyumba lakini
sikumuona.
“Nilikwenda nyumba ya jirani ambapo ndiko huwa anakwenda mara nyingi
kucheza lakini pia sikumkuta, baada ya kujiridhisha kuwa hayupo nilienda
kutoa matangazo msikitini kuwa mtoto amepotea,” alisema Mwamvita
Hassan, mama wa mtoto huyo.
Alisema kuwa baada ya jitihada zote hizo bila mwanaye kupatikana
aliondoka na wenzake na kwenda Mbagala, Dar akihisi labda kuna mtu
amemchukua mtoto wake kwani huko kuna nyumba yao nyingine lakini nako
hawakumkuta.
Kwa mujibu wa bibi wa mama Fatihia, walipomuuliza mtoto wa jirani
alisema kuwa amemsikia mtoto akilia chumbani kwa mjomba’ke Said waende
wakaangalie huenda alikuwa huko.
“Kweli tulivyoangalia tulimkuta mtoto amewekewa nguo chini ya kitanda,
juu yake kawekewa magodoro, tayari alishaaga dunia, hatukujua kama
alimnyonga au alimfanya nini kwani bado uchunguzi unafanyika kwa sababu
mtoto alikutwa na mapovu mdomoni,” alisema bibi huyo.
Mjomba wa mtuhumiwa, Shaban Juma alisema kuwa mtuhumiwa hakuwa na akili
nzuri kwani mara nyingi amekuwa akimpeleka Hospitali ya Wilaya ya
Temeke, Dar na akawa anapewa dawa ingawa yeye hakutambua ni dawa gani.
Mjomba huyo alipoulizwa kama mtuhumiwa alikuwa akitumia madawa ya
kulevya, alikubali na kusema kuwa kuna mtu alimthibitishia kuwa amekuwa
akimuona ‘akijidunga’.
Habari za uchunguzi zilibainisha kuwa mtuhumiwa huyo amewahi kufanya
matukio mbalimbali kama kujaribu kuchoma nyumba yao, kukojolea maji ya
kunywa na kutishia kufanya kitu cha ajabu ambacho watu hawatakisahahu.
Baba wa mtoto aliyejitambulisha kwa jina moja la Said alisema kuwa
alisikitishwa na tukio lililompata mtoto wake lakini huyo shemeji yake
alikuwa akimtishia kila siku.
“Nimeumia sana lakini naacha sheria ichukue mkondo wake kwa sababu ameshakamatwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment