KESI ya kikatiba iliyofunguliwa dhidi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda
kutokana na kauli yake ya kuruhusu wanaokaidi maagizo ya Dola wapigwe,
inatajwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Kesi
hiyo ilifunguliwa Agosti Mosi mwaka huu na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), dhidi ya Waziri Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), wakipinga kauli hiyo iliyotolewa bungeni. Itasikilizwa
na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, likiongozwa na Jaji Kiongozi
Fakhi Jundu wengine ni Jaji Augustine Mwarija na Dk Fauz Twaib. Inadaiwa
Mei 20 mwaka huu, Pinda akiwa bungeni katika nafasi yake ya Waziri
Mkuu, kinyume na Katiba ya Nchi alitoa kauli ya kuruhusu askari wa Jeshi
la Polisi kuwapiga raia ambao hawatatii amri yao kunapokuwa na vurugu.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi,
wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu kwa
sababu hakuna namna nyingine, eeh maana tumechoka sasa,” sehemu ya hati
ya mashitaka iliyonukuu kauli ya Waziri Pinda. Katika
hati hiyo inadaiwa kwa mujibu wa utekelezaji wa Sheria za Jinai, kauli
inayotolewa na kiongozi wa nafasi ya Waziri Mkuu, inaonekana kama amri
inayopaswa kutekelezwa na vyombo vya Dola kama Polisi, hivyo
itachukuliwa kama amri halali na kusababisha waendelee kuwatesa na
kuwapiga wananchi wasio na hatia. Aidha
inadaiwa Pinda alivunja ibara ya 100 ya Katiba inayompa kinga mbunge
anapotoa jambo lolote bungeni, kwa kuwa yeye hakuzungumza bungeni kama
mbunge, bali alikuwa anatoa msimamo wa Serikali yake. Akizungumza
hivi karibuni, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alisema hakuna uhalali wa
mashitaka hayo kwa sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua,
alichosema ni kupiga wale wasiotaka kutekeleza amri halali na kuna
sheria inayoruhusu wananchi kupigwa pindi wanapokaidi amri.
No comments:
Post a Comment