Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
imempongeza Mzee Muhidini Gurumo kwa mchango wake uliotukuka katika
tasnia ya Muziki nchini pamoja na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
Akiwasilisha barua ya Serikali ya kutambua mchango wa nguli huyo juzi
nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Bibi. Lilly Beleko amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini
mchango wake katika muziki wa Dansi hapa nchini.
‘Serikali inathamini mchango wako katika Muziki hapa nchini na
itaendelea kuzienzi kazi hizo na inakupongeza kwa kazi nzuri ulioifanya
ya kuelimisha, kuhamasisha na kuburudisha jamii’. Amesema Bibi. Beleko.
Naye Rais wa Shirikisho la Muziki nchini, Bw. Addo Mwasongwe, amesema
kuwa Shirikisho linampongeza kwa kazi zake nzuri na litaendelea kumtumia
katika kazi za muziki ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri katika tasnia
hiyo.
Nguli huyo wa muziki wa dansi nchini katika enzi zake za uimbaji
ametunga nyimbo za kuelimisha jamii kufanya kazi kwa bidii, kudumisha
usawa, amani na kuwakumbusha wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea
watoto katika maadili mema.
Mzee Gurumo ambaye ameanza kazi ya muziki mnamo miaka ya 1960 na
kustaafu kazi hiyo mwaka huu amesema kuwa anaishukuru Serikali kwa
kutambua kazi yake na amefarijika kwa kukabidhiwa barua ya kumtambua na
kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bibi. Lilly Beleko kutoka
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akimkabidhi Mzee
Muhidini Gurumo barua kama ishara ya Serikali kutambua mchango wake
uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini pamoja na kumpongeza kwa
kustaafu kazi kazi hiyo, hivi karibuni nyumbani kwake Makuburi, Jijini
Dar es Salaam. Wanaoshuhudia nyuma ya Mkurugenzi ni Rais wa Shirikisho
la Muziki Tanzania, Bw. Addo Mwasongwe na kulia pembeni ya Mzee Gurumo
ni Mkewe, Bibi. Pili Said Kitwana.
Nguli wa Muziki wa
Dansi, Mzee Muhudini Gurumo (aliyevaa shati la drafti) akiwa na
watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
walipomtembelea nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar es Salaam hivi
karibuni. Serikali kupitia Wizara hiyo ilimkabidhi barua rasmi Mzee huyo
kutambua mchango wake katika tasnia ya Muziki na kumpongeza kwa
kustaafu kazi hiyo. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Utamaduni, Bibi Lilly Beleko, wa pili ni mke wa Mzee Gurumo, Bibi. Pili
Said Kitwana na wa Pili Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara
Upande wa Sanaa, Bibi. Joyce Hagu. Picha zote na Concilia Niyibitanga
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
No comments:
Post a Comment