Pages

Translate

Monday, 9 September 2013

AFISA TARAFA AMBAKA MAMA LISHE NJINI TABORA


AFISA Tarafa ya Kaliua Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Josephat Brown anatuhumiwa kumbaka mama lishe na kumsababishia maumivu makali na kisha kutokomea kusikojulikana.

Tukio hilo limetokea Agosti 29 mwaka huu, saa tano usiku nyumbani kwa afisa tarafa huyo baada ya kumrubuni mama huyo (jina) mwenye miaka (38) katika baa iitwayo Leaders akitaka ampelekee nyama ya kuku ana wageni.

Kwa mujibu wa maelezo ya mama huyo katika kituo cha polisi wilaya ya Kaliua, siku hiyo wakati akiuza nyama ya kuku wa kukaanga kwenye baa, mtuhumiwa alimuomba ampelekee kitoweo hicho nyumbani.

Alisema kuwa baada ya kukubali waliongozana naye hadi nyumbani kwa afisa tarafa huyo na baada ya kufika alimuamru amsokotee bangi iliyokuwa mezani huku akiwa amemshikia kisu akimtisha kumuua.

Baada kusokotewa bangi hiyo, afisa huyo aliivuta huku akimpulizia moshi mama lishe usoni na baada ya kumaliza alimshikia kisu tena na kumuamuru avue nguo wafanye mapenzi.

Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa mama huyo aligoma kufanya tendo la ndoa, ndipo afisa tarafa alipomuingilia kwa nguvu hali ambayo ilizusha tafrani kidogo.

Baada ya kubakwa, mama huyo alipata upenyo na kukimbilia kwa wasamaria wema ambapo alisaidiwa kufika kituo cha polisi na kuandikisha maelezo ya tukio hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Saveli Maketa alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa afisa tarafa huyo hadi sasa hajulikani alipo.

“Tukio hilo kweli lipo na limeripotiwa kituo cha polisi na linachunguzwa lakini mtuhumiwa ametoweka karibu wiki nzima sasa hajafika kazini bila ya taarifa zozote na ofisi yake hadi sasa imefungwa,” alisema.

Aliongeza kuwa jalada la kesi hiyo Kumb/RB/1058/2013 limefunguliwa polisi na maelezo ya kina juu ya tukio hilo yameshafikishwa kwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora, Peter Ouma.

Maketa alisema kuwa afisa tarafa huyo alikuwa ofisini kwake na kwamba aliwahi kumuonya juu ya matumizi ya bangi na dawa za kulevya ambazo alikuwa akitumia.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Peter Ouma, alisema suala la afisa tarafa kutuhumiwa kumbaka mama lishe bado halijamfikia mezani kwake, hivyo hawezi kulizungumzia hadi hapo atakapopata taarifa sahihi toka OCD wilaya ya Kaliua.

No comments:

Post a Comment