MAZISHI ya kufuru ya yule bilionea
mfanyabiashara wa madini ya tanzanite mkoani hapa, marehemu Erasto Saimon
Msuya, yameacha gumzo kubwa.
Mfanyabiashara huyo aliuawa kwa kumiminiwa
risasi zaidi ya 20 na watu wawili wasiojulikana Agosti 7, mwaka huu maeneo ya
Kia wilayani Hai, Kilimanjaro kabla ya kupumzishwa Jumanne wiki hii kijijini
kwao Kairo huko Simanjiro mkoani Manyara.
Baada ya kutokea kwa mauaji hayo, iliundwa
kamati ya mazishi ikihusisha wafanyabiashara wa madini ya tanzanite pekee
ambayo ilitengeneza bajeti ya maziko ya tak
ribani shilingi milioni 100.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zilieleza
kuwa gari maalum la kifahari na jeneza lililobeba mwili vilinunuliwa Nairobi
nchini Kenya.
Jeneza lake
INASEMEKANA kuwa jeneza hilo liliagizwa na
kampuni inayojishughulisha na shughuli za maziko ya Montezuma & Monalisa
Funeral Home.
Ilielezwa kuwa jeneza hilo lilinunuliwa
shilingi milioni nane ikidaiwa kuwa lilikuwa lina uwezo wa kufunga na
kufunguliwa kwa kutumia ‘rimoti’.
Ilidaiwa kuwa jeneza hilo lilikuwa na vishikio
maalum vilivyokuwa viking’aa kama dhahabu au tanzanite na kulifanya kuonekana
la aina yake.
Hali hiyo iliwaacha na mshangao maelfu ya
waombolezaji waliofika kuaga mwili wakati wa ibada iliyofanyika nyumbani kwa
marehemu, maeneo ya Kwaiddi, barabara inayoelekea Ngaramtoni wilayani Arumeru
kabla ya kusafirishwa kwenda Simanjiro kwa maziko.
Pamoja na lile lililobeba mwili wa marehemu,
msafara wa magari ya kifahari kuelekea kijijini huko ulisababisha Jiji la
Arusha kuzizima kwa majonzi huku wengi wakishindwa kuamini kama jamaa huyo
amefariki dunia na kuacha utajiri wa kutisha.
“Hebu ona, hakuna gari la ovyo, yote ni
makali. Ingekuwa utajiri unaweza kumfufua mtu, basi Erasto angefufuliwa,”
alisema mmoja wa waombolezaji akimwelezea jamaa huyo kuwa alikuwa mtu ‘smati’.
Habari za ndani zilidai kuwa hata suti
aliyozikwa nayo ilitoka nje ya nchi, London, Uingereza kwa Malkia Elizabeth.
Pia ilidaiwa kuwa jamaa huyo alizikwa na cheni
ya dhahabu (gold) shingoni yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10.
Habari zilinyetisha kuwa huduma kama vyakula,
vinywaji, mapambo na magari ya kukodishwa kutoka Arusha kwenda kijijini na
kurudi viligharimu zaidi ya shilingi milioni 80.
Ili kuthibitisha kuwa msiba huo haukuwa wa kitoto,
Msema Chochote ‘MC’ alikuwa ni staa mkubwa wa filamu za Kibongo, Jacob Steven
‘JB’.
Habari zilidai kuwa waombolezaji walipofika
kijijini kwa ajili ya maziko Jumanne mchana, watu walikanyagana makaburini huku
vijana wakitaka azikwe na mtu hai wa kumlinda.
Walipofika walikuta kaburi la kifahari
limeshajengwa ambapo kulikuwa na zulia maalum la kufuta miguu kabla ya
kukanyaga marumaru za madini ya tanzanite zilizolizunguka.
Kuthibitisha kuwa ilikuwa ni kufuru, baadhi ya
wachimbaji wadogo ‘nyoka’ walikuwa wakiwataka matajiri kulifungia kaburi hilo
umeme na kiyoyozi.
Baada ya mazishi hayo, inaelezwa kuwa familia
ilikubaliana kufanya juu chini kulinunua shamba alilouliwa katika Mji wa
Bomang’ombe, Mtaa wa Wasomali eneo la Mjohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro ili
kujenga mnara wa kumbukumbu.
Ilidaiwa kuwa baada ya kujenga mnara huo,
familia itakuwa inatembelea eneo hilo Agosti 7, kila mwaka kwa ajili ya
tambiko.
Kaka wa marehemu, Israel Msuya, alisema kuwa
walifikia uamuzi wa kufanya mazishi hayo kwenye makaburi ya familia ya mzee
Elisaria Msuya ‘Kikaango’ ambaye ni baba wa marehemu Erasto.
Kwa mujibu wa kaka huyo wa marehemu, familia
haitalipiza kisasi kwa watu waliomuua Erasto bali wao wanamwachia yote Mungu.
Kuhusu kesi
Katika hatua nyingine, polisi mkoani hapa
wanaendelea kuwahoji wafanyabiashara maarufu wa madini ya tanzanite wa mji
mdogo wa Mererani wanaodaiwa kuhusika na kifo hicho.
No comments:
Post a Comment