Mwanamke avunjwa nyonga na kunyolewa nywele kwa kisu na mume wake
Tajiri ambaye ni mfanyabishara mkubwa katika maduka ya Kariakoo, Dar aliyetajwa kwa jina moja la Urio anadaiwa kumvunja nyonga na kumjeruhi mkewe Eva Pascal anayeuguza majeraha kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akizungumza kwa uchungu akiwa wodini hospitali hapo, Eva au mama Tina alisema kuwa tukio hilo lilitokea hivi karibuni nyumbani kwao Kimara-Temboni, Dar.
Mama Tina alisimulia kuwa siku ya tukio mumewe alikuwa ana siku kadhaa hajarudi nyumbani hivyo akamfuata katika Baa ya Temboni Resort kwa ajili ya kumuuliza sababu za kushindwa kurudi nyumbani.
Alisimulia huku akitokwa machozi: “Nilipofika tu nikamuuliza swali hilo, alinitandika kofi kisha akanipiga ngumi ya jicho hadi nikazimia.
“Nilishangaa nilipozinduka na kuwakuta manesi wamenizunguka. Nilipomuuliza mume wangu imekuwaje aliniambia eti nililewa na kuanguka ndiyo sababu nipo hapa.
“Kiukweli baba Tina ananinyanyasa sana, ananipiga hadi kufikia hatua ya kuniunguza na pasi. Kwa sasa naiona ndoa ni mateso makubwa na Mungu akinijalia nikapona, sitarudi tena katika mateso haya, nimechoka jamani.
“Ni baba Tina huyuhuyu aliwahi kuninyoa nywele na kisu eti kisa tu nilimcheleweshea supu ambayo ilikuwa bado haijaiva ikiwa jikoni. Alinichukua akaniingiza chumbani akaninyoa nywele na kisu kisha akaniingiza bafuni akaniosha na maji baridi eti akidai nywele hizo zilikuwa zinanipa kiburi.
“Yaani nikikorofishana naye kidogo tu ananitupia kila kitu nje na kufunga chumba chetu cha kulala.”
Baada ya kusikia upande wa mama Tina, Ijumaa ilimgeukia baba Tina ambaye alikanusha kumpiga mkewe lakini akakiri kuwa aliwahi kumpiga na kumchoma na pasi huko nyuma ingawa walishakaa na kuyamaliza mambo hayo.
“Safari hii sijampiga kabisa, alikuja baa akanifanyia fujo, alikuwa amelewa sana, baadaye alianguka na kuumia ndiyo nikampeleka hospitalini, hayo mengine watu wananisingizia tu,” alisema baba Tina.
Hata hivyo, mwandishi wetu hakuishia hapo kwani alitinga eneo la Kimara-Temboni nyumbani kwa wanandoa hao na kuzungumza na baadhi ya majirani ambao walikiri kuwa mama Tina alipigwa na amekuwa akinyanyaswa na mumewe kiasi cha kufikishana polisi.
Wanahabari wetu walifika polisi katika kituo kidogo cha Kimara-Temboni ili kupata taarifa ya tukio hilo ambapo walisema kuwa Urio alifika kituoni hapo akiwa na mkewe mahututi na kuomba PF-3 ambapo walimpa na kumsihi mgonjwa akishapokelewa hospitalini airudishe lakini siku iliyofuata alikwenda pale na kusema kuwa mgonjwa anaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment