MAANDAMANO YA CHADEMA HUKO JIJINI MWANZA
MAANDAMANO ya amani yaliyokuwa yameandaliwa na chama cha demokrasia na
maendeleo(chadema) yamegeuka shubiri kwa wakazi wa jiji la Mwanza baada
ya kuibuka mapambano makali baina ya waandamanaji hao na jeshi la polisi
mkoani Mwanza na kusababisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi
wa chama hicho.
Maandamano hayo ya amani ambayo yalianzia katika eneo la Buzuruga nje
kidogo ya jiji la Mwanza yalikuw ayakiongozwa na wabunge Highness Kiwia
wa Ilemela pamoja na Ezekiel Wenje kuelekea katika viwanja vya
Furahisha yalilenga kumshinikiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo
kutoa barua zinazodaiwa kuandikwa na ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi
kuwarejesha madiwani watatu waliotimuliwa katika Manispaa ya Ilemela
kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo.
Polisi wenye silaha pamoja na askari kanzu walianza kutanda katika eneo
hilo la Furahisha wakiongozwa na Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai
Mkoa wa Mwanza RCO Konyo ambaye alikuwa akitumia gari lenye namba za
usajili DK 068EXV aina ya Toyota Land Cruiser
Maandamano hayo ambayo awali yalionekana kana kwamba yangelimalizika
salama yaliwasili katika viwanja vya Furahisha majira ya saa 5.38 huku
yakiongozwa na gari la polisi lenye namba za usajili za nchi ya Uganda
779 UAG likiwa nimesheheni polisi wenye silaha nzito ikiwa ni pamoja na
mabomu ya machozi na bunduki pamoja na askari kadhaa ambao walikuwa
katikati ya maandamano hayo.
Baada ya maandamano hayo kuwasili katika viwanja vya Furahisha kwa
amani,waandamani hao ambao walikuwa na mabango mbalimbali yaliyosomeka
kuwa ‘Matata hatutaki uendelee kuwa Meya wa Ilemela rudia kazi yako ya
awali, na jingine Jaji Sumari tumechoka kuahirisha mara kw amara kesi
dhidi ya Matata na jingine lililosomeka kuwa RD Ndikilo tunahitaji
barua za kurejeshwa kwa madiwani wetu.
Hata hivyo tofauti na ilivyokuwa imetangazwa kuwa maandamano hayo ya
amani yangelipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo,hakukuwa
na kiongozi yoyote wa Serikali ambaye alikuwepo uwanjani hapo kupokea
maandamano hayo.
Kufuatia kutoonekana kwa kiongozi yoyote wa Serikali,viongozi wa chadema
pamoja na wabunge wao walikutana kwa faragha kwa dakika kadhaa kwa
ajili ya kujua hatima ya maandamano hayo ambapo Mbunge wa Nyamagana
Ezekiel Wenje alipanda jukwaani saa 6.45 na kuwaeleza maelfu ya
waandamanaji kuwa wameamua kumtuma Mbunge wa Ilemela Highnes Kiwia
kwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuchukua majibu kwa ajili ya
kuwaletea wananchi walioandamana juu ya hatima ya madiwani hao.
Hata hivyo saa moja baadae Mbunge huyo alisimama jukwani na wakuwaeleza
waandamani hao kuwa simu ya Mbunge Kiwia ilikuwa haipatikani hivyo
kuwataka kuandamana kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza kujua kulikoni na
hapo ndipo hali ya hewa ilipochafuka.
Jeshi la polisi baada ya kuona wandamanaji hao wameanza kuelekea katika
ofisi za Mkuu wa mkoa liliwataka kutawanyika ambapo waandamanaji hao
walikaidi ndipo jeshi la polisi lilipoamua kutumia mabomu ya machozi
kuwatawanya wafuasi hao.
Vurugu hizo ambazo zilianza majira ya saa 7.30 zilisababisha kufungwa
kwa baadhi ya barabara kutokana na waandamanji hao kuweka vizuizi vya
mawe na kuchoma matairi,ambapo pia maduka na ofisi mbalimbali
zililazimika kufungwa kwa muda kupisha vurugu hizo.
Baadhi ya wananchi ambao walikuwa wakitumia usafiri wa umma walionekana
wakishuka kupitia katika madirisha ya magari hayo na kukimbia kwa hofu
ya kujeruhiwa na mabomu pamoja na mawe ambayo yalikuwa yakirushwa na
waandamanji hao kwa jeshi la polisi.
MKUU WA MKOA WA MWANZA ALONGA
Mkuu wa mkoa wa Mwanza akizungumza na Mbunge Kiwia pamoja na viongozi wa
chadema ofisini kwake alisema kuwa ameshangazwa na uvumi huo kuwa ofisi
yake imekalia barua a kurejeshwa kwa madiwani Abubakar
Kapera(Nyamanoro),Dan Kahungu(Kirumba) pamoja na Marietha
Chenyenge(Ilemela).
RC Ndikilo alisema kuwa Serikali imekuwa ikifanya kazi zake kwa
maandishi na sio kwa kufuata maneno ya mtaani na kueleza kuwa hana barua
yoyote toka ofisi ya Waziri Mkuu inayomualifu kuhusu kuwarejesha
madiwani hao baada ya kukata rufaa.
“Hata Mbunge kuna siku ulinipigia simu ukiniuliza juu ya kuwepo kwa
barua hizo name nilikujibu kuwa kwa kuwa uko hapo Bungeni Dodoma ambapo
pia kuna ofisi ya Waziri Mkuu nilikujibu kuwa ni muhimu ukawaona
viongozi wakuu wa Tamisemi ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu,pia
nilikushauri kuwa wakupe japo nakala ya barua hiyo”,alisema RC Ndikilo.
“Lakini cha kushangaza nimekuwa nikisikia maneno ya ajabu kuwa nimeficha
barua za madiwani hao,ikumbukwe kuwa madiwnai hao hawakukata rufaa
kwangu bali walikata rufaa ngazi ya juu kabisa,ili kukata mzizi wa
fitina naomba kati ya tarehe 26 hadi 27 wewe Mbunge pamoja na mimi
twende TAMISEMI kukutana na viongozi ili kukata mzizi wa fitina na tuje
tuwaeleze wananchi ukweli uliopo”,alisema RC Ndikilo.
Kuhusu suala la Meya Henry Matata kutoondolewa madarakani RC Ndikilo
alisema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kw akuheshimu mamlaka ya
mahakama na kuwataka chadema kuvuta subira hadi pale mahakama itakapotoa
maamuzi yake.
KAULI YA MBUNGE KIWIA
Akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Kiwia alisema kuwa
waliamua kuitisha maandamano hayo kutokana na kuelezwa na Waziri Hawa
Ghasia kuwa tayari barua hizo zimeishatumwa mkoani Mwanza.
“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa hawa madiwani waliosimamishw ani wawakilishi wa
wananchi,wamekaa nje kwa miezi saba sasa na uchaguzi wa Meya haukuwa
halali ndio maana tuliamua kuitisha maandamano kwa ajili ya kuhakikisha
madiwani hawa wanarejeshwa.
RPC MANGU
Akizungumza kwa simu juu ya kutokea kwa vurugu zilizosababisha kupigw
akwa mabomu ya machozi,Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ernest Mangu
alisema kuwa polisi walifanikiwa kudhibiti vurugu hizo na hadi sasa
hawezi kusema ni wananchi wangapi ambao walikamatwa kuhusu vurugu hizo.
WANANCHI WAWALAUMU VIONGOZI NA WANASIASA NA KUWAPONGEZA POLISI.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mtanzania juu ya vurugu zilizotokea
waliwaonyoshea kidole wanasiasa pamoja na viongozi wa mkoa wa Mwanza
kutokana na kushindwa kusema ukweli juu ya tukio hilo.
Baadhi walisikika wakisema kuwa kama barua zipo kweli madiwani hao
wanapaswa kupewa na kama azipo basi walioeneza maneno hayo wachukuliwe
hatua kali kutokana na uchochezi.
Wananchi hao pia walilipongeza jeshi la polisi kutokana na kutumia
busara badala ya nguvu kuhakikisha maandamano hayo yanakuwa ya amani.
No comments:
Post a Comment