 
 
SHAHIDI wa tano katika kesi ya kutorosha wanafunzi inayomkabili 
Mchungaji wa Kanisa la TAG, raia wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo 
(DRC), Jean Felix Bamana ameieleza mahakama namna alivyolazimishwa 
kufanya mapenzi na mchungaji huyo.
Shahidi huyo, Angela Swai (19), akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu, 
Naomi Mwerinde wa Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi, alisema Mchungaji huyo
 alimlazimisha kufanya kitendo hicho jaribio ambalo lilishindikana 
kutokana na mshitakiwa huyo kukataa kutumia kondomu.
Akiongozwa na mwendesha mashtaka, wakili wa serikali, Esther Majaliwa, 
katika ushahidi wake, Shahidi huyo alieleza Mahakama hiyo alivyokutana 
na mshtakiwa kwa mara ya kwanza na mara ya pili ambapo alisema alikutana
 naye kupitia marehemu mama yake mzazi huku mara ya pili akikutana naye 
kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Shahidi huyo alieleza mahakamani hapo kuwa alikutana na mshtakiwa kwa 
mara ya kwanza kupitia mama yake na alimtambulisha yeye na mdogo wake 
aliyemtaja kwa jina la Arthur kuwa mchungaji huyo ni baba yao mwingine 
na waliendelea kufahamiana kwani alikuwa ni rafiki mkubwa wa mama na 
mshirika wake katika Biashara ya Madini.
Alisema kwa kipindi kirefu hakuwahi kumuona hadi alipokutana naye kwa 
mara ya pili mwaka jana kupitia mtandao wa Facebook ambapo alimwomba 
urafiki kwa nia njema kwani alikuwa ni rafiki mkubwa wa marehemu mama 
yake, na kuongeza kuwa mawasiliano yalikuwa ni ya kawaida tu.
Shahidi huyo alisema baada ya hapo mshtakiwa alianza kumsisitiza kuhamia
 Dar es Salaam kwa ahadi ya kumsaidia kuendelea na masomo baada ya 
kumueleza amefukuzwa shule jambo ambalo yeye binafsi alilikataa.
Alisema baada ya kukataa kukubaliana na wazo la kwenda Dar es Salaam, 
mshtakiwa huyo alimwambia atafika Moshi ambapo alifikia katika Hoteli ya
 Moshi View, Februari 14, mwaka huu na kufanya naye mawasiliano kupitia 
simu ya mdogo wake aliyetajwa mahakamani hapo kwa jina la Arthur Swai, 
akimtaka kumfuata hotelini hapo.
 
 
No comments:
Post a Comment