Pages

Translate

Sunday, 21 July 2013

SIRI YAFICHUKA NYARAKA ZAONYESHA TENDWA ALIIBARIKI 'RED BRIGADE' YA CHADEMA...MWENYEWE ASHANGAA



 Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa

  • Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri,
  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed    Seif Khatib;
  • Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu;
  • Inspekta Jenerali wa Polisi na
  • Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai

LICHA ya kuwapo kwa shutuma mbalimbali zinazopinga mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzisha kikundi cha kujihami cha Red Brigade kitakachotoa ulinzi kwa viongozi wao, imebainika kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa alitoa baraka za kuanzishwa kwake.

Tanzania Daima imeona nakala ya barua ya mwaka 2005 kutoka katika ofisi ya Tendwa, ikionyesha kubariki jambo hilo ambalo katika siku za hivi karibuni limezua gumzo kubwa na kusababisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuhojiwa na polisi kuhusiana na kauli zake.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa Desemba 30, 2004 ofisi ya msajili wa vyama siasa ilimwandikia Katibu Mkuu wa CHADEMA barua yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/29 ikitaka ufafanuzi baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa chama hicho kinataka kuanzisha kikundi cha kujihami (Red Brigade). “Kulingana na Ibara ya 9 (2) (c) ya Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa 1992, ibara ya 147 na 148 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi, kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kinyume cha sheria hizo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo ambayo Tanzania Daima inayo iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa, inaeleza kuwa kuvunjwa kwa sheria hizo kutasababisha CHADEMA kufutwa. CHADEMA baada ya kupata barua hiyo, Januari 6 mwaka 2005 iliijibu kuwa kikundi kinachozungumziwa ni walinzi wa ndani ya chama, vijana wa kike na wa kiume, wanachama wa CHADEMA, watu wasio na silaha, chini ya usimamizi wa kurugenzi ya ulinzi na usalama ya chama hicho. “Kikundi kinachokusudiwa kuundwa ni kutokana na Katiba ya CHADEMA ambayo inaruhusu uundwaji wa Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama chini ya Katiba ya CHADEMA, kifungu cha 7.6.4 (h),” inaeleza barua ya CHADEMA yenye kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/64 iliyosainiwa na Suzan Kiwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CHADEMA. Chama hicho kiliilaumu serikali kwa vitisho ilivyotoa vya kutaka kukifuta endapo kingeendelea na kusudio la kuanzisha kikundi hicho.

Barua ya ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini ya kuithinisha uanzishwaji

Hata hivyo, baada ya ufafanuzi huo, Januari 11 mwaka 2005, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ilipopata majibu hayo ya CHADEMA, ilieleza kuwa kwa madhumuni yaliyoelezwa na chama hicho inakubaliana na malengo ya kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama. “Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwa madhumuni mliyoyatoa kwenye barua yenu C/HQ/ADM/62 inakubaliana na maelezo yenu ya kuanzishwa kwa kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama ingawa Katiba ya CHADEMA haijatoa ufafanuzi huo, vinginevyo tunawatakia kila la heri kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho,” ilisema barua ya msajili wa vyama vya siasa nchini.

Barua hiyo yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/32 iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa nchini, pia iliwatakia kila la heri CHADEMA kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho.

Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed Seif Khatib; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu; Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.



No comments:

Post a Comment