Pages

Translate

Monday, 22 July 2013

MNYIKA AKOSWA NA BOMU ALIPOKUWA AKIHUTUBIA JANA

LILIRUSHWA NA POLISI ALIPOSIMAMA


    VITUKO na matukio ya hatari kwenye mikutano ya CHADEMA vimeendelea kushika kasi. Jana Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa na bomu la machozi lililorushwa na polisi waliokuwa wakizuia kufanyika mkutano ulioitishwa na chama hicho. Tukio hilo lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye viwanja vya Sahara ambapo bomu hilo lilimpata mtu aliyekuwa karibu na Mnyika anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa sehemu ya paja. Baada ya kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka kumchukua majeruhi huyo ili wamweke kwenye gari lao apelekwe hospitalini, lakini Mnyika aliwaelekeza wafuasi wa CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo kilichofanywa na askari hao kililenga kuficha ushahidi wa jambo hilo.

      Polisi waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na matakwa ya wafuasi wa CHADEMA waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali ambako hali yake inadaiwa inaendelea vizuri. Akielezea hali ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema polisi walifika katika viwanja vya Sahara wakiwa na magari matatu kwa lengo la kutawanya wafuasi wa CHADEMA wasifanye mkutano wakidai haukuwa na baraka za jeshi hilo. Mnyika alisema polisi hao walisema sababu ya kuuzuia mkutano huo ni uwepo wa ziara ya Makamu wa Rais katika Wilaya ya Kinondoni, hivyo walikuwa wameelekeza nguvu zao katika ziara hiyo, kwamba hawakuwa na uwezo wa kuulinda mkutano wa CHADEMA.

       “Nikiwa nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi walikuja kusema tuache tusifanye mkutano, nilisogea karibu na gari kumlalamikia ofisa wa polisi kwani kitendo cha kuahirisha mkutano kwa barua waliyoileta saa sita mchana siku ya mkutano wakati sisi tuliwapa taarifa siku nne zilizopita ilikuwa sio haki. “Nilimwambia ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa najadiliana kwa simu na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema kumlaumu kutumika vibaya kwa Jeshi la Polisi. “Nilipokuwa bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu lilirushwa kutoka ndani ya gari ya polisi na kupita karibu na mimi likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu yangu, ki ukweli nimeshangazwa sana na matumizi mabaya ya silaha za moto,” alisema. Aliongeza kuwa katika purukushani zilizotokea baada ya bomu kupigwa, alipoteza nyaraka mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi kuwaonyesha wafuasi wa chama hicho hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge wake walivyopitisha kodi ya huduma za simu, na kodi ya laini za simu.

Slaa anena

    Aidha katika mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa ungehutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza kuhutubiwa naye kwa kile alichosema kuwa watu wake wa usalama walimwambia mapema hali si salama kwenye mkutano huo. “Nilipata taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi walikuwa na mpango wa kuleta fujo, hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda nisingeenda kuhutubia, pengine bomu lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu au kwa mwingine,” alisema Dk. Slaa alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya kutoonekana mkutanoni.

Zuio la polisi

     Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana liliahirisha mkutano huo wa CHADEMA kabla viongozi hao kupanda jukwaani. Liliwapelekea barua ya zuio CHADEMA inayosomeka: “Kumbuka barua ya tarehe 17 Julai, yenye kumb. CHADEMA/MKT/UBUN/015/2013 uliyomwandikia Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam. Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam amezuia kufanyika kwa mkutano huo tarehe 21 Julai 2013 katika viwanja vya Sahara, Mabibo kwa sababu siku mliyoomba kufanya mkutano wenu wa hadhara, Wilaya ya Kinondoni ina mapokezi ya ugeni wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Hata hivyo Mnyika alipinga sababu hiyo ya polisi kwa madai CHADEMA wamepeleka taarifa kwa Jeshi la Polisi tangu Julai 17 kwamba wangefanya mkutano katika viwanja hivyo Julai 21, lakini jeshi hilo halikuwajibu hadi walipokuwa wanaenda mkutanoni.

CHADEMA wabadili mbinu

       Kutokana na kuzuiwa kufanya mkutano kwenye viwanja vya Sahara, CHADEMA waliamua kuufanyia Ubungo kutokana na kuomba vibali viwili kwenye maeneo tofauti. Baada ya kuzuiliwa Mabibo, kibali cha Ubungo kilikuwa halali, hivyo Mbunge wa Ubungo aliyekuwa amefika Sahara kwa ajili ya kuhutubia, aliandamana kwa miguu na wafuasi wa chama hicho hadi Ubungo, huku kukiwa na makachero wengi wa polisi waliofuatilia maandamano hayo. Akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema polisi walifanya kitendo cha kikatili, kusubiri watu wamalize maandalizi, wakusanyike uwanjani ndipo wanaleta barua ya kupiga marufuku mkutano kwa kisingizio kuwa katika Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na ziara ya makamu wa Rais katika Jimbo la Kawe na Kindondoni.

       “Sisi tupo Ubungo, Makamu wa Rais yupo Kawe na Kinondoni, sasa suala la kuzuia mikutano isifanyike lilikuwa na maana gani? Kama Jeshi la Polisi walisema hawana askari wa kutosha kulinda mkutano wetu mbona katika kuutawanya wamekuja na magari matatu?” alihoji. Mnyika alitumia muda mwingi kulilaumu Jeshi la Polisi, kwanza kwa kuahirisha mkutano muda mfupi kabla ya viongozi kupanda jukwaani, lakini pia kitendo cha kurushwa bomu mahali ambapo hakukuwepo fujo zozote.

Madudu zaidi ya CCM
   
      Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameendelea kuanika madudu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), safari hii akitoa nyaraka za mikakati ya chama hicho tawala kufundisha vijana kukabiliana na wapinzani. Akihutubia mkutano wa hadhara juzi katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo, Nguzo Nane, mjini Shinyanga, Mbowe alisema kuwa ili kujilinda dhidi ya vitendo alivyodai wanafanyiwa na vijana wa Green Guards - kikosi cha vijana wa CCM, chama chao kitaendelea na mipango ya kuwapatia vijana wao mafunzo ya ukakamavu. Mbowe alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha kuwa chama hicho tawala kupitia wanachama wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) kimekuwa kikitoa mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake, huku nyaraka moja ikionyesha kuwa moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kukabiliana na upinzani.

      “Tunashambuliwa, watu wetu wanapigwa, wanateswa, wanatekwa na wengine kuuawa, kwa sababu tu wanataka mabadiliko na wanapenda CHADEMA, majuzi mlisikia Waziri Mkuu Pinda anasema wamechoka...sasa tunasema Pinda kama umechoka ondoka upishe ofisi ya umma hiyo, upishe kwenye ofisi ya watu kama umechoka, maana kuchoka huko ni kuchoka kwa CCM. Pisheni ofisi sio za kwenu hizo, ni za Watanzania. “Wananchi hapa mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM, moja ni cheti cha kuhitimu mafunzo na nyingine hapa juu imeandikwa ‘Sera za Msingi za CCM’, sasa mi sitawasomea, naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote anayejua kusoma, awasomee mjue tunaposema CCM wamekuwa na kikundi kinachoshambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua Watanzania wenzao eti tu kwa sababu wanaunga mkono CHADEMA, huwa tunamaanisha nini,” alisema Mbowe.

       Mmoja wa wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara, ambao ulikuwa ni sehemu ya shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya Ziwa Mashariki (mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa na kusoma sehemu inayozungumzia majukumu ya jumuiya za chama hicho. Gazeti hili pia lilifanikiwa kuona kabrasha hilo kwa karibu, ambapo kifungu cha 9.1 kinachozungumzia UVCCM, kinasomeka hivi;

 “(i) Umoja wa vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana katika itikadi, ukakamavu na mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana wenye ari ya kutimiza wajibu wao wakiwa walinzi wa chama, viongozi na wagombea wa CCM.

 “(i) Utaratibu wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe kwa dhati. Chama kiwe na mipango mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi watakaofaa kuwapatia vijana mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu ya uchaguzi/uraia. Mafunzo ya makambi ya vijana, mbali ya kujifunza nyimbo za hamasa yatilie mkazo pia mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya kihuni vya baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani.”

      Mbowe pia aliwaonyesha wananchi waliofurika kwenye mkutano huo cheti cha mmoja wa watu waliohitimu mafunzo ya makambi ya vijana wa CCM ambacho kilionyesha mhusika alianza mafunzo Juni 27, 2009 na kumaliza Julai 4, 2009, mkoani Dodoma. Cheti hicho kimesainiwa na watu wawili, mmoja mwenye jina la Jumanne Kitundu, akiwa na nafasi ya Katibu wa UVCCM, Dodoma mjini na mwingine, Robert Mwinje, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Wilaya ya Dodoma mjini. Cheti hicho kinaonyesha mhusika (jina linahifadhiwa) alihitimu mafunzo ya masomo ya kanuni ya umoja wa vijana, wajibu wa vijana katika chama, ulinzi na usalama, ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa vijana katika uchaguzi, rushwa, ukimwi, historia ya TANU na ASP pamoja na maadili.

Msimamo wa CHADEMA

       Mbowe alisitiza kuwa CHADEMA kitasimamia azimio la kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho juu ya kuimarisha kitengo chake cha ulinzi na usalama ikiwemo kuanzisha makambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wa chama hicho watakaokuwa na jukumu la kulinda viongozi wao. Ingawa msimamo huo umekuwa ukipingwa na wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na CCM, Mbowe amesisitiza kuwa hawatarudi nyuma juu ya mpango huo utakaoimarisha ulinzi.

Kodi ya laini za simu

      Hoja ya tozo ya simu imekuwa ajenda kubwa kwenye mikutano iliyofanywa na viongozi mbalimbali wa CHADEMA. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Heche alisema kama wananchi wasingeipa ushirikiano CHADEMA na kupinga maovu mbalimbali, CCM ingekuwa imeshauza nchi na wananchi wake. Alisema tozo la laini za simu lilipitishwa wakati wabunge wa CHADEMA walipokwenda Arusha kushiriki maombolezo na mazishi ya marehemu wa tukio la bomu, hivyo serikali ikaona ipeleke jambo hilo lililobarikiwa na wabunge wengi wa CCM. “Maana yake ni nini? Kodi hii kwanza mwananchi maskini kabisa ambaye amedunduliza na kununua simu, atakuwa analipa sawa sawa na matajiri wakubwa, yaani wewe hapa utakuwa unalipa kodi sawa na Reginald Mengi...lakini kama hiyo haitoshi, ukipiga mahesabu utakuwa unalipa kodi takriban shilingi 12,000 kwa mwaka.

    “Serikali hii ya CCM inayowaletea kodi ya sh 12,000 kwa mwaka ndiyo ililazimika kuondoa na kufuta kodi ya kichwa, baada ya CHADEMA kuwa imefanya hivyo kwenye halmashauri zake, kwa kuanza na Hai ambako Mwenyekiti Mbowe alikuwa ni mbunge na Karatu kwa Dk. Slaa. Sasa walifuta kodi ya manyanyaso ya kichwa kwa maelekezo ya CHADEMA iliyokuwa sh 3,000 kwa mwaka, ambapo watu walikuwa wanakimbia nyumba na kujificha maporini, wengine wakaliwa na wanyama, sasa wanataka mlipe kimya kimya, sh 12,000 kwa mwaka. Ni matokeo ya kushindwa kwa sera za CCM,” alisema Heche.

Mkutano wa Geita

     Wabunge wa CHADEMA wanaotoka Kanda ya Ziwa na viongozi wa chama hicho nao waliendelea kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali huku wakilalamikia tozo la laini za simu pamoja na mapendezo ya rasimu ya katiba mpya yaliyotolewa na CCM hivi karibuni yakipinga mambo mengi yaliyopendezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Jana, wabunge hao wa viongozi walifanya mikutano ya hadhara katika mji wa Kasamwa huko Geita na Sengerema mkoani Mwanza ambako walisema CCM imekosa sifa ya kuongoza ndiyo maana maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu kadiri siku zinavyokwenda mbele.

     Wabunge hao pamoja na viongozi na makada wa CHADEMA ambao wapo kwenye msafara wa kuimarisha chama katika kanda hiyo, ni pamoja na Ezekiel Wenje (Mbunge wa Nyamagana), Profesa Kulikoyela Kahigi (Bukombe), Dk. Anthony Mbasa (Biharamulo Magharibi) na Conchesta Rwamlaza (Viti Maalumu – Kagera). Viongozi na makada wengine ni pamoja na mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar Kashaga, katibu wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, Lenatus Kilongozi pamoja na Mwenyekiti wa Wilaya ya Biharamulo Magharibi, George Kasaiza. Akizungumza kwenye mikutano hiyo, Wenje alisema CHADEMA inatarajia kuunda mabaraza ya wananchi kuhusu muundo wa serikali tatu, na wanatarajia kukusanya saini za Watanzania kupinga tozo ya kodi mpya ya laini za simu iliyopitishwa hivi karibuni bungeni.

     Alisema kwa sasa CCM wametoa mapendekezo ya kutaka kusiwepo uwazi wa mikataba, maadili ya umma na haki za binadamu kwenye katiba mpya, na inataka Spika wa Bunge lazima atokane na mbunge, jambo aliloliita ni kuendeleza ukandamizaji kwa wananchi. “Wakati CHADEMA tunataka spika na mawaziri wasitokane na wabunge, CCM wao wamependekeza viongozi hao watokane na wabunge ili waendelee kuwakandamiza Watanzania. CHADEMA tunataka nchi iwe na mawaziri saba tu, na siyo 15 wa pendekezo la tume na 64 waliopo sasa. “Si hilo tu, ibara ya 22 hadi 23 ya rasimu ya katiba mpya, CCM kwa mapendekezo yao wanataka haki za binadamu zisiwepo kwenye katiba mpya ijayo, bali ziwepo kwenye sheria tu. CCM haitaki kuwepo malengo ya taifa kwenye katiba mpya!

   “Tutakusanya saini milioni 10 za wananchi kuhusu mapendekezo ya katiba mpya. Pia tutakusanya saini milioni tano za wananchi kutaka tozo ya laini za simu ifutwe,” alisema Wenje huku akisisitiza uundwaji wa serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Shirikisho.Mbunge wa Biharamuro Magharibi, Dk. Mbasa, mbunge Conchesta, Katibu wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar pamoja na mwenyekiti wa chama hicho Biharamulo Magharibi, Kasaiza waliishutumu serikali kwa kushindwa kuwaondolea umasikini wananchi wake.

      Walisema kwa sasa Watanzania walio wengi wanalazimika kuvaa viatu vya ‘yebo yebo’ kwa sababu ya umasikini unaotokana na kushindwa kwa Serikali ya CCM kuwatumikia wananchi wake kwa kuwanufaisha na rasilimali zilizopo hapa nchini. “Serikali ya chama tawala imekosa sifa ya kuwaongoza wananchi. Tunahitaji tuungane wote kuiondoa CCM mwaka 2015. CHADEMA ni mkombozi wa Watanzania na ndiyo maana wabunge na viongozi wake wanapambana usiku na mchana kutwa kupigania maendeleo ya wananchi,” alisema Dk. Mbasa.

No comments:

Post a Comment