Kibaha/Tanga. Hata kabla ya maziko askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa Darfur, Sudan hayajafanyika, mchumba wa mmoja wa wapiganaji hao, Amina Juma ameonja chungu nyingine baada ya kutimuliwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu mwenza wake.
Amina ambaye inadaiwa kuwa alikuwa akiishi na Fortunatus Msofe aliyekuwa askari katika Kambi ya Msangani, 36KJ Pwani alisema jana: “Kumekuwa na mzozo wa hali ya juu na ndiyo maana tumeshindwa hata kufika Uwanja wa Ndege kuupokea mwili na hata kesho (leo) sidhani kama nitakwenda... kuna mtafaruku mkubwa wakifamilia.”
Baada ya kutimuliwa, Amina ambaye hawakuwahi kupata mtoto na marehemu Msofe, alilazimika kuondoka kwenye nyumba hiyo na kwenda Mlandizi kwa wazazi wake.
“Nimeishi na Msofe kwa miaka mitatu, akiwa kambini mimi niko hapa na wakati mwingine alikuwa analala huku... lakini leo wamenitimua,” alisema huku akilia. Habari zilizothibitishwa na baadhi ya waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema baadhi ya wanandugu walimkana Amina siku chache baada ya kutangazwa vifo hivyo.
Ilidaiwa kwamba Amina alitimuliwa katika nyumba hiyo Ijumaa iliyopita, saa saba mchana baada ya ndugu watatu wa marehemu kufika hapo wakitokea Tanga. Walipofika inadaiwa kuwa walitangaza kusitishwa msiba huo katika nyumba hiyo na kutangaza kutomtambua mke huyo.
Watu hao waliwaeleza waombolezaji kuwa walitumwa na baba mzazi wa marehemu, Willbad Msofe kutoka Kange, Tanga kufika Kibaha kusitisha msiba uliokuwa ukiendelea nyumbani kwa mtoto wake huyo.
Inadaiwa pia kuwa katika msafara huo, alikuwapo mdogo wa marehemu ambaye aliwahi kuishi kwa miaka miwili na Amina hapo Visiga.
Ilidaiwa kuwa walipofika nyumbani hapo walionana na mfiwa, Amina na wazazi wake ambao pamoja na majirani na watu wengine wengi, walikuwa wakimfariji binti yao huyo.
Mmoja wa waombolezaji alisema baada ya salamu wanandugu hao walianza kuulizia mali za marehemu na walikuwa wakimuuliza Amina ambaye aliwaleza kila kitu kilipo na baada ya hapo ndipo walipomweleza kuwa wametumwa na baba wa marehemu kuwa watu hawatakiwi kuomboleza kwenye eneo hilo kwani msiba upo Tanga tu ambako ndiko iliko familia yake.
Alipoulizwa baba wa marehemu, Mzee Msofe alisema: “Mimi ndiye niliyeagiza nyumba ifungwe na ukweli ninamfahamu Amina, lakini simtambui kama mkewe kwa kuwa hawajafunga ndoa... Hata wewe si unayafahamu haya? Uchumba si ndoa na ukifunga ndoa ndipo unatambulika rasmi,” alisema.
Akiwa kwa wazazi wake Mlandizi jana, Amina alisema:
“Namwachia Mungu maana hayo yote nashangaa yanatokea wakati huu mume wangu ‘Fortu’ amekufa, mbona kipindi chote cha miaka mitatu iliyopita familia ya Tanga dada zake na mdogo wake tuliishi nao vizuri kwangu nilipokuwa na marehemu? Nimeishi na ndugu wote lakini hawakuwahi kuhoji, hata nilipokwenda na mume wangu Kange baba na mama Msofe nilikaa nao zaidi ya wiki na hawakunikana, ila nashangaa,” alisema na kulia kwa uchungu.
Akizungumzia kitendo hicho, baba yake Amina, Juma Juma alisema: “Nimeshangaa hizi taarifa. Tulikuwa tunajiandaa kupokea msiba wa mwanetu, lakini leo yanakuja mengine kwa kweli imetushangaza sana.”
“Nasubiri baada ya kumzika marehemu, nitazungumza nao... Kinachonishangaza ni kwamba walituandikia barua ya kumposa binti yangu na tukawajibu na gharama zilikuwa Sh1.2 milioni... Tutazungumza, ngoja hili lipite kwanza,” alisema mzee Juma.
Maisha ya Amina na ‘Fortu’
Akisimulia maisha yao, Amina alisema: “Tulianza kuishi Mbezi Luis mwaka 2010 katika nyumba ya kupanga na nikamshawishi tununue kiwanja na kwa kuwa mimi ni mwenyeji wa Kibaha, niliwatumia marafiki wa familia yangu Mlandizi wakatafutia eneo na mwaka 2011 tulipata na tukaanza ujenzi.
“Tukiwa Mbezi, tulianza kufyatua matofali kisha ujenzi ukaanza Visiga mwaka 2012 mwanzoni na Septemba mwaka huo tulihamia kwenye nyumba yetu na hapo ndiyo ilikuwa makazi yetu hadi marehemu anaondoka kwenda Darfur.
“Wakati wote huo ‘Fortu’ alikuwa keshaniposa na hata barua zote za posa zipo na tulikuwa tukisubiri utaratibu wa kijeshi marehemu kukamilisha miaka sita ya kukaa kambini kisheria ndipo aruhusiwe kuoa.
“Fortu alikamilisha miaka hiyo mwaka 2012 mwishoni na wakati akijiandaa kwa kufunga ndoa ndipo ikatokea safari ya Darfur mwanzoni mwa mwaka huu na tukakubaliana tusitishe kwanza akirudi tukamilishe, lakini haikuwa.... Halafu wananifukuza wanasema hawanijui,” alieleza huku akiangua kilio.
No comments:
Post a Comment