Chadema
cha Demokdrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesisitiza kuwa kitasimamia
azimio la kikao cha Kamati Kuu yake kuhusu kuimarisha kitengo chake cha
ulinzi na usalama na kuibua nyaraka ‘nyeti’ za Chama Cha Mapinduzi (CCM)
zinazoweka hadharani mikakati ya CCM kufundisha vijana kukabiliana na
wapinzani. Pia
kimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuachia madaraka kama amechoka
kuendelea kuwa kiongozi anayepaswa kusimamia misingi ya uongozi bora,
ikiwamo kufuata haki za binadamu, sheria na demokrasia kwa ajili ya
ustawi wa jamii ya Watanzania. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara, katika viwanja vya
Mahakama ya Mwanzo, Nguzo Nane, mjini Shinyanga juzi. Alisema
ili kujilinda dhidi ya vitendo alivyodai wanafanyiwa na vijana wa Green
Guards wanaotoka kikosi cha vijana wa CCM, Chadema itaendelea na
mipango ya kuwapa vijana wake mafunzo ya ukakamavu.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa mji huo
na vitongoji vyake, Mbowe alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha
kuwa chama hicho kupitia wanachama wa Umoja wa Vijana (UVCCM), kimekuwa
kikitoa mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake, huku nyaraka moja
ikionyesha kuwa moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kukabiliana na
upinzani. “Tunashambuliwa, watu wetu wanapigwa, wanateswa, wanatekwa na
wengine kuuawa, kwa sababu tu wanataka mabadiliko na wanapenda Chadema,”
alisema Mbowe na kuongeza: “Majuzi mlisikia Waziri Mkuu, Pinda anasema
wamechoka...sasa tunasema, Pinda kama umechoka ondoka upishe ofisi ya
umma hiyo, upishe kwenye ofisi ya watu kama umechoka. Maana kuchoka huko
ni kuchoka kwa CCM. Pisheni ofisi siyo za kwenu hizo, ni za
Watanzania.”
“Wananchi
hapa mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM. Moja ni cheti cha kuhitimu
mafunzo na nyingine hapa juu imeandikwa: ‘Sera za Msingi za CCM’. Sasa
mi sitawasomea. Naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote anayejua kusoma,
awasomee mjue tunaposema CCM wamekuwa na kikundi kinachoshambulia,
kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua Watanzania wenzao eti tu kwa sababu
wanaunga mkono Chadema, huwa tunamaanisha nini.” Mmoja
wa wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara, ambao ulikuwa ni
sehemu ya shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya Ziwa Mashariki
(mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa
lililoandikwa: “Sera za Msingi za CCM” na kusoma sehemu inayozungumzia
majukumu ya jumuiya za chama hicho.
Kifungu cha 9.1 kinachozungumzia UVCCM kinasomeka kuwa:
‘Umoja wa vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana katika
itikadi, ukakamavu na mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana
wenye ari ya kutimiza wajibu wao wakiwa walinzi wa wa chama, viongozi na
wagombea wa CCM.’ ‘Utaratibu wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe kwa
dhati. Chama kiwe na mipango mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi
watakaofaa kuwapatia vijana mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu
ya uchaguzi/uraia.’ ‘Mafunzo ya makambi ya vijana, mbali ya kujifunza
nyimbo za hamasa yatilie mkazo pia mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la
kukabiliana na vitendo vya kihuni vya baadhi ya vijana wa vyama vya
upinzani,’ inasomeka sehemu ya kitabu hicho cha CCM. Mbowe pia alimwomba
mtu huyo asome cheti cha mmoja wa wahitimu wa kile alichodai ni mafunzo
ya makambi ya vijana wa CCM.
Cheti hicho kinaonyesha mhitimu alianza mafunzo Juni 27, 2009 na
kumaliza Julai 4, 2009, Wilaya ya Dodoma mjini, kimesainiwa na watu
wawili; mmoja mwenye jina la Jumanne Kitundu, akiwa ni Katibu wa UVCCM,
Dodoma Mjini na mwingine, ni Robert Mwinje, Mwenyekiti wa Umoja huo
Wilaya ya Dodoma Mjini. Pia cheti hicho kinaonyesha mhusika (jina
linahifadhiwa) alihitimu mafunzo ya kanuni ya UVCCM, wajibu wa vijana
katika chama, ulinzi na usalama, ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa
vijana katika uchaguzi, rushwa, Ukimwi, historia ya Tanu na ASP pamoja
na maadili. Katika mkutano huo, Mbowe aliwataka Watanzania kuacha
kugombana kwa sababu ya vyama, badala yake wasumbuliwe na waunganishwe
pamoja na matatizo yanayowakabili sasa, ambayo alidai yanasababishwa na
uongozi mbovu wa CCM.
Alisema Chadema inajiandaa kusambaza ushahidi ilionao wenye tuhuma
nzito dhidi ya CCM kushindwa kufanya siasa na kuongoza nchi, badala yake
imekuwa ikishambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua
watu. Ushahidi huo umewekwa kwenye kitabu kimoja ambacho kwa mujibu wa
Mbowe, kitatolewa nakala nyingi, kinaonyesha matukio mbalimbali ya
kisiasa ambayo wananchi wamepigwa, wameumizwa na wengine kuuawa katika
shughuli za siasa, huku uchunguzi huru ukiwa haujawahi kufanyika kubaini
wahusika wa matukio hayo na sheria kuchukua mkondo wake. Mwenyekiti wa
Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche, katika mkutano huo,
aliifananisha kodi mpya ya kadi za simu kuwa ni zaidi ya iliyokuwa kodi
ya kichwa ambayo ilifutwa.
No comments:
Post a Comment