Walioficha mabilioni Uswisi wabanwa
Dar es Salaam. Wakati ikisubiriwa ripoti ya uchunguzi wa Tume
Maalumu iliyoundwa kwa Azimio la Bunge kuchunguza kashfa ya vigogo
walioficha Sh323.4 bilioni katika benki nchini Uswisi, Shirika la
Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo (Eurodad), leo
linaanza kuwachunguza walioficha mabilioni hayo ya fedha nchini humo.
Kazi
hiyo ya uchunguzi inaanza leo hadi Novemba 5, mwaka huu, ambapo pamoja
na mambo mengine watafanya ziara ya uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi
katika kodi katika nchi za Ulaya.
Uchunguzi
huo utafanywa na jopo la wataalamu waliobobea katika masuala ya kodi na
maendeleo na wataongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali
(PAC), Zitto Kabwe ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Sakata
la kashfa hiyo liliibuliwa bungeni kwa hoja binafsi ya Zitto, ambaye
pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, mwishoni mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Kufuatia
hoja hiyo, Bunge chini ya Spika Anne Makinda liliipa Serikali kipindi
cha mwaka mmoja ambacho kinaishia Oktoba mwaka huu, iwe imekamilisha
uchunguzi na kuwasilisha ripoti hiyo bungeni.
Ripoti
ya Tume hiyo iliyoundwa na Serikali kwa Azimio la Bunge ilitolewa
mwishoni mwa mwaka jana, ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), Jaji Frederick Werema, mpaka sasa tayari imewahoji vigogo 200
wakiwamo wabunge, wanasiasa na wafanyabiashara.
Muda
wa tume hiyo kufanya uchunguzi unakamilika mwezi huu na inatarajiwa
katika mkutano ujao wa Bunge unaoanza Oktoba 29 mjini Dodoma,
itawasilisha ripoti hiyo.
Taarifa
zilizolifikia Mwananchi Jumapili na kuthibitishwa na Zitto jana jioni
zilieleza kuwa Eurodad ambao ni mtandao wa mashirika yasiyo ya
kiserikali 48 kutoka nchi 19 za Ulaya, yanayojihusisha na masuala ya
kufuatilia madeni ya nchi zinazoendelea, kwa muda sasa umekuwa
ukipambana na watu wanaokwepa kulipa kodi.
“Mashirika
haya yamekuwa kwenye kampeni ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia
ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya kimataifa kwa nchi
zinazoendelea,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo inaeleza kuwa kesho Zitto atakutana na Waziri wa Fedha wa Uswisi
na maofisa wa benki mbalimbali na asasi za kiserikali zilizopo katika
mji mkuu wa nchi hiyo, Geneva.
“Zitto
pia atahudhuria mkutano wa Kamati ya Kodi ya Umoja wa Mataifa katika
kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za kimataifa ili kuzuia unyonywaji wa
nchi za Kiafrika unaofanywa na kampuni kubwa za kimataifa,” inaeleza
taarifa hiyo.
Juzi
21 mwaka huu, Werema alizungumza na Mwananchi Jumapili na kuthibitisha
kuhojiwa kwa vigogo hao 200, lakini akasita kuwataja kwa majina kwa
maelezo kuwa asingeweza kuwataja kwa kuwa uchunguzi bado ulikuwa
unaendelea.
“Uchunguzi
huo unaendelea,” alisema Werema huku akisita kueleza kwa undani juu ya
kazi hiyo kwa kile alichosema kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa
sasa.
“Subiri uchunguzi bado unafanywa,” alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika tu.”
Uchunguzi
wa walioficha mabilioni ya Uswisi uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya
Uswisi (SNB) kutoa taarifa Juni, 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki
akaunti za benki nchini humo.
Orodha
hiyo iliorodhesha pia baadhi ya Watanzania wenye akaunti zenye fedha
zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.
Jarida
la kimataifa la uchunguzi la ‘The Indian Ocean Newsletter’ toleo la
hivi karibuni, lilimnukuu Werema akisema uchunguzi huo kwa sasa unatia
matumaini.
Mbali
na Werema, tume hiyo inaundwa na viongozi kadhaa wa taasisi nyeti kama
vile Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman na
Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Tume
hiyo inawahusisha pia Mkuu wa Sheria wa BoT, Mustapha Ismail na maofisa
kutoka idara ya upelelezi na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa
Serikali.
Kwa
mujibu wa jarida hilo la kimataifa, miongoni mwa watuhumiwa hao ni
wanasiasa na majenerali wastaafu wanaotuhumiwa kutorosha zaidi ya
Dola133 milioni mwaka 2005, kupitia Mfuko wa Ulipaji Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi
ya watu wanaodaiwa kuhusika wamehojiwa kutokana na taaluma zao, familia
zao, akaunti zao za benki zilizoko nchini na nje ya nchi pamoja na nchi
walizotembelea mara kwa mara kwa miaka mitatu iliyopita.
Lengo
la kuwahoji inaelezwa ni kutaka kujua iwapo walifuata njia zinazotakiwa
katika kufungua akaunti hizo nje ya nchi na iwapo fedha zilizohifadhiwa
huko zilipatikana kihalali.
Akiwa
mkoani Tabora wiki moja iliyopita katika mikutano ya kuimarisha chama,
Zitto alisema tayari amemwandikia barua Katibu wa Bunge kutaka taarifa
ya uchunguzi huo itolewe katika mkutano ujao.
source: Mwananchi
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment