Na Makongoro Oging'
SIRI nzito imefumuka na ukweli
kuanikwa baada ya Rajabu Kandunda, 43, mkazi wa Kigogo Luhanga kufariki
dunia wiki iliyopita jijini Dar es Salaam akiwa na madawa ya kulevya
tumboni.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini
kwamba, Kandunda alifariki dunia wakati akitoa madawa kwa njia ya haja
kubwa nyumbani kwa rafiki yake aitwaye Nassiri Omari Rajabu maeneo ya
Tabata Mawenzi, jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi unaonyesha kwamba marehemu
aliondoka jijini Dar es Salaam Septemba 19, mwaka huu kwenda nchini
Malawi huku akiwa amemeza madawa tumboni aina ya heroine lakini
alipofika Newala, mkoani Mtwara akawa amelemewa na mzigo, hivyo kuamua
kufupisha safari.
Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa
Kandunda zinadai kwamba, baada ya kuona amezidiwa aliwapigia simu ndugu
zake kuwaarifu juu ya kuzidiwa kwake ambapo mkewe aitwaye Mwanaisha
Salim,36, Nassiri Omari,36, na Doto Omari waliondoka Dar es Salaam
Septemba 20 na kumfuata Newala.
“Pamoja na marehemu kuwa na hali mbaya
kiafya lakini wanandugu hao walipofika Dar, hawakumfikishia hospitali
wala nyumbani kwake Kigogo Luhanga bali walimsafirisha hadi kwa
Nassiri, Tabata Mawenzi, kilisema chanzo hicho.
Habari zinadai kuwa alipofika hapo
alipoenda chooni , baada ya muda mfupi akawa amefariki dunia wakati
akitoa dawa kwa njia ya haja kubwa.
Chanzo hicho makini kilieleza kwamba
marehemu alishaanza kutoa madawa lakini pumzi zilimuishia ghafla na
kufia chooni ndipo Doto na mke wa marehemu wakaondoka kwenda Kigogo
kuandaa utaratibu wa msiba.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba kutokana
na kifo hicho cha utata, Doto anadaiwa kutoweka na hajulikani alipo na
jeshi la polisi linamsaka kwa udi na uvumba.
Imeelezwa kuwa mara baada ya marehemu
kufariki dunia mmoja wa wanandugu aliwatonya polisi kuhusiana na kifo
hicho na ilipofika saa 2.00 usiku askari walitinga nyumbani kwa Nassiri
na kumkamata.
Polisi pia walimfuatilia mke wa
marehemu aliyekwenda Kigogo na kumtia mbaroni, hadi leo watu hao wapo
mikononi mwa polisi kwa uchunguzi.
Polisi walichukua mwili wa marehemu
hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi na daktari
alipopasua tumbo lake walikuta madawa aina ya heroine pipi 33.
Hata hivyo, imeelezwa na mmoja wa
wanafamilia kwamba marehemu aliwahi kufungwa mwaka 2008 huko Dubai
baada ya kukutwa na madawa na alimaliza kifungo chake Agosti mwaka huu
na kabla hajamaliza hata mwezi mauti yakamkuta.
Taarifa za kipolisi zinaeleza kwamba
mke wa marehemu alipoulizwa kwamba kipindi cha nyuma mumewe alikuwa
wapi, alieleza kuwa tangu mwaka 2004 alitoweka nyumbani na hakumuaga
alikoenda hadi alipooneka Agosti mwaka huu.
Taarifa zaidi zinapasha kwamba, mkewe
alieleza Septemba 19, mwaka huu mumewe alimuaga kwamba alikua anaenda
Nairobi na hakumweleza anachofuata na alishangaa kusikia kuwa yupo
Newala anaumwa.
Mwenye nyumba anayoishi Nassiri, Gidion
Mpuya alipohojiwa na gazeti hili alisema kwamba siku hiyo ya kifo
hicho alifika nyumbani kwake saa 2.00 usiku na kuwakuta polisi nje ya
geti kuu na hakujua kilichotokea.
“Nilipoingia chumbani kwangu mke wangu
alinieleza kwamba kuna mtu kafariki kwa Nassiri na haikuchukua muda
nikaona gari la polisi linaingia kuchukua mwili, Nassiri na mkewe
wakashikiliwa na polisi.
“Hakukuwa na mtu wa kumuulizia kwa Nassiri bali nilipotoka nje majirani walinieleza kwamba mtu huyo kafariki na madawa tumboni.
“Nassiri ana zaidi ya miaka miwili na
nusu tangu ahamie hapa, alikuwa akiishi na mkewe baadaye
walikorofishana na zaidi ya miezi miwili hakuwepo hapo nyumbani,”
alisema Mpuya.
Aliongeza kuwa mke wa Nassiri alirudi
siku chache kabla ya marehemu kuja hapo kwao na yeye amekuwa akiwaona
wageni wake wakifika na kuondoka lakini hakujua ujio wa marehemu kwani
siku hiyo alifika na hakumalizika hata saa mmoja akafariki dunia.
Kamanda wa Polisi wa Kitengo cha
Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, Kamishna Mwandamizi,
Godfrey Nzowa katika mahojiano na gazeti hili amesema kwamba
wanamshikilia Nassiri na mke wa marehemu.
“Tunaendelea kumtafuta Doto, uchunguzi
unaendelea na utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale
watakaopatikana na hatia,” alisema Nzowa.
No comments:
Post a Comment