KIKUNDI
cha Al Shabaab kimetishia kumwaga damu zaidi Kenya kwa kufanya
mashambulizi mapya na safari hii wanatamba kupiga patakapouma zaidi.
Kundi
hilo limesema kwamba litaongeza idadi ya watu katika kikosi cha
mashambuzi nchini humo kutokana na Kenya kukaidi kuondoa majeshi yake
Somalia.
“Tutaishambulia Kenya sehemu itakayowauma zaidi, tutageuza miji yao makaburi na mito ya damu itatiririka Nairobi nzima,” al Shabaab ilisema katika taarifa yake na kuongeza:
“Uamuzi
wa Serikali ya Kenya kuendelea kuyaacha majeshi yake Somalia ni ishara
ya wazi kwamba, hawajataka kujifunza kutokana na yaliyotokea katika
shambulizi la Westgate,” ilieleza taarifa hiyo huku ikijigamba kuwa,
Kenya itakuwa eneo litakalogubikwa na wingu la damu na vurugu.
Wakati
kikundi hicho kikitoa tishio hilo, takriban miili isiyopungua tisa
imepatikana katika eneo la ndani ya kifusi kwenye jengo hilo, na sehemu
ya eneo liliunguzwa kwa moto wakati wa shambulio hilo la Westgate.
“Baadhi
ya miili haiwezi kutambuliwa kabisa na utambuzi wa vinasaba (DNA)
utafanywa ili kutambua, mingine imeharibiwa na inatisha,” taarifa
kutoka Polisi ilieleza.
Hata
hivyo haikuwekwa wazi kama idadi ya miili hiyo tisa imejumlishwa na
watu 67 wakiwemo wanajeshi sita waliokufa katika shambulizi hilo. Rais
Kenyatta ajibu Hata hivyo Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, juzi
alikaririwa akisema majeshi yake yataendelea kubaki Somalia hadi hapo
amani na usalama wa nchi nchi hiyo vitakapotengamaa.
Septemba
21 Shambulio la Westgate lililotokea Septemba 21 mwaka huu katika jengo
hilo la maduka ya bidhaa mbalimbali za watu wenye maisha ya juu,
wanadiplomasia na wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya Kenya.
Mbali
ya vifo hivyo vilivyofahamika hadi sasa, watu zaidi ya 170 walijeruhiwa
vibaya huku wengine wakipata matatizo ya kisaikolojia. Miongoni mwa
waliouawa ni watoto waliokuwa kwenye tamasha la mashindano ya kupika
kwenye jengo hilo.
Baadhi
ya manusura wa shambulio hilo walieleza namna walivyokutana uso kwa uso
na magaidi hao. Kupitia taarifa mbalimbali, magaidi hao walisikika
wakidai wanawasaka Wakenya na Wamarekani ingawa waliouawa na kujeruhiwa
katika shambulio hilo ni pamoja na raia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo
Ufaransa, Canada, Australia, Marekani, Uingereza, Ghana na kwingineko.
Pamoja
na majeshi na polisi wa Kenya kuzingira jengo hilo tangu saa chache
baada ya tukio, taarifa zinadai baadhi ya magaidi waliokuwa katika
jengo hilo, walitoroka kupitia mtaro wa maji machafu uliokuwa chini ya
jengo hilo na huenda watu wengi zaidi wakawa wamepoteza maisha ikiwemo
mateka waliodaiwa kushikiliwa na magaidi hao ndani ya jengo hilo.
Shambulio
hilo ni la pili kwa ukubwa nchini humo likihusisha kikundi cha al
Shabaab chenye ushirika na al Qaeda ambao wanadaiwa kuhusika na
shambulizi kubwa lililotokea mwaka 1998 katika Ubalozi wa Marekani
nchini humo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 220.
No comments:
Post a Comment