KAWAWA, NKUMBA WADAIWA KUJILIPA MAMILIONI TTB
MJADALA wa Bunge jana jioni ulitawaliwa na kauli nzito baada ya
wabunge kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kutuhumiana kuhusika na
ubadhirifu katika vyama vya ushirika nchini. Hoja
hiyo iliibuka wakati Bunge likijadili muswada wa sheria ya vyama vya
ushirika wa mwaka 2013 uliowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Balozi Christopher Chiza. Aliyekuwa
wa kwanza kuwasha moto huo baada ya mapumziko ya mchana alikuwa mbunge
wa Busega, Dk.Titus Kamati (CCM), ambaye alisema waziwazi kuwa wanasiasa
ndio wezi wa vyama vya ushirika. Dk.
Kamani alihoji ni kwa nini serikali inapata kigugumizi kuwachukulia
hatua wahusika na kusisitiza kuwa hapo kuna kulegalega kumaliza ufisadi
katika ushirika.
“Wanasiasa hawa kwa nafasi zao wameingia kwenye ushirika na
kufanya ufisadi lakini serikali inashindwa kuwachukulia hatua. “Huku
ni kulegalega na ndio maana hata tumeshindwa kuwataja wauza dawa za
kulevya, waziri anaishia kusema tunayo orodha,” alisema. Alihoji
ni kwa nini sasa serikali isiige mfano wa China wa kuwafunga na hata
ikibidi kuwanyonga watuhumiwa wa ufisadi wa vyama hivyo ikithibitika
bila kujali nafasi zao kwenye siasa. Mbunge
wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM), ndiye aliyefuata na kuchafua
hali ya hewa kwa kumtuhumu Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Nchini (TTB)
kufanya ufisadi mkubwa ambao serikali inaujua lakini imeamua
kuunyamazia. Bila
kumtaja kwa jina lakini alikuwa akimlenga mbunge mwenzake wa Namtumbo,
Vita Kawawa, akisema kuwa anajilipa mshahara mara mbili ya ule
uliopitishwa na serikali.
Alisema kuwa analipwa sh milioni mbili za mawasiliano na anachukua
dola 1200 (zaidi ya sh milioni 1.8) kwa ajili nyumba badala ya sh
800,000 zilizoidhinishwa. Mbunge huyo alisema mwenyekiti huyo anayajua mambo hayo na ndiye aliyeidhinisha. “Nina
uhakika na ninachozungumza, waziri nilishamletea taarifa juu ya jambo
hili lakini amenyamaza, hivi hapa tunategemea ushirika utakuwa hai
wakati mabosi wanautafuna?” alihoji. Wakati mbunge huyo anaendelea kuzungumza, Kawawa akitaka kumpa taarifa juu ya jambo analolizungumza. Kawawa
alisema muda wake wa kuwa mwenyekiti kwenye bodi hiyo uliisha Juni 31
mwaka huu, hivyo ni vema mbunge mwenzake akatoa ushahidi wake juu ya
tuhuma za watendaji wa bodi husika. Baada
ya Kawawa kumaliza, Kakosa aliendelea kuchangia ambapo alikataa taarifa
hiyo kwa madai ana ushahidi wa kile kilichofanyika.
Mara baada ya Kakoso kumaliza kuchangia muswada huo, mbunge wa
Kondoa Juma Nkamia alipewa fursa ya kutoa taarifa ambapo alisema tuhuma
zilizotolewa na Kakoso dhidi ya Kawawa ni nzito sana na Bunge lipate
fursa ya kuangalia jambo hilo pamoja na mhusika kutoa ushahidi. Naibu Spika, Job Ndugai, alisema ofisi ya Bunge iko wazi kwa Kakoso kuwasilisha ushahidi wake juu ya kile alichosema. Mara
baada ya Ndugai kutoa ufafanuzi huo, alimpa nafasi mbunge wa Sikonge,
Saidi Nkumba (CCM), ambaye alimtuhumu Kakoso kwa kushindwa kuliambia
ukweli Bunge kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Chama Kilele (APEX) ambacho
kinapigiwa kelele kuwa kinawanyonya wakulima. Alisema
wakiwa Dar es Salaam kwenye vikao vya kamati za Bunge, Katibu wa Apex,
aliitwa katika kamati kama mdau ambapo alipobanwa juu ya wizi
unaofanyika kwenye chombo hicho alisema serikalini ikiiba kelele
zinapigwa lakini APEX ikiiba kidogo kelele zinakuwa kubwa sana.
“Katibu wa Kakoso ndiye aliyetuambia hivyo. Huu ni wizi, sisi
hatuwezi kukubaliana na jambo hilo, serikali haivumilii wizi, huyu
Kakoso anasema APEX ni mkombozi lakini pale Tabora wamewaibia wananchi
bilioni 16, hivi kweli hizi si fedha nyingi? “Hii
APEX ni lazima ifutwe, wenye tamaa ya kwenda kwenye ushirika ni vema
waache siasa, na wenye ushirika ni vema wakabaki huko huko.” Alibainisha
kuwa wizi unaofanyika kwenye vyama vya ushirika unasababishwa na
wanasiasa ambao wana kinga za kisiasa ndiyo maana wanaendelea kutafuna
fedha za wananchi. Mbunge
wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alisema wabunge wana taarifa za wizi
wanatoa taarifa hapa bungeni lakini hakuna wanachokifanya. “Yaani
kila kukicha mnalea wizi halafu leo hii mnaanzisha tume za kuwanyonya
wakulima, kule kwangu wakulima waliuza tumbaku, msianzishe vitu vya
ajabu ajabu…, huu ni wizi mtu, msituletee wizi hapa kwa kubadilisha
majina ya vitu,” alisema.
Tundu Lissu wa Singida Mashariki (CHADEMA) alisema sababu kubwa ya
kuporomoka kwa ushirika ni serikali kuuingilia, kuudhibiti na
kuuporomosha. Alisema
serikali ilianza kuvuruga mambo 1966 sheria za ushirika ilibadilishwa
na msajili wa vyama vya ushirika alipewa mamlaka ambayo alianza
kuyatumia vibaya ambapo mwaka 1976 alipigwa marufuku zikaja bodi za
mazao. Mwaka 1982 vilirejeshwa vyama vya ushirika lakini mamlaka yake yalikuwa yakitolewa na mrajis ambaye ni serikali. Mbunge
wa Nzenga, Andrew Kigwangalah, aliibua upya mzozo wa awali kwa kuanika
nyaraka za ufisadi katika TTB kama ilivyokuwa imedokezwa awali na
Kakoso. Kingwangalah
ambaye alidai kuwa hatarudi nyuma kuwataja mafisadi na wauza dawa za
kulevya alisema kuwa kodi ya nyumba ya mwenyekiti wa bodi inalipiwa
gahara tofauti na ile iliyoidhinishwa.
Alionyesha nyaraka kadhaa za malipo ya viongozi wa bodi hiyo na
kisha kumvaa Nkumba akisema kuwa tatatizo la nchi hii si Apex bali ni
rushwa, wizi, ubadhirifu halafu watu wanaona wizi wanaungalia badala ya
kuchukua hatua. “Waliobaki kwenye ushirika ni wezi watupu, wazalendo wameisha, wezi tunawajua lakini hatuwawajibishi wala kuwachukulia hatua. “Nkumba
ni msaidizi wa Kawawa katika bodi ya tumbaku anajua ukaguzi
haujafanyika na ukifanyika wao hawatasalimika ndiyo maana wanaanza
kuipiga vita Apex. “Kuna
watu wanatumiwa na kampuni za ubebari ambazo zilikuwa zikisafirisha
tumbaku na kusambaza pembejeo, hawa sasa wanaona hatari za kampuni zao
ndiyo maana zinawatumia wabunge ili APEX ifutwe, tuwe makini na wabunge
waovu,” alisema.
Mzozo huo ulidumu huku Kawawa na Nkumba wakisimama kujitetea bila
mafanikio hatua iliyomlazimu Naibu Spika wa Bunge kutoa nafasi kwa
baadhi ya wabunge kuomba viongozi, lakini akaliahirisha Bunge hadi leo
ambapo atatoa uamuzi wake. Mapema
asubuhi, wabunge walipendekeza wabadhirifu wa mali za ushirika
walazimishwe kufidia hasara iliyotokea pamoja na kufilisiwa mali zao. Pendekezo
hilo limetolewa na Nkumba alipokuwa akisoma hotuba ya Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Peter Msolla. Nkumba
alisema ushirika umewakatisha tamaa wananchi kutokana na ubadhirifu wa
viongozi wake hivyo ujio wa sheria hiyo utakuwa mkombozi.
Aliongeza kuwa watuhumiwa wa ubadhirifu wa ushirika wafikishwapo
mahakamani mashauri yake yamekuwa hayathibitiki licha ya taarifa za
fedha kuonyesha kuwa upotevu fedha upo; ni vema kuwepo na utaratibu wa
kuwabana wahusika. Nkumba
alisema vyama vya ushirika vimekuwa vikikaguliwa na Shirika la Ukaguzi
na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) ambalo halifanyi kazi zake
vizuri na kuitaka serikali kuweka utaratibu mzuri ikiwemo kuhusishwa kwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali. Waziri wa Kilimo, Chiza alisema kuundwa kwa sheria hiyo litakuwa suluhisho la matatizo ya ushirika nchini. Alisema
serikali inalenga kuifuta sheria ya vyama vya ushirika namba 20 ya
mwaka 2003 na inaamini sheria mpya itaimarisha, kuendeleza na kuufufua
ushirika. Chiza
alisema sheria ya ushirika ya mwaka 2013 ina lengo la kutekeleza sera
ya maendeleo ya ushirika ya mwaka 2002, inayovitaka vyama vya ushirika
imara, endelevu na vyenye kukidhi mahitaji ya wanachama kiuchumi chini
ya mazingira ya soko huria.
No comments:
Post a Comment