Pages

Translate

Thursday, 12 September 2013

MWIZI WA BODA BODA ANASWA AKIWA AMEJIFICHA KWENYE PAA LA NYUMBA HUKO TEMEKE




MTU anayedaiwa kuwa mwizi wa pikipiki za biashara maarufu kama Bodaboda, hivi karibuni alichomolewa kutoka ndani ya paa la nyumba alikokimbilia kujificha baada ya kuoneshwa bastola ya polisi huko Temeke, karibu na kituo cha mabasi cha daladala cha Bandari jijini Dar.
  Mwizi huyo akitolewa darini.
Tukio hilo lililojaza umati lilitokea baada ya mtuhumiwa huyo kukimbizwa na askari waliokuwa na silaha kufuatia jaribio lake la kupora pikipiki hiyo kushtukiwa.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye jina linahifadhiwa, alisema kuwa mtuhumiwa alipofika nyumbani hapo kwa nia ya kujificha, mikononi mwake alikuwa ameshika visu viwili huku akidai kuwa mwenzake aliyekimbia, ndiye aliyekuwa na  bunduki iliyotumika kumtishia dereva wa bodaboda ili kumnyang’anya pikipiki.
Baada ya kuingia katika nyumba moja iliyo pembeni mwa kituo hicho cha daladala, mtuhumiwa huyo alipanda juu ya dari na kuanza kutambaa akitokomea chumba kimoja baada ya kingine.
Kuona hivyo, wananchi walisaidiana na polisi kumdhibiti.
Mmoja wa askari asiye na sare alipanda juu ya paa hilo na kumwelekezea bastola, akitishia kumlipua kama hatashuka kwa hiyari, kitendo kilichomlazimisha jamaa huyo kutii amri na kuteremka.
Shuhuda huyo alisema kuwa matukio hayo ya uporaji wa pikipiki yamekuwa mengi wilayani Temeke ambapo yamekuwa kero kubwa kwa wananchi, kiasi kilichosababisha mtuhumiwa huyo kupata wakati mgumu kuponyoka.
“Unajua ujambazi umezidi sana hapa Temeke na kuna baa moja kubwa (jina linahifadhiwa) ndiyo wamekuwa wakikaa kwa ajili ya kupanga mipango yao, sisi hivi karibuni tuliibiwa gari lakini tunashukuru Mungu tulilikamata baada ya Fuso moja kuligonga wakati majambazi walipokuwa wakikimbia nalo,” alisema.
Baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo alipelekwa kwenye Kituo cha Polisi cha Chang’ombe lakini Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo alipoulizwa na gazeti hili hatma ya tukio hilo, alisema bado halijafika mezani kwake na kuwa atafuatilia kwa mkuu wa kituo na kutoa ufafanuzi baadaye.

No comments:

Post a Comment