Washington.
Wanasayansi nchini Marekani wamegundua chanjo ambayo wanaamini itaweza
kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa binadamu. Katika majaribio ya
chanjo hiyo, wanasayansi hao wameelezea kuwa imeonyesha mafanikio kwa
kuangamiza kabisa virusi wanaofanana na VVU kwa nyani. Shirika la
Utangazaji la Uingereza (BBC) limechapisha kwenye tovuti yake kuwa baada
ya kubaini hilo sasa wamekusudia kufanya majaribio ya chanjo hiyo kwa
binadamu. Likinukuu taarifa iliyochapishwa kwenye jarida la kisayansi
linaloitwa; Nature, lilimnukuu Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya
Tiba cha Oregon, nchini Marekani akisema walijiridhisha kuwa chanjo
hiyo iliangamiza virusi vyote kwenye mwili wa nyani. Virusi hao jamii
yake inafanana sana na VVU wanajulikana kama Simian Immunodeficiency
Virus (SIV) ikiwa na maana ni virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga
ya kujikinga na maradhi kwa nyani. Taarifa za kisayansi zinaonyesha
kwamba SIV ni virusi ambao wamekuwa wakienea kwa njia ya kujamiiana
miongoni mwa vizazi vya nyani na vilibadilika baada ya kuambukizwa kwa
binadamu vikawa vimezaa VVU. Wanasayansi hao wanasema kati ya nyani 16
waliopewa chanjo hiyo, waliyoipa jina la Cytomegalovirus (CMV),tisa
walipona kabisa maradhi ya SIV. Mtaalamu wa Taasisi ya Chanjo na Jeni
katika Chuo Kikuu cha Oregoni, ambaye alihusika kwenye utafiti huo,
Profesa Louis Picker aliielezea chanjo hiyo kuwa ni ya kutia moyo
ukilinganisha na nyingine ambazo zimewahi kufanyika. “Katika chanjo
nyingi ambazo ziliwahi kuonyesha mafanikio ya kuangamiza virusi ni
kwamba kuna baadhi ya seli virusi walibakia,” alisema Profesa Picker,
akifafanua: “Lakini kwa chanjo hii tulichunguza sehemu nyingi nyeti
katika mwili wa nyani tukagundua kwamba hakuna kirusi aliyebakia.”
Alisema chanjo yao wameiamini kutokana na uwezo wake wa kupenya maeneo
mbalimbali ya mwili kiasi kwamba siyo rahisi kirusi kubakia. Wanasayansi
hao walisema kwa kawaida nyani ambaye ameambukizwa SIV hufa ndani ya
kipindi cha miaka miwili.
No comments:
Post a Comment