WATOTO WANNE WA SHULE YA MSINGI WAMBAKA MWENZAO WA DARASA LA PILI MPAKA KUPOTEZA FAHAMU..!!
MATUKIO
ya uvunjifu wa maadili kwenye shule mbalimbali hapa nchini yameendelea
kushamiri baada ya wanafunzi wanne wa Shule ya Msingi Lulanzi wilayani
Kibaha mkoani Pwani kutuhumiwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili na
kumsababishia maumivu yaliyopelekea kulazwa Hospitali ya Tumbi kwa
matibabu.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi jana babu wa mtoto huyo, Jacob Mrope
alisema tukio hilo lilitokea Septemba 2 saa 6 mchana ambapo mjukuu wake
ambaye ni yatima alikuwa akitoka shuleni huku akiwa na wenzake wawili
wakike, walikimbizwa na watuhumiwa hao ambapo yeye alishindwa kukimbia
kutokana na kuumia mguu na kujikuta akibakwa.
Mrope
alisema kuwa wanafunzi wenzake aliokuwa nao walisema kuwa baada ya
watuhumiwa hao kumkamata walimziba mdomo kisha wakaanza kumuingilia kwa
zamu ambapo mwanafunzi huyo hakuweza kupata msaada wowote hadi
watuhumiwa hao kutimiza haja zao.
"Wenzake
waliokuwa nao walitoa taarifa nyumbani kwa mlezi wake ambaye ni dada
yake ambapo alikwenda na kumkuta akitokwa na damu nyingi na alipomuuliza
alisema kuwa wenzake wamembaka ndipo alimchukua na kumpeleka shuleni
kutoa taarifa," alisema Mrope.
Kwa
upande wake dada yake Lwiza alisema kuwa yeye alipata taarifa kupitia
kwa wanafunzi hao ambao alikuwa nao wakati wanatoka shule na kukimbizwa
na watuhumiwa hao, ambapo walisema kuwa ilibidi warudi na kumkuta
mwenzao akitokwa damu, wamkokota mwenzao hadi nyumba iliyojirani na
kumjulisha.
"Alikuwa
kwenye hali mbaya kwani alikuwa akitokwa na damu nyingi na
nilipomuuliza alisema kuwa amebakwa na mtuhumiwa ambaye alimtambua na
kumtaja jina mwenye umri wa miaka 10 akiwa na wenzake watatu," alisema
Lwiza.
Lwiza
alisema kuwa baada ya kuona hali ile walimpeleka shule na uongozi wa
shule ukamwelekeza kufuata taratibu za kisheria ambapo walikwenda
Serikali ya mtaa kisha kwenda polisi na baadaye Hospitali ya Tumbi kwa
matibabu zaidi ambapo hadi juzi mwanafunzi huyo alikuwa bado kalazwa na
hali yake inasemekana kuwa ni mbaya.
Naye
Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Lulanzi, Anna Bilali alisema kuwa wao
kama uongozi wa shule hawawezi kusema lolote kwani suala hilo liko
kwenye vyombo vya sheria pamoja na kitabibu na watakuwa tayari kusema
mara taarifa zitakapokamilika.
"Ni
kweli tukio hili limetokea lakini bado haijathibitishwa kama ni kweli
au la na pia lilitokea nje ya shule na muda wa shule kwa wanafunzi wa
madarasa ya chini walisharuhusiwa kurudi nyumbani mara baada ya masomo
kwisha," alisema Bilali.
Akizungumzia
tukio hilo mjumbe wa mtaa wa Lulanzi, Rasul Shaban alisema kuwa
walipata taarifa hiyo na kushangazwa na kitendo hicho ambapo tukio hilo
ni la mara ya kwanza kutokea katika shule hiyo ambayo iko kwenye mtaa
huo na pia walitoa barua za kuwadhamini wanafunzi wanaotuhumiwa kufanya
tukio hilo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa hadi sasa wanawashikilia wanafunzi wanne wenye umri kati ya miaka 10 na 13 kuhusiana na tukio hilo.
Source: Majira

No comments:
Post a Comment