Pages

Translate

Thursday, 22 August 2013

MTANGA ADAI MTOTO WA KIKE DILI


BILA shaka wasomaji wa Staa na Mwana mko poa kabisa, kama kawa tunakutana hapa kuzungumza na mastaa ambao tayari wamebarikiwa kupata watoto.
Leo tunaye msanii wa komedi anayeuza sura kupitia Runinga ya EATV, Hamisi Changale ‘Mtanga’ ambaye kwa sasa analea kichanga cha miezi miwili kupitia kwa mkewe, Liganice Benny Tamba.
Staa na Mwana: Vipi Mtanga uko poa?
Mtanga: Niko poa bwana, ulezi tu kwa sasa kama unavyoona. Shughuli zangu kidogo zinasuasua.
Staa na Mwana: Kawaida ya watoto wachanga huwa wanapenda kulialia, wa kwako vipi?
Mtanga: Wangu mimi halii, lakini kutwa nzima ananuna hata hacheki, tabu tupu!
Staa na Mwana: Unaye huyohuyo mmoja?
Mtanga: Nina watoto wawili, huyu Shadiya (miezi miwili) na dada yake Nadiya (miaka 6) utamwona muda si mrefu, akirudi kutoka dukani.
Staa na Mwana: Kwa upande wako unapendelea zaidi watoto wa kiume au wa kike?
Mtanga: Watoto wote ni sawa ila wa kike nawapenda zaidi, mtoto wa kike dili. Anaolewa unakula mpunga. Hata akienda mbali kutafuta maisha, atapata moyo wa huruma kurudi kunisaidia, tofauti na wa kiume.
Staa na Mwana: Huyo mwanao wa kwanza (Shadiya) unamsomesha shule zile za gharama au hizi za kawaida? Samahani lakini.
Mtanga: Hahaha! Yupo chekechea, anasoma shule ya gharama kidogo ili apate muongozo wa lugha, ila shule ya msingi nitampeleka shule za ‘Kayumba’ ili akapate muongozo bora wa elimu na tabia nzuri, halafu nikiona amenyooka nitakapeleka shule za bei mbaya hapo baadaye.
Staa na Mwana: Kwani katika shule za gharama, watoto hawafundishwi maadili?
Mtanga: Siyo kama shule za Kayumba, huko wanapelekwa kijeshi zaidi hakuna ulegelege, tofauti na shule za kulipia wanadekezwa sana, lazima ajifunze kula mihogo, huko atakula makaroni tu.
Staa na Mwana: Unapenda watoto wako waje kuwa na wadhifa upi hapo baadaye?
Mtanga: Wawe miongoni mwa wapiganaji katika nchi hii, hata mwenyewe nitajiona kweli nimezaa na ndiyo maana najitahidi kuwapatia malezi bora.
Staa na Mwana: Huyu kichanga umefanana naye sana, ila huyu mkubwa hamuendani kabisa umepakaziwa nini?
Mtanga: Mimi kidume bwana, siwezi kuchakachuliwa hata siku moja. Hii damu yangu kabisa, kamebadilika siku hizi tu, kalivyokuwa kadogo nilikuwa nimefanana nako sana (akatoa picha ya utotoni ya Shadiya). Si unakaona kalivyokuwa kadogo ‘kopi laiti’.
Staa na Mwana: Unafikiri yupo atakayerithi fani yako?
Mtanga: Hilo siyo la kuuliza, huyu mkubwa  naona atanirithi kabisa, halafu atakuwa muimbaji sababu anapenda kufuatilia vipindi vya muziki na filamu mpaka usiku wa manane.
Staa na Mwana: Mtanga nikushukuru, hongera na pole ya kulea.
Mtanga: Nashukuru, karibu tena.

No comments:

Post a Comment